Lifahamu kundi la BTS litalowasha jukwaa Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Kundi la BTS ambalo awali lilijulikana kama ‘Bangtan Sonyeondan’ likiwa na maana ‘Bulletproof Boy Scouts’ lilianzishwa rasmi mwaka 2010 chini ya kampuni ya Big Hit Entertainment (HYBE) huku mwanzilishi wake akiwa ni Bang Si-hyuk.
Korea. Kwa zaidi ya miaka 10, jina la BTS limeendelea kutikisa ulimwengu wa muziki. Huku kundi hilo kutoka South Korea likiweka rekodi ambazo awali zilionekana kuwa ngumu kufikiwa na wasanii wa Asia.
Kundi la BTS ambalo awali lilijulikana kama ‘Bangtan Sonyeondan’ likiwa na maana ‘Bulletproof Boy Scouts’ lilianzishwa rasmi mwaka 2010 chini ya kampuni ya Big Hit Entertainment (HYBE) huku mwanzilishi wake akiwa ni Bang Si-hyuk.
Kabla ya kundi hilo kuzinduliwa rasmi, vijana kadhaa walifanyiwa majaribio ya kujiunga na BTS. RM ambaye jina lake halisi ni Kim Nam-joon alikuwa mwanachama wa kwanza kujiunga na kundi hilo.
RM alikuwa tayari anafahamika kwenye underground hip-hop scene ya Seoul kutokana na uwezo wake mkubwa wa rap. Baadaye akaungana na Suga pamoja na J-Hope ambao nao walikuwa na historia kubwa kwenye rap na dansi. Wengine waliofuatia ni Jin, Jimin, V pamoja na Jungkook ambaye ndiye msanii mdogo zaidi kwenye kundi hilo.
Safari yao haikuwa rahisi walianza kufanya mazoezi kwa miaka kadhaa huku wakikabiliwa na changamoto za kifedha. Kutokana na hali zao za kiuchumi waliamua kuishi pamoja kwa muda mrefu ili waweze kufanya mazoezi usiku na mchana kwa lengo la kuingia kwenye tasnia ya muziki.
Hatimaye Juni 13,2013 walijitosa rasmi katika tasnia ya muziki wakiachia albamu yao ya kwanza iitwayo ‘2 Cool 4 Skool’. Huku wimbo wao wa kwanza ukipewa jina la ‘No More Dream’.
Tofauti na makundi mengine ya K-pop yaliyokuwa yanaimba kuhusu mapenzi, BTS waliamua kuzungumzia presha za maisha, mfumo wa elimu wa Korea Kusini, matarajio ya wazazi na ndoto za vijana.
Jambo ambalo lilifanya nyimbo zao kuwagusa na kukubalika zaidi na vijana wengi wanaopitia changamoto kama hizo. Hata hivyo kutokana na kutoka kwenye kampuni ndogo, BTS hawakupewa nafasi kubwa kwenye vyombo vikubwa vya habari na mara nyingi nyimbo zao zilipuuzwa ukilinganisha na makundi yaliyokuwa chini ya kampuni kubwa za K-pop kama SM Entertainment na YG Entertainment.
Aidha moja ya vitu vilivyowasaidia BTS kukua kwa haraka na kutambulika duniani kote ni mitandao ya kijamii. Tofauti na makundi mengine kwa upande wao walitumia mitandao yote ya kijamii kuchapisha video, picha, livestreams na maisha yao ya kawaida, hali iliyowafanya kujizolea mashabiki duniani kote, mashabiki ambao walipewa jina la ‘ARMY’.
Maisha ya kundi la BTS yalianza kubadilika kuanzia mwishoni mwa 2015 hadi 2016 baada ya kuachia albumu mfululizo kama ‘The Most Beautiful Moment in Life (HYYH)’.
Albamu ambazo zilibeba nyimbo zenye ujumbe kuhusu maisha ya ujana, maumivu, ndoto pamoja na changamoto za maisha, huku wimbo wa ‘Dope’ ukitikisa zaidi. Kisha kundi hilo kuanza kuingia kwenye chati za muziki za Marekani ikiwemo Billboard 200.
Umaarufu wao uliendelea kupanda kupitia albamu yao ya WINGS kisha mwaka 2018 iliandika hostoria kupitia albamu yao ya Love Yourself: Tear kuwa albamu ya kwanza ya kundi la Korea Kusini kushika namba moja kwenye Billboard 200 nchini Marekani.
Mafanikio hayo yaliifanya BTS kuwa sura mpya ya muziki wa K-pop duniani. Kundi hilo lilianza kufanya ziara kubwa duniani, kujaza viwanja vikubwa na kushinda tuzo nyingi za muziki kimataifa.
Pia kwa wakati huo walifanikiwa kupewa nafasi katika kutoa hotuba kwenye sehemu mbalimbali ikiwemo katika shirika la United Nations (UN) wakihamasisha vijana kujipenda na kujiamini kupitia kampeni yao ya “Love Myself” kwa kushirikiana na UNICEF.
Mwaka 2020 BTS waliingia kwenye kiwango kingine cha mafanikio kupitia wimbo wao wa Kiingereza Dynamite. Wimbo huo uliwawezesha kuwa wasanii wa kwanza wa K-pop kushika nafasi ya kwanza kwenye Billboard Hot 100 na pia walipata nomination yao ya kwanza kwenye Grammy Awards.
Nyimbo kama “Butter”, “Permission to Dance” na “Boy With Luv” nazo ziliendelea kuvunja rekodi za YouTube, Spotify na majukwaa mengine ya muziki duniani.
Umaarufu wao ulizidi kuongezeka hadi kufikia hatua ya kutembelea White House nchini Marekani kujadili masuala ya chuki dhidi ya watu wa Asia pamoja na umuhimu wa utofauti na usawa.
Mwaka 2022 BTS walitangaza mapumziko ya shughuli za pamoja ili wanachama wake waweze kutekeleza huduma ya lazima ya kijeshi nchini Korea Kusini. Mwanachama wa kwanza kwenda jeshini alikuwa Jin kabla ya wengine kufuata. Katika kipindi hicho kila mwanachama aliendelea na kazi zake binafsi za muziki, matangazo na ushirikiano na kampuni mbalimbali duniani.
Aidha BTS walirejea kuungana tena kama kundi kamili mwaka 2025 baada ya wanachama wote kukamilisha huduma ya lazima ya kijeshi nchini South Korea. Baada ya kuungana waliingia studio ambapo walitengeneza albumu ya comeback iliyopewa jina la ‘Arirang’ ambayo iliachiwa Machi, 2026 ikibeba nyimbo kama Swim, 2.0, Body to Body.
Hata hivyo inaelezwa kuwa kwasasa wanajiandaa kufanya ziara kubwa ya dunia (world tour) inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni. Huku kwa siku zijazo wakijiandaa kukiwasha katika fainali ya Kombe la Dunia la FIFA 2026 akiungana na mastaa kama Shakira na Madonna.
Kundi la BTS limefanikiwa kunyakuwa tuzo zaidi ya 700 duniani kote, jambo linalowafanya kuwa moja ya wasanii waliopata tuzo nyingi zaidi katika historia ya muziki wa kisasa.
Wakishinda tuzo kama Billboard Music Awards ambazo mpaka sasa wamebeba 10, American Music Awards (AMAs), MAMA Awards, Melon Music Awards na Golden Disc Awards, lakini pia wameingia kwenye Guinness World Records kwa zaidi ya mara 20 kwa rekodi za mitandao ya kijamii, YouTube na streaming.