Lulu: Namtamani Jay Dee lakini..

Muktasari:

  • Katika mahojiano yake na Mwananchi, Lulu Diva ambaye kwa sasa anatamba na kibao cha ‘Mtaalam’ alichomshirikisha Nandy, alijikuta akiyasema hayo baada ya kuulizwa kuwa mwaka jana ulikuwa mzuri kwa wasanii wa kike kufanya kolabo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo ilionekana zaidi kwa wanaume.

Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Lulu Abbas’Lulu Diva’, amesema anatamani kufanya kazi na dada Komando, Lady Jay Dee, lakini anafikiria aanzie wapi.

Katika mahojiano yake na Mwananchi, Lulu Diva ambaye kwa sasa anatamba na kibao cha ‘Mtaalam’ alichomshirikisha Nandy, alijikuta akiyasema hayo baada ya kuulizwa kuwa mwaka jana ulikuwa mzuri kwa wasanii wa kike kufanya kolabo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo ilionekana zaidi kwa wanaume.

Kutokana na hilo, tulitaka kujua kutoka kwake kama ana mpango wowote wa kufanya kazi na wasanii wa zamani wa kike na katika majibu yake, alisema anatamani nafasi hiyo haswa kwa Ray C na JayDee.

Hata hivyo, alisema mchakato wa kumfikia Ray C, umeanza na wimbo ambao angependa kufanya naye kazi ni ule wa ‘Uko Wapi”

Wakati kwa upande wa Lady Jay Dee, ambaye jina lake halisi ni Judith Wambura, alisema anaona kuna kipengele kidogo kwa kuwa msanii huyo ni mkali na hivyo haitakuwa kazi rahisi kumfikia haraka.

“Naomba tu huko alipo ajue kuwa mdogo wake nina hamu ya kufanya naye kazi, ila bwana mimi ni mkali lakini yeye ni mkali zaidi hivyo nafikiria namuanzaje anzaje,” alisema Lulu.

Kuhusu wasanii wa kike sasa kuanza kufanya kazi pamoja, Lulu alisema ni jambo zuri na wakati mwingine akitaka wasilaumiwe kwa kuwa huenda kazi mtu anayoifanya  unakuta hamhitaji msanii wa kike kwa muda huo.


Atamani prodyuza, Director wa kike

Katika hatua nyingine, Lulu ambaye pia ni msanii wa filamu, alisema anatamani kuona maprodyuza wa kike na waongozaji wa kike katika kazi za muziki kama ilivyo kwa upande wa tasnia ya filamu.

Msanii huyo alisema waongozaji kama wakina Lamata, Jenifer Kyaka, Irene Paul, wameonyesha kuwa wanawake wanaweza katika upande wa filamu, hivyo kuwataka wa aina hiyo pia kwenye upande wa muziki.

Hata hivyo, anasema moja ya changamoto anayoiona kwa wanawake kushindwa kuingia huko, inatokana na aina hiyo ya kazi inavyofanywa na kueleza kuwa wanawake wanatumia hisia zaidi huku wanaume wakitumia nguvu.

“Kutokana na hilo, utakuta prodyuza mwanamke akiudhiwa kidogo tu na msanii, anasusa, lakini hii haipo kwa wanaume, japokuwa isiwavunje moyo bali wajifunze wenzao wanafanyaje hadi kuyakabili hayo,” anasema Lulu.