Mambo kumi kuhusu Q Chief
Muktasari:
- Sauti yake yenye mvuto wa kipekee ilimfanya kutambulika kama mmoja wa 'vocalists' bora, sasa anaheshimika kama msanii mwenye kipaji cha hali ya juu anayejua kutunga na kuimba kwa ustadi. Fahamu zaidi.
Dar es Salaam. Mkongwe wa Bongofleva, Abubakar Katwila almaarufu Q Chief ni miongoni wasanii wenye sauti ya kipekee na waliowahi kutamba sana katika muziki kupitia miondoko ya R&B na Afro Pop, pamoja na uwezo wake mkubwa wa kuimba live.
Sauti yake yenye mvuto wa kipekee ilimfanya kutambulika kama mmoja wa 'vocalists' bora, sasa anaheshimika kama msanii mwenye kipaji cha hali ya juu anayejua kutunga na kuimba kwa ustadi. Fahamu zaidi.
1. Q Chief alianza kupenda muziki kipindi anaishi na mama yake nchini Botswana alipokuwa akifanya kazi, lakini alipoanza kusoma madrasa kukamfanya kuelezwa zaidi muziki kabla ya kuja kurekodi.
2. Wimbo wa Q Chief 'Aseme' aliurekodi kufuatia kifo cha mama yake mzazi, Khadija ambacho kilitokea wakiwa wote Botswana ambapo alienda kuishi huko kufuatia kutengana kwa wazazi wake.
3. Wakati Q Chief anatoa albamu yake ya kwanza 'Mwana Mnyonge' mkurugenzi wa E FM Redio, Majizzo ndiye alikuwa meneja wake akishirikiana na Aboubakar Sadiq, mtangazaji wa Redio One.
4. Q Chief ndiye aliyempeleka Shilole studio kwa C9 ambapo alimlipia Sh300,000 kwa ajili ya kurekodi na kuja kutoka kimuziki, ikiwa ni baada ya kucheza filamu 'First Decision' akiwa na Ray Kigosi, Irene Uwoya na kadhalika.
5. Q Chief ni msanii wa pili Bongo kufanya kazi na mtayarishaji muziki kutoka nchini Kenya, Dunga wa Mandugu Digital pindi alipoaza kufanya kazi zake Bongo.
Dunga ndiye alitengeneza wimbo maarufu wa Q Chief 'My Boo' ambao Harmonize alikuja kuurudia, huku pia akimshirikisha mkongwe huyo.
6. Mbali na Q Chief, Dunga aliyeleta muziki wa Bounce, alifanya kazi na wasanii wengine - Professor Jay (Hapo Vipi), Noorah (Ladha Tamu), Black Ryno (Happy), Mh. Temba (Nipe Mimi), Nakaaya Sumari (Mr. Politician) nk.
7. Marehemu Ruge Mutahaba ndiye alimuomba Q Chief kuwaruhusu Linah na Barnaba kurudia wimbo wake 'Nikilala Naota' ambao alirekodi na Lady Jaydee.
Ruge alimueleza Q Chief na yeye anatakiwa kushiriki katika wimbo huo ili kusaidia wasanii hao kukua kimuziki, ombi ambao alilikubali pia.
8. Wimbo wa kundi la Top Band linaloundwa na Q Chief na TID, 'Nilikataa' wakimshirikisha Mr. Blue, ulirekodiwa na Marco Chali ila mixing na mastering alifanya Master J.
9. Q Chief ndiye msanii wa kwanza wa Bongofleva kufanya kazi na staa wa Nigeria, Patoranking kisha wakafuata wengine kama Diamond Platnumz, Navy Kenzo, Rich Mavoko na Alikiba.
10. Kwa miaka takribani 25 ndani ya Bongofleva, Q Chief amefanya kazi na watayarishaji muziki wengi ila Allan Mapigo aliyetengeneza wimbo wake 'Uhali Gani' ndiye anatamani kurekodi naye tena siku za mbeleni.
Hiyo ni sawa na Banana Zorro ambaye alimtaja Allan Mapigo kuwa miongoni mwa watayarishaji wake bora wa muda wote. Wengine ni Enrico Figueiro, Bizman na Miikka Mwamba ambaye ndiye alimtoa kimuziki na ngoma yake, Mama Yangu (2003).