Mitupio ya fasheni ndani ya Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Licha ya michuano la kombe hilo ilipoanza kufunguliwa kwa 2026 kuwa na burudani ya kutoasha kutoka kwa mastaa mbalimbali akiwamo Rayvanny, Shakira, Burna Boy na wengineo. Lakini pia suala la fasheni na mitindo ya mavazi imeendelea kutawala viwanjani.
Marekani. Kwa kawaida Kombe la Dunia huwavutia watu kutoka maeneo mbalimbali duniani kutokana na mabao ambayo timu hutandikana uwanjani.
Licha ya michuano la kombe hilo ilipoanza kufunguliwa kwa 2026 kuwa na burudani ya kutoasha kutoka kwa mastaa mbalimbali akiwamo Rayvanny, Shakira, Burna Boy na wengineo. Lakini pia suala la fasheni na mitindo ya mavazi imeendelea kutawala viwanjani.
Wakati michuano ya timu mbalimbali ikiendelea kupambania kombe hilo, wabunifu wa mavazi, kampuni za fasheni na hata mashabiki kutoka mataifa mbalimbali wamekuwa wakitoka na mitupio mbalimbali.
Katika viwanja mbalimbali vya Marekani, Canada na Mexico, baadhi ya mashabiki wameonekana wakiwa wamejichora nyuso na miili yao kwa rangi za bendera za mataifa yao. Wengine wakiwa wamevaa kofia za ajabu, miwani zilizochorwa.
Miongoni mwa picha na video zilizosambaa zaidi ni za shabiki mmoja mwanamke ambaye ni shabiki wa Mexico. Kuibuka uwanjani huku kichwa kizima akiwa amekipamba kwa bendera za nchi ambazo timu zake zinashiriki kwenye kombe hilo yaani kachomeka kama vibanio.
Mwonekano wake ulivutia mamia ya watu duniani huku wengi wakimsifia kwa kuzifanya bendera kuwa sehemu ya fasheni. Yaani sio poa!
Mbali na shabiki huyo kati ya timu ambayo iliyotikisa duniani kwa fasheni ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Pale ambapo wachezaji wa timu hiyo walipowasili nchini Marekani kwa ajili ya michuano ya hilo huku wakiwa wamevalia suti nyeusi zenye kisha upande wakati kukiwa na kitambaa chenye michoro ya chui.
Pamoja na mabegi makubwa yenye michoro hiyo hiyo. Ndani ya dakika chache picha zao zilikuwa zimesambaa Instagram, TikTok na X. Ilikuwa balaa tupu
Suti hizo zilibuniwa na mbunifu Alvin Junior Mak ambaye kupitia mavazi hayo alitaka kufikisha ujumbe wa nguvu, ujasiri na ustahimilivu unaowakilishwa na chui katika utamaduni wa Kongo.
Uruguay nayo haikubaki nyuma. Mbunifu maarufu Gabriela Hearst alitengeneza sare maalumu za timu hiyo kwa kutumia sufu ya merino inayozalishwa nchini humo.
Kila vazi lilikuwa na mwonekano wa kipekee unaoelezea historia na urithi wa taifa hilo. Kwa kifupi ni kwamba wachezaji walionekana kama mabalozi wa utamaduni katika nchi yao.
Aidha nchini Hispania, kampuni kubwa ya Loewe ndiyo ilikuwa na jukumu la kuwavisha wachezaji wa timu za taifa za wanaume na wanawake. Mavazi yao tu ya safarini yalikuwa ya kibosi sana kama vile wanaenda kwenye maonesho ya Paris Fashion Week lakini kumbe ni kwenye michuano ya soka.
Makocha hawakubaki nyuma
Kocha wa Ujerumani Julian Nagelsmann alivutia kwa mavazi yake yenye mvuto. Alivalia fulana kali yenye kola ambayo aliifunga vifungo vyote. Mtindo huo ulifanya aanze kujadiliwa kwenye mitandao ya kijamii
Kwa upande mwingine, kocha wa Japan Hajime Moriyasu aliwashangaza wengi kwa kuendelea kuvaa suti na tai licha ya kuwa na joto kali Texas. Watu wengi walijiuliza alikuwa anapata wapi nguvu za kuvumilia hali hiyo ya hewa na lile vazi lake kama afisa mkuu wa benki.
Wakati huohuo, kampuni kubwa kama Nike na Adidas zimeendelea kutumia mashindano haya kama jukwaa la kibiashara. Nike imevutia watu wengi kupitia ushirikiano wake na wabunifu mbalimbali pamoja na kampeni yake kubwa iliyowashirikisha mastaa wa michezo na burudani duniani.
Adidas nayo ilivutia kwa ushirikiano wake na mafundi wa Mexico waliotengeneza jezi. Hayo yote yanaonesha kuwa fasheni katika michezo hutumika kuonesha tamaduni za mataifa mbalimbali.
Hata hivyo, mwanamuziki Drake kupitia chapa yake ya NOCTA naye aliingia kwenye mjadala huu kwa kutengeneza toleo maalumu la jezi za Canada. Jezi hizo ni moja ya bidhaa zilizotafutwa zaidi na vijana.
Kilichoonekana wazi katika Kombe la Dunia 2026 ni kwamba mpira wa miguu hauhusishi tu mchezo wa dakika 90. Limegeuka kuwa biashara, burudani, utamaduni na sehemu ya kuonesha fasheni.
Unaweza kusema mitandao ya kijamii imeongeza nguvu katika mabadiliko haya. Na pengine huo ndio jambo kubwa wa Kombe la Dunia la mwaka huu. Yaani kila mtu anapata anachotaka wakati wengine wakihesabu mabao na pointi za makundi, wengine wanatazama mavazi bora, wabunifu bora na mashabiki waliovaa wakanoga zaidi.