Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipi tutarajie albamu ya sita ya Harmonize

Muktasari:

  • Albamu hiyo inakuja ikiwa ni miaka 10 tangu Harmonize alipotoka rasmi kimuziki baada ya kusainiwa na WCB Wasafi, lebo ambayo alifanya nayo kazi kwa miaka minne.

Dar es Salaam. Zimesalia takribani wiki mbili kabla ya Harmonize kuachia albamu yake ya sita tena chini ya Konde Music Worldwide, albamu ambayo kwa sehemu imevuka mipaka ya kihistoria katika biashara ya muziki.  

Albamu hiyo inakuja ikiwa ni miaka 10 tangu Harmonize alipotoka rasmi kimuziki baada ya kusainiwa na WCB Wasafi, lebo ambayo alifanya nayo kazi kwa miaka minne.

Hivyo anaenda kuungana na mastaa wengine Bongo waliotoa albamu, na Extended Playlit (EP) kwa mwaka huu, nao ni Darassa (Take Away The Pain), Jay Melody (Addiction), Lady Jaydee (Silver) n.k.

Upande wa EP kuna Jux (A Day To Remember), Mbosso (Room Number 3), Nedy Music (The Voice of The Island), Lava Lava (Time), Yammi (After All), Phina (Melanin Therapy) n.k.

Kwa mujibu wa Konde Music, albamu hiyo inatarajiwa kutoka Novemba 31, 2025, hatua itakayopelekea staa huyo kuwa na rekodi ya kipekee Bongo ya kuachia albamu kwa miaka sita mfululizo!.

Harmonize, mkali wa kibao cha Single Again (2023), tayari ameachia albamu kama Afro East (2020), High School (2021), Made For Us (2022), Visit Bongo (2023) na Muziki wa Samia (2024).

Kila albamu ilifanya vizuri kwa nafasi yake, mathalani Visit Bongo (2023) ilishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023 kama Albamu Bora ya Mwaka.

Na hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kushinda kipengele hicho kufuatia kuwania mara mbili mfululizo na kuangukia pua kupitia albamu zake, High School (2021) na Made For Us (2022).

Kulingana na Harmonize mwenyewe, albamu hii ya sita ameiandaa kwa utulivu mkubwa kiasi kwamba anaamini ina hadhi ya kushinda tuzo kubwa za muziki duniani za Grammy!.

Mbali na hilo, kati ya mambo tunayotarajia kutoka katika albamu hiyo, ni kolabo mbili za nguvu ambazo bila shaka mashabaki wengi wana kiu ya kuzisikia kutokana na kuvuka mipaka ya kihistoria ya wasanii hao.

Kolabo hizo ni zile alizofanya na Alikiba kutokea Kings Music, na Mbosso, msanii mwenzake wa zamani pale WCB Wasafi ambapo walikaa pamoja kwa takribani miaka miwili kisha Harmonize akaondoka.

Kufanya kazi na wasanii hao ina maana kubwa kwa Harmonize na tasnia kwa ujumla kwani ameonyesha ukomavu wa kibiashara katika muziki na sio kuongozwa na hisia hasi.

Wakati akiwa WCB Wasafi mshindani wao alikuwa ni Alikiba na Kings Music yake, ni wazi kipindi hicho hili lisingeweza kutokea, lakini sasa yupo nje ya Wasafi, kaacha mambo yao na yeye akafungua ukurasa wake.

Hivyo hivyo kwa Mbosso, wakati yupo WCB Wasafi mshindani wao alikuwa Harmonize na Konde Music yake, ila kufuatia kuachana na lebo hiyo, ameamua kufanya kazi na Harmonize bila kujali historia ya awali.

Hata hivyo, kumekuwa na maswali mengi kwa muda sasa  kwanini wasanii wanapoondoka WCB Wasafi huwa wanakimbilia kufanya kazi na washindani wa lebo hiyo au Diamond?.

Harmonize ni msanii wa pili aliyeondoka WCB Wasafi na kuja kushirikiana na Alikiba baada ya Rayvanny aliyempa shavu mwimbaji huyo katika wimbo wake ‘Naoa’ kutoka katika albamu yake, The Big One (2024).

Ni wazi kuwa nyimbo alizorekodi na Alikiba na Mbosso ndizo zitaongozwa kwa kusikilizwa (streaming) na mashabiki wengi katika majukwaa ya kidijitali kitu ambacho kitaipa zaidi heshima albamu hiyo.

Hiyo ni kwa sababu ya historia yao kama nilivyoeleza, pili, wote wana nguvu ya mashabiki mtandaoni, mathalani EP ya Mbosso, Room Number 3 (2025) ndani ya mwezi mmoja ilisikilizwa zaidi ya mara milioni 50.

Ukiachana na hilo, pia huwenda kolabo yake mpya na Abigail Chams, Lala (2025) ikajumuishwa katika albamu hiyo, ikiwa ni kolabo yao ya nne baada ya kutoa, Closer (2022), Leave Me Alone (2022) na Me Too (2025).

Ikumbukwe kabla ya Harmonize kuanza kutoa mfulizo wa albamu, alianza na EP, Afro Bongo (2019) iliyobamba sana kutokana na kushirikisha wasinii wazito kama Diamond, Yemi Alade, Mr. Eazi na Burna Boy.

Matarajio ya mashabiki
Akizungumzia ujio wa kazi hiyo ya Harmonize, Saadam Mwanza mkazi wa Mwenge, Dar es Salaam amesema  hategemei na hatopenda kukuta kazi ambazo tayari zimeshatoka zikiwa zimejaa kwenye albamu hiyo.

“Unajua hawa wasanii wetu huwa wanatuchezea ubongo. Anatoa kazi unajipanga kabisa unatumia bando lako kuipakua lakini ajabu unakutana na nyimbo mbili au tatu tu ndiyo mpya nyingine zote ni zilezile ambazo zilitoka zamani. Sitafurahi kukuta hivyo,” amesema

Kwa upande wake Happyness Jovin mkazi jijini humo anasema kazi nzuri ni desturi ya Harminize hivyo anasubiri kwa hamu ujio wa kazi hiyo.

“Huyo kijana wa Kimakonde nisiwe muongo ni mzuri sana kwenye kuandika na hata melodi kwa hiyo naimani albamu haitakuwa kinyonge. Lakini nadhani kazi ambayo ataachia na Mbosso itafanya vizuri zaidi kwani wote wapo vizuri,” amesema Happyness.