Mfahamu Madilu System msanii aliyetamba kwenye rhumba
Muktasari:
- Madilu Multi System, msanii aliyezaliwa kwenye maisha ya kawaida na kugeuka kuwa ngome ya uimbaji, kipenzi cha mashabiki na mwimbaji, alilitikisa jiji la Kinshasa kwa muziki mzuri na sauti yake tamu.
Congo. Katika historia ya muziki wa rhumba kutoka DRC Congo, kuna majina mengi yaliyowahi kuvuma na kupotea. Lakini jina mojawapo ambalo limesalia hadi leo kwenye muziki wa Congo, Madilu.
Madilu Multi System, msanii aliyezaliwa kwenye maisha ya kawaida na kugeuka kuwa ngome ya uimbaji, kipenzi cha mashabiki na mwimbaji, alilitikisa jiji la Kinshasa kwa muziki mzuri na sauti yake tamu.
Safari yake haikuwa na mafanikio ya haraka. Ilijaa misukosuko, maumivu, usaliti na hakukata tamaa licha ya magumu aliyopitia na baadaye akaibuka shujaa.
Hadi sasa ni miaka 18 tangu mwanamuziki huyo afariki dunia Agosti 11, 2007.
Mwananchi linakuchambulia misukosuko ya mkali huyo wa zamani ambaye hakukata tamaa hadi ndoto zake za kuwa mwanamuziki mkubwa zilipotimia.
HISTORIA YAKE
Jina lake halisi ni Jean de Dieu Makiese. Alizaliwa Mei 28, 1950 mjini Leopoldville kwa sasa Kinshasa, kipindi ambacho DRC Congo ilikuwa bado chini ya utawala wa Wabelgiji.
Madilu alikulia kwenye mji uliojaa kelele za muziki, idadi kubwa ya bendi na ushindani mkali uliowafanya vijana wengi kuwa na ndoto ya kuwa wanamuziki.
Katika miaka ya 1960, Madilu alikua kijana mkorofi, mwenye ndoto nyingi na shauku ya kuwa kwenye jukwaa. Ndani ya Kinshasa kwa wakati huo muziki wa Rhumba ulitawala na kuwa ndio maisha ya watu.
ASILI YA JINA LAKE
Mwaka 1969 akiwa na umri wa miaka 19, alijiunga na bendi ya Orchestra Simba. Hapa alijifunza msingi, nidhamu na sauti. Baadaye alifanyakazi na Bamboula ya Papa Noel, kisha Festival de Maquisard akiwa na mkongwe Sam Mangwana.
Mwaka 1971, alijiunga na bendi ya Fiesta Popular ya Mfalme wa Rhumba, Fagus Izeidi. Hapa ndipo historia ya jina lake ilipozaliwa, lakini kabla ya hapo, Jean alikuwa bado ni kijana wa kawaida mwenye ndoto zisizo na muelekeo, aliimba tu kama kujifurahisha nafsi yake.
Fagus aliamua kumpa jina la kisanii James kutokana na umaarufu wa msanii wa Marekani, James Brown, akachukua na neno Madhi lenye asili ya India ilikiwa na maana ya mchawi mkuu.
Lakini Madilu alitamani jina lake litokane na utu wake akaondoa herufi 'h' kwenye madhi ikabaki Madi kisha akaongeza 'lu' kutoka kwenye neno Bialu. Hapo ndipo jina Madilu lilipozaliwa na baadaye akajiongezea System likiwa na maana ya alama ya usanii, akili na ubunifu.
MISUKOSUKO YA MUZIKI
Mwanzoni mwa mwaka 1970, Madilu pamoja na wenzake wawili, Yossa Taluki na Pires waliondoka Fiesta Popular na kuanzisha kikundi chao kilichoitwa Bakuba Mayopi.
Ni kama walianza upya kwenye muziki na miaka sita baadaye waliibuka na kibao cha Pamba-Pamba kilichofanya vizuri na kuwatambulisha DRC Congo nzima kama wanamuziki wapya wa Rhumba.
Lakini mambo hayakuwa mazuri kwani ngoma moja pekee ndio ilifanya vizuri hivyo Madilu akaamua kuondoka na kuunda bendi yake mwenyewe iliyoitwa Orchestra Pamba Pamba na msanii mwenzie Soki Vangu mwaka 1976.
Miaka miwili ya bendi hiyo haikuzaa matunda. Haikupata 'hit song' hata moja, hapo ndio kwanza palimrudisha nyuma badala ya kumpa umaarufu kama ambavyo yeye alitarajia.
Mwaka 1978, akaamua kuondoka akajiunga na kundi la Tabu Ley Rochereau wakati huo alikuwa wa moto kweli kweli ambaye kwa hapa Bongo kwa sasa unaweza kumfananisha na Diamond Platnumz wa lebo ya Wasafi.
