Mabadiliko kundi la Weusi baada ya Nikki wa Pili kuwa DC

Mabadiliko kundi la Weusi baada ya Nikki wa Pili kuwa DC

Muktasari:

  • Kundi la Weusi limesema kutakuwa na mabadiliko katika kundi hilo baada ya mmoja wa wasanii wake, Nickson Simon maarufu Nikki wa Pili kuteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.


  

Dar es Salaam. Kundi la Weusi limesema kutakuwa na mabadiliko katika kundi hilo baada ya mmoja wa wasanii wake, Nickson Simon maarufu Nikki wa Pili kuteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.

Juni 19, 2021 Rais wa Tanzania, Samia Suluhu alimteua Nikki kuwa mkuu wa wilaya hiyo akichukua nafasi ya Jokate Mwegelo ambaye amehamishiwa Temeke, Dar es Salaam.

Nikki wa wakuu wengine wa wilaya waliapishwa jana Juni 21, 2021 na mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge na kuwataka kujifunza mara moja mazingira ya kazi, kutatua kero za wananchi na kuja na vipaumbele vya wilaya husika.

Akizungumza baada ya Nikki kuapishwa, Joh Makini ambaye ni kaka wa mkuu huyo wa wilaya amesema mdogo wake alikuwa msemaji wa kundi, kwa sasa ni vigumu kuendelea na majukumu hayo kutokana na majukumu yake mapya.

"Kuna vitu vitabadilika kwa sababu anaenda kulitumikia Taifa pale Kisarawe, hatuwezi kusema ataendelea kuwa msemaji wa Weusi kwa sababu anayo majukumu mengine makubwa ambayo sisi tunamsapoti pia. Kwa hiyo tunaweza kuangalia namna ya kufanya mambo mengine ili yeye awe huru zaidi kufanya kile kitu ambacho ameteuliwa kukifanya ambacho ndicho muhimu kwa sasa" amesema Joh Makini.

Kwa upande wake G Nako amesema, "Itakuwa mapema sana kuzungumza kama kutakuwa na mabadiliko baada ya Nikki kupata majukumu ya kiserikali, lakini mabadiliko yatakuwepo kwenye muziki wa Weusi.”

Kuhusu uwezo wa Nikki katika uongozi, Joh Makini amesema ni moja ya ndoto zake na anaamini ana uwezo, kikubwa ni kumuombea kwa Mungu amzidishie hekima na maarifa ili akatende haki katika kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande wake Lord Eyes amesema, "Nikki nilikuwa namuona kwenye uongozi, hivyo sikushangaa ila nilifurahi sana, namuombea kwa sababu uongozi ni zaidi ya kutaka au kupenda, atumie mifano iliyopo nchini ili kuwa bora zaidi.”

Mwaka 2020 mmoja wa wasanii wa kundi hilo, Bonta alitia nia ya kuwania Ubunge Kahama Mjini anapofanya kazi ya udaktari, hata hivyo hakufanikiwa kupita katika kura za maoni. Wasanii wengine wa kundi hilo ni Joh Makini, G Nako, Lord Eyes na Nikki wa Pili.