Kumbe Bieber alikataa ofa ya Usher kutumbuiza Super Bowl

Muktasari:

  • Kabla ya tukio la Jumapili iliyopita, kulizuka uvumi katika mitandao ya kijamii uliodai marafiki hao wa muda mrefu watapanda jukwaani pamoja katika onyesho hilo lililohudhuriwa na watu 65,000, huku mamilioni wakilitazama kupitia mitandao mbalimbali.

Marekani. Imefichuka kuwa Usher Raymond IV alimuomba Justin Bieber ili watumbuize pamoja kwenye onyesho lake la Super Bowl wiki iliyopita lakini Bieber hakuwa tayari kwa ofa hiyo licha ya ukaribu wao wa miaka mingi.

Kabla ya tukio la Jumapili iliyopita, kulizuka uvumi katika mitandao ya kijamii uliodai marafiki hao wa muda mrefu watapanda jukwaani pamoja katika onyesho hilo lililohudhuriwa na watu 65,000, huku mamilioni wakilitazama kupitia mitandao mbalimbali.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Page Six, Usher alijitahidi sana kumshawishi Bieber ashiriki lakini mkali huyo wa wimbo 'Baby' hakuwa tayari kutokana na sababu ambazo bado hazijawekwa wazi.

"Hakuna jambo mbaya kati ya Usher na Justin Bieber, hakuwa tayari kwa hilo, hakuwa akijisikia." chanzo kimoja cha kuaminika kutoka tasnia ya muziki kiliiambia Page Six.

Usher ambaye inasemekana alifunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Jennifer Goicoechea huko Vegas muda mfupi baada ya onyesho hilo, alikuwa na mchango mkubwa katika kutoka kimuziki kwa Bieber na kuitangaza chapa yake.

Alimsaidia kijana huyo kupata umaarufu duniani kote akiwa na umri wa miaka 13 tu baada ya kipaji chake kugunduliwa na mwanamuziki maarufu Scooter Braun, na punde Usher na Bieber waliimba pamoja wimbo, Somebody to Love (2010).

Kabla ya kipindi cha mapumziko cha Super Bowl, shabiki mmoja aliandika kwenye mtandao wa X kwamba Bieber na Usher wangetumbuiza na kutoa burudani yenye uwezo wa kutatua tatizo la njaa duniani, kumaliza ongezeko la joto, kusafisha bahari na kujenga vijiji.

Lakini badala yake, Usher aliwaleta jukwaani mastaa wengine kama Alicia Keys na H.E.R na kutumbuiza pamoja na bendi kwa ustadi mkubwa.

Kwa mujibu takwimu zilizotolewa mapema Jumatatu, onesho hilo la Usher lilikuwa limeangaliwa na watu zaidi ya milioni 30 duniani.

Hadi sasa onyesho la Super Bowl linaloshikilia rekodi ya kutazamwa zaidi ni la Rihanna (2023), hili limepata watazamaji milioni 121.01, likifuatiwa na la Katy Perry (2015) - watazamaji milioni 121, kisha nafasi ya tatu ni la Lady Gaga (2017) - watazamaji milioni 117.

Ikumbukwe Bieber amekuwa hatumbuiza sana tangu alipogundulika ana ugonjwa wa Ramsay Hunt ambao hapo Septemba 2022 ulimfanya afute maonyesho yake yote yaliyokuwa yamesalia katika ziara yake, Justice Tour.

Mbali na kupata upele wenye maumivu, ugonjwa wa Ramsay Hunt unaweza kusababisha kupooza kwa uso na kupoteza uwezo wa kusikia. Wakati huo, Bieber aliandika kwamba ziara hiyo ilimletea madhara makubwa ya kiafya.

Lakini mapema mwezi huu, alitumbuiza mubashara katika klabu moja huko Toronto, Canada ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuonekaa jukwaani kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Justin Bieber, mshindi wa tuzo mbili za Grammy alivuma duniani na albamu yake ya kwanza, My World 2.0 (2010) iliyoshika namba moja Billboard 200 na kumfanya kuwa msanii mdogo zaidi kuongoza chati hizo baada ya miaka 47. Albamu hiyo ndiyo iliyotoa wimbo wake maarufu 'Baby' akimshirikisha Ludacris.