Katika bendi ya Tabu Ley iliyokuwa inaitwa Afrisa International, Madilu hakua tena staa. Alikuwa mwimbaji aliyepungua thamani, aliyefunikwa na kivuli cha Tabu Ley. Kwa miaka miwili, alihangaika kutafuta nafasi yake bila mafanikio. Ndipo tukio lililovunja moyo wake likatokea.
ALIACHWA AIRPORT
Tukio la kuachwa kwenye uwanja wa ndege ni tukio lililomuumiza kwenye maisha yake na aliwahi kuhadithia kwenye vyombo mbalimbali vya habari, ambalo lilitokea mwaka 1980 wakati huo anaendelea kujitafuta ili aweze kurudi kwenye ubora wake.
Bendi hiyo ilitakiwa kusafiri kwenda Ulaya mwaka 1980. Madilu akaambiwa afike kesho yake uwanja wa ndege kwa ajili ya safari hiyo.
Basi unaambiwa hakulala usiku kucha akiamini ndoto zake za kwenda Ulaya zinatimia akafika mapema uwanja wa ndege, akasubiri… akasubiri…wee kimya, hadi ndege ikaanza kupaa, lakini bosi wake Tabu Ley hakutokea kumpa taarifa yoyote.
Madilu alisimama na kutazama ndege ikiruka, ikimuacha akiwa hajui hatma yake wala wapi anakwenda, mbaya zaidi alikuwa anawaza atawaambia nini vijana wenzake aliowatambia kwamba umasikini basi kwani anakwenda kuyasaka maisha bora Ulaya.
Hilo lilikuwa tukio lililomjeruhi moyo wake kwa miaka mingi na ndipo likampa hasira ya kupambana kuhakikisha ndoto zake zinatimia.
Baada ya tukio hilo mwanamuziki Ntesa Dalienst alimpeleka kwa Franco Luambo Makiadi na mwaka 1980 akajiunga na bendi ya TPOK Jazz.
Hapo alikaa miaka mitatu bila kusikika, akifanya viitikio vya nyimbo na kuonekana kama mwimbaji wa kawaida tu. Bosi wa bendi hiyo, Franco hakumuamini tena.
Unaambiwa usimkatie tamaa mtu ambaye anatafuta kwa jasho na anayeamini kile anachokipenda.
WIMBO WA NON UKAMFUNGULIA
Mwaka 1983, Franco alitaka wimbo 'Non' ambao ulihusu matatizo ya ndoa uimbwe na wasanii wawili, Josky na Ntesa, lakini hao wawili waliukataa kwa kuhofia kufungiwa.
Sasa wakati Franco yuko Ulaya alimuita Madilu hotelini na kumwambia anaweza kuimba wimbo huo? Basi hapo ndipo kulimrejesha mwamba huyo baada ya kuimba ndio inakawa njia yake.
Ndipo jina Madilu System likarejea tena, kazi yake na Franco ikazalisha vibao vikubwa kama Mamou, Marion, Mario (reprise) na nyingine nyingi.
Miaka sita baadaye Franco alifariki dunia mwaka 1989, na bendi ya TPOK Jazz iliyumba. Simaro Lutumba alianzisha Bana OK mwaka 1994, lakini Madilu hakufuata kundi hilo akaamua kubaki na kuendelea kufanya kazi zake mwenyewe.
Hapo aliachia albamu kama Sans Commentaire (1994), Album ’95
L’Eau, Pouvoir, Tenant du Titre, Bonheur, La Bonne Humeur (2007) na nyinginezo.
Ngoma zake kali kama Apula, Si Je Savais Ca, Ya Jean, Pie Mboyo, Franco de Mi Amor, Blessure d'Amour na Nzele, ni kati ya ambazo zinaendelea kukonga nyoyo za wapenda burudani kila zinapochezwa.
KIFO CHAKE
Madilu alifariki dunia Agosti 11, 2007 huko Kinshasa, DRC, kwenye hospitali ya Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 55.
Umauti ulimkuta miezi michache tu baada ya kuiingiza sokoni albam yake ya mwisho iliyoitwa Bonne Humor.
Kuhusu chanzo cha kifo chake, ripoti za wakati huo zilisema kuwa alifariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo baada ya kulazwa hospitalini kwa matatizo ya kiafya aliyokuwa akikabiliana nayo kwa muda.
FAMILIA/ UTAJIRI
Madilu alikuwa ameoa na alikuwa na watoto kadhaa. Taarifa za majina yao hazikuchapishwa sana kwenye vyombo vya habari, kwa kuwa familia yake ilikuwa ya maisha ya faragha.
Pia hakuna rekodi rasmi ya kiwango cha mali au utajiri wake.