Koffi ajitupa kwenye siasa DR Congo

New Content Item (1)

Mwanamuziki mkongwe Afrika, Koffi Olomide ametangaza kuwa atagombea nafasi ya usenata nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa nchini humo kutokana na upinzani uliopo na unatarajiwa kufanyika Aprili 21, 2024.

Koffi ambaye anatajwa kama mwanamuziki mwenye mafanikio makubwa zaidi nchini DR Congo, amesema atagombea eneo la Sud- Ubangi  lililopo Kasikazini mwa Congo, akiwa na chama chake kipya cha AFDC-A, ambacho kinaongozwa na  Modeste Bahati Lukwebo.

Koffi mwenye miaka 68, anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo ikiwa mwaka 2022, aliteuliwa kuwa Balozi wa Utamaduni wa Congo na Rais wa nchi hiyo, Felix Tishisekedi ambaye alimpa pasipoti ya Kidiplomasia kutokana na cheo hicho.

Koffi ambaye jina lake kamili ni Antoine Christophe Agbepa Mumba, alikuwa mwanamuziki wa Congo wa tatu kupewa pasi hiyo, wengine ni  Maître Gim na Dadju.

Mwanamuziki huyo ambaye ameshiriki muziki zaidi ya miaka 40,  nyimbo zake zimekuwa zikiwavutia mashabiki wengi Afrika akihojiwa juzi alisema anataka kugombea ili kuwasaidia Wacongo.

“Nimeisaidia Congo. Nimeitangaza Congo kile mahali duniani kupitia muziki wangu kila mahali ambapo nimekuwa nikipita watu wamekuwa wakinieleza kuwa wananiona nakwenda kuwa seneta siku moja.

“Nafikiri hii ni nafasi sasa na kuwasaidia watoto na kina mama wa hapa Congo,” alisema mwanamuziki huyo ambaye hapa nchini amewahi kufanya nyimbo na Diamond Platnium na Nandy.


 Koffi ambaye baba yake ni Mcongo na mama amezaliwa Sierre Leone, ana mafanikio makubwa akiwa ameshatwaa tuzo sita za Kora, nne kati ya hizo akiwa msanii anayejitegemea ambazo zimemfanya kuweka rekodi ya kipekee duniani.

Koffi anakwenda kufuata nyayo za wanamuziki wengine wengi wa Afrika ambao wameingia kwenye siasa baada ya kuwa maarufu kwenye muziki, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Joseph Haule (Profesa Jay),  Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’  ambao walipata umaarufu kwenye muziki na kwenda kwenye siasa kwa upande wa Tanzania.

Upande wa Kenya anafuata nyayo za Jackson Ngechu Makini, maarufu kama  Prezzo, ambaye aligombea kwenye uchaguzi wa Kenya mwaka 2022.

Staa huyo wa Hip Hop aliingia kwenye siasa mwaka 2019, mwingine ni mwanasiasa wa Uganda  Bob Wine ambaye amegombea urais mara kadhaa nchini Uganda akiwa anatajwa kuwa mpinzani mkubwa wa Rais wa sasa Yoweri Museveni.

Mwingine ni mbunge wa Jimbo la Starehe nchini Kenya,  Charles Njagua Kanyi ‘Jaguar’ ambaye aligombea kupitia Chama cha  Jubilee Party na kushinda.