Master J: Wasanii wanapaswa kuwekeza, siyo kuonesha utajiri wao
Muktasari:
- Kutokana na hilo mtayarishaji mkongwe wa muziki nchini Joachim Kimario ‘Master J’ wakati alipokuwa kwenye mahojiano na Iroc amewataka wasanii chipukizi kuanza kujitambua na kufikiria namna mpya ya kusimamia fedha zao.
Dar es Salaam. Katika tasnia ya muziki imekuwa desturi kwa wasanii kuonyesha magari ya kifahari, mtindo wa maisha pamoja na mitoko katika klabu za usiku lakini ni nadra sana kuona wanafanya uwekezaji kwa ajili ya maisha yao ya mbeleni.
Kutokana na hilo mtayarishaji mkongwe wa muziki nchini Joachim Kimario ‘Master J’ wakati alipokuwa kwenye mahojiano na Iroc amewataka wasanii chipukizi kuanza kujitambua na kufikiria namna mpya ya kusimamia fedha zao.
“Nilipokuwa nikisaini na Wagosi, hakukuwa bado na majukwaa ya kidijitali. Muziki ulikuwa unapatikana zaidi kupitia wasambazaji kutoka India. Wakati huo walinipa malipo ya awali ya shilingi 100 milioni na hapo ndipo nilipoanza kwa mara ya kwanza kushughulika na fedha kubwa. Baada ya kupata, nililazimika kuwa makini kusimamia na kudhibiti fedha,”alisema.
Aidha aliongezea kwa kuweka wazi kuwa elimu yake na kujitambua mapema kulimuokoa na utumiaji wa fedha hovyo huku akidai kuwa anajutia sana kununua magari saba, ikiwemo gari jipya lililogharimu dola 67,000.
“Ninajutia hilo kwa sababu baadaye nilijifunza kuhusu uwekezaji, mali huweka fedha mfukoni mwako, madeni huiondoa. Nakumbuka miongo mitatu iliyopita nilinunua zaidi ya viwanja 100.
"Viwanja hivyo hivyo, ambavyo awali vilikuwa vinauzwa kwa shilingi 1 milioni kila kimoja, leo hii vinaweza kufikia hadi shilingi 900 milioni. Ukiuza kiwanja kimoja leo, mtoto wako anaweza kusoma kwa amani. Usiweke tu fedha benki nunua ardhi,”alisema.
Aidha wakati wa mahojiano hayo naye mwanamuziki Marioo aliunga mkono hoja hiyo huku akithibitisha kuwa wasanii wengine wakubwa, akiwemo Diamond Platnumz, wamewekeza kwenye ardhi, akiwahimiza wanamuziki chipukizi waige mfano huo.
Hata hivyo, Master J akizungumza kuhusu muziki amesisitiza kuwa kipimo cha kweli cha mafanikio ya Bongo Fleva hakipo tu kwenye nyimbo zinazoongoza chati au matamasha bali kwenye kujua namna ya kuthibiti fedha zao pamoja na uimara katika muziki.
“Ukinunua ardhi leo, kesho thamani yake inaongezeka, hivyo basi wasanii wa Bongo Fleva wanapaswa kuwekeza, na siyo tu kuonesha utajiri wao,”amemalizia.