Kontawa anatembea na nembo ya kitaa
Muktasari:
- Unakuta mtu yupo migodini achimba madini lakini akipata pesa, akiingia mtaani watu watakunywa na kufanya kila kitu halafu pesa ikiisha anarudi tena chimboni, hayo ndiyo yalikuwa maudhui yangu.”
Kuna wakati unaweza kufananisha muziki na michezo ya bahati nasibu, kwa sababu wapo wasanii wakali na wenye ‘voko’ za hatari mtaani na licha ya kujituma kwenye muziki lakini bado hawajatusua.
Mbali na hao wapo wale ambao baada ya kuchanga kete bahati ikawadondokea, ngoma moja tu ikawatambulisha mtaani na kusikika kila kona.
Wengine baada ya kujaribu zaidi ya mara moja mitaa ndiyo ikawaelewa, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mwanamuziki Kontawa ambaye licha ya kujitafuta kwenye muziki kwa muda mrefu, mapokezi ya wimbo wake uitwao ‘Champion’ yalikuwa ya tofauti sana.
Mwaka mmoja uliopita Kontawa aliachia ‘Champion’ ambayo iligusa washikaji wengi mtaani, mistari yake aliiandika na mashabiki wakaielewa, akajikuta anapata wafuasi wengi zaidi wa kazi zake.
Mkali huyo akaendelea kushikilia palepale mashabiki wanapopataka, bila ya kupoteza ramani. ‘Haso’ zake za kitaa zikaendelea kutamba kwenye ngoma zake zilizofuata ikiwemo ‘Shida’, ‘Dunga Mawe’, ‘Wewe’, na nyinginezo.
Kontawa anaiambia Mwananchi kuwa tungo zake zinawagusa watu wengi hasa wanaojitafuta kitaani kwa vile anachokiandika hata yeye amewahi kukipitia.
“Kinachonisukuma kuandika mistari ya aina hiyo ni kwa sababu na mimi nimeishi maisha hayo, hivyo mara nyingi naimba maisha yangu yaliyopita na ya sasa hivi, huwa najizungumzia mwenyewe kwa hiyo naamini uhalisia wa maisha yangu huwa unazungumzia maisha ya watu wengi sana,” amesema Kontawa.
Licha ya kutoa ngoma nyingi zenye mistari ya kuwagusa vijana kitaani wenye maisha ya chini, Kontawa ametolea mfano mistari iliyopo kwenye wimbo wake uitwao ‘Wewe’ ambao umetoka miezi mitatu iliyopita.
“Maudhui makuu ya kwenye wimbo wangu wa ‘Wewe’ ni washikaji au watu ambao tunafanya kazi ngumu sana lakini tukiokota hela matumizi yetu yanakuwa ya kusahau kile ambacho tumetoka kukifanya.
“Unakuta mtu yupo migodini achimba madini lakini akipata pesa, akiingia mtaani watu watakunywa na kufanya kila kitu halafu pesa ikiisha anarudi tena chimboni, hayo ndiyo yalikuwa maudhui yangu.”