Mapenzi longolongo yalizaliwa Pwani

Muktasari:

  • Kwa mfano binti na mamaye walinufaika kwa mafao ya kujikimu kutokana na ubwege wangu. Uongo unaweza kusaidia kuepusha shari, kuokoa maisha, kujenga uchumi wa mtu na kadhalika. Lakini amini usiamini upo uongo wa burudani tu.

Zamani zile nilipokuwa nikianza kujitegemea nilikutana na binti mwenye asili ya mikoa iliyo kando ya Bahari ya Hindi. Alikuwa anaishi  jirani na njia niliyoitumia kurudi nyumbani nitokapo kazini. Alinifurahisha kwa uchangamfu wake,  tukajenga mazoea ya kutoka ikiwamo mwisho wa juma. Na ilifikia mahali tukatambulishana kwa wazazi wetu kama marafiki.

Alikuwa akiishi na mama yake aliyekuwa na vyuo vitano vya ndoa (Wanapwani wananielewa). Nikawa namsaidia bint baadhi ya mambo ya kielimu na mama yake pia kwa kuwa hakuwa anafanya shughuli yoyote ya kuaminika.

Tukaanza kufungua milango ya uchumba. Kwa wazazi hakukuwa na pingamizi, tena mama yake alilishangilia wazo hilo kwa kuona bintiye atatua kwenye mikono salama. Lakini mimi kabla ya kupeleka posa nilifanya tathmini katika urafiki wetu, nikagundua mapungufu. Wanasema ukimchunguza bata hutamla, kweli ilikuwa hivyo.

Kila nilipopita nyumbani kwao ninaporudi k kazini, nilimkuta ameketi ngazini akijisomea. Lakini nilipokwenda tofauti na muda huo sikumkuta. Mama alinihakikishia kuwa yupo jirani na  kunisukumia nikamsubiri nyumbani. Miaka hiyo wabongo hatukuwa tunatumia simu za viganjani, hivyo tulitafutana kwa kope.

Siku moja sikumkuta mama nyumbani na binti hakuwapo. Nilimtuma mdogo wake wa mwisho akamsake, nikampa na motisha ya shilingi mia (siku hizo ilinunua soda na chenji ikarudi). Baada ya muda binti alikuja lakini hakupenda kuniona pale. Alibeba madaftari mawili na mfuko wa ‘rambo’. Nilitaka kumpokea mizigo lakini alikataa katakata kupokelewa hata madaftari. Nilijiuliza kwa nini amekuwa mkali kupokelewa madaftari.

Alipongia ndani waligombana sana na mdogo wake. Mimi kwa kuwa machale yalikwishanicheza, nikawekeza zaidi kwa mdogo wake. Siku moja nilimtia mia mbili akaniletea yale madaftari. Kumbe moja lilikuwa la vikoba vya mama na jingine la kliniki ya dada! Nilipomwongeza mia mbili tena, dogo alinipeleka mtaa wa pili ambako nilimfumania akifua mashuka uwani kwa njemba lake. Nilifunika kombe kumnusuru dogo asiuawe na mama.

Wabongo tunathamini sana uongo maishani mwetu, wakati mwingine unasaidia, kuna wakati hausaidii.

 Kwa mfano binti na mamaye walinufaika kwa mafao ya kujikimu kutokana na ubwege wangu. Uongo unaweza kusaidia kuepusha shari, kuokoa maisha, kujenga uchumi wa mtu na kadhalika. Lakini amini usiamini upo uongo wa burudani tu.

Kuna usemi maarufu wa ‘fundi mkweli ni kinyozi pekee’. Watu walifanya utafiti kwa mafundi wa aina zote, wakagundua zaidi ya kinyozi hakuna mkweli. Kwa mfano fundi mshoni, kwanza anajiita ‘fundi cherehani’ ilihali hatengenezi cherehani. Huyu unampelekea kitambaa na pesa ya kushonea, anakuahidi uifuate kesho. Kumbe ameshapanga akukabidhi keshokutwa na maneno ya ‘jana nilichelewa msibani’.

Uongo huu upo sana huku pwani, ambapo mtu hufurahi kuona mwenziye anaingia mkenge kwa uongo wake.

Masikhara yakiwa mengi umakini unapungua. Wakati mwingine mkuu hata akiwa siriaz watu wanachukulia masikhara. Bila shaka Serikali ilijifunza mambo hata ikaamua Makao Makuu ya Serikali kuondolewa Dar es Salaam. Hata Wakuu wa Mkoa wanaohudumu hapa hupata shida sana, wakati mwingine inawabidi wawe wanachimba mikwara badala ya kutoa maelekezo.

Maradhi haya yameenea katika nchi nzima. Fikiria Tanesco wanavyotuongopea bila sababu wakati tatizo la umeme si la Tanzania pekee. Wenzetu wamekuwa wakweli juu ya kushindwa gharama za kufua umeme wa gesi, wakaongeza nguvu za jua ambapo gharama zake ni za ziada. Sisi badala ya kuongezewa nguvu za jua tunaongezewa ‘nguvu za giza’, halafu kila kukicha zinapigwa saundi za migawo, mara maji yamepungua... mara maji yamefurika...

Gharama kitu gani. Kwani mlivyopandisha bei ya bia tuliacha kulewa? Au mnavyopandisha nauli tunaacha kusafiri? Leteni umeme sisi tutajua namna ya kubana matumizi. Tunawezaje kuishi na unga robo tushindwe umeme? Tena mjue mnatuchanganya sana na migawo ya umeme wakati nauli zipo juu. Wenyewe tulishafungua magoli yetu ya sebuleni ili tuokote hizo buku-buku za nauli halafu nyie mnazingua. Wakati fulani hapa tulipewa sera ya elimu ya bure lakini tunagharamia nauli, madaftari, sare, twisheni, mitihani hadi chakula. Afadhali basi shule iwe na bima ya afya kwa wanafunzi wake, lakini wakiumwa tunagharamia tena. Gharama za kusomesha kwa staili hii ni sawa na shule inayolipwa ada kubwa lakini mtoto anapata madaftari, sare, twisheni, mitihani, chakula na matibabu bure. Tena analala humohumo. Ndio mana nasema wabongo longolongo ni “hobby” yetu.