Mjue Dr Nico mwamba wa gitaa la solo

Muktasari:
- Mwaka 1953 akiwa na umri wa miaka 14 tu alijiunga na kundi maarufu la African Jazz chini ya mkongwe Joseph Kabasele, toka akiwa mdogo ubora wake katika kupiga gitaa ulionekana, wapenzi awali wakampa jina la Nico Mobali au Mwanaume Nico, baadaye ndipo akapewa jina la Dr Nico linaloendelea kudumu mpaka leo kwenye vichwa vya watu walioupenda muziki wake.
Miaka thelathini na tisa imepita toka Nicholaus Kasanda wa Mikalay, maarufu kwa jina la Dr Nico alipofariki. Dr Nico alikuwa mpiga gitaa la solo na mtunzi mzuri sana, alizaliwa tarehe 7 Julai 1939 katika eneo la Mikalay, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati huo ikiitwa Belgian Congo.
Mwaka 1953 akiwa na umri wa miaka 14 tu alijiunga na kundi maarufu la African Jazz chini ya mkongwe Joseph Kabasele, toka akiwa mdogo ubora wake katika kupiga gitaa ulionekana, wapenzi awali wakampa jina la Nico Mobali au Mwanaume Nico, baadaye ndipo akapewa jina la Dr Nico linaloendelea kudumu mpaka leo kwenye vichwa vya watu walioupenda muziki wake.
Mwaka 1960 wakati Kongo imo katika harakati za mwisho za kupata uhuru, bendi ya African Jazz ilitoa kibao kilichoitwa Independence Cha Cha, Dr Nico akiwa anapiga gitaa la solo wakati kaka yake Dechaud akiwa kwenye gitaa la rithimu, kibao hicho murua kilikuja kuwa kama ndio wimbo wa Taifa wa Uhuru wa Kongo.
Wakati Dr Nico anajiunga na African Jazz mwaka 1953 walikuweko wanamuziki wengine waliokuja kutoa mchango mkubwa katika kutambulika kwa muziki wa Kongo. Walikuwemo akina Isaac Musekiwa, huyu alikuwa na asili moja na King Michael Enoch, Michael Enoch alikuwa mwanamuziki aliyechangia sana umaarufu wa bendi za Dar es Salaam Jazz Band, Dar es Salaam International Orchestra na Mlimani Park Orchestra.
Isaack na Michael wote walitoka Kusini mwa Tanzania, Musekiwa alisema alitoka Southern Rhodesia, nchi inayojulikana sasa kama Zimbabwe na Michael Enoch alitoka Northern Rhodesia inayojulikana sasa kama Zambia.
African Jazz pia walikuwepo akina Roger Izedi, Balonji Tino Baroza, Charles Mwamba Dechaud kaka yake na Dr Nico,Tabu Ley, Joseph Mulamba Mujos, majina yaliyokuja kutawala muziki wa Kongo katika miaka ya sitini na sabini.
African Jazz lilikuwa kundi la kwanza la muziki wa rumba kutumia neno Jazz kwenye jina lao, jambo ambalo hatimaye lilikuja kuwa utamaduni wa kila bendi kujiita Jazz Band. Wanamuziki wengi wa miaka hiyo hapa Tanzania walijiita majina ya hawa wanamuziki maarufu wa African Jazz, walikuweko wanamuziki wa Kitanzania waliojiita Mujos, Baroza, Izedi na kadhalika.
Mwaka 1963, kundi kubwa la wanamuziki wa African Jazz wakajitenga kutoka kwa Joseph Kabasele na kuanzisha kundi lao la African Fiesta Orchestra. Dr Nico akiwa kwenye gitaa la solo na Tabu Ley akiongoza kwenye uimbaji, moto mkali uliwashwa Africa nzima.
Muziki wa kipindi hicho mpaka leo bado unapendwa, nyimbo kama Bougie ya Motema, Salam Aleikum, Biatondi ya Kasanda na kadhalika bado zinakonga nyoyo za wapenzi wa rumba hata leo bara lote la Afrika.
Mwaka 1965 Novemba 16 kukatokea mpasuko mkubwa, African Fiesta ikameguka na kukatokea makundi mawili, African Fiesta Sukisa chini ya Dr Nico na African Fiesta National chini ya Tabu Ley. Dr Nico akabaki na kaka yake Charles Mwamba “Dechaud”, na akina Pierre Bazeta, André Lumingu aliyejulikana zaidi kama “Zoro”, Victor Kasanda “Vixon”, Joseph Mingiedi “Jeff”, PEDRO, Josky Kiambukuta .
Mwaka 1966 Kundi la African Fiesta Sukisa chini ya Dr Nico lilifanya ziara Tanzania na kupiga muziki Dar es Salaam katika Ukumbi wa Arnatogro, nilibahatika kuwa nje ya Ukumbi wa Arnatougro wakati wakiporomosha wimbo maarufu wa Hommage ya Lumumba uliokuwa na kibwagizo kilichokuwa kikitaja marais wote wa Afrika wakati ule, ‘Afrika muzima wanalia, Lumumba wa Kongo, President Nyerere analia Lumumba wa Kongo, President Mobutu analia….’
Bendi hii pia ilifanya onyesho Morogoro lakini kulitokea majanga, bendi ilifanya uhuni na kukatisha dansi mapema baada ya wanamuziki kupata wasichana wapenzi. Mkuu wa mkoa wakati huo aliingilia kati na kuwalazimisha waendelee kupiga muziki mpaka saa tisa ya usiku au la angewaweka ndani, walilazimika kuendelea na dansi, na mwisho wa dansi walisindikizwa na polisi mpaka mpakani mwa mkoa.
African Fiesta Sukisa pia ililirekodi nyimbo kadhaa katika studio za RTD, ukiwemo wimbo wa TANU Yajenga Nchi na pia walirekodi wimbo Hommage ya Lumumba.
Mwanzoni mwa miaka ya 70 kundi la African Fiesta Sukisa lilikuwa kati ya makundi pendwa ya muziki wa Kongo, kundi hili pia hupewa sifa ya kuwa ndio walioanzisha staili ya kupiga gitaa la second solo, kaka yake Dr Nico, Charles Dechaud ndiye huaminika kuwa alianzisha mfumo wa second solo, pia bendi hii inasifika kwa kuutambulisha mtindo wa Mutwashi, mtindo uliotokana na ngoma ya kabila la Wakasai ambalo ndilo kabila lake Dr Nico.
Kufikia mwanzoni mwa miaka ya 80 nguvu ya kundi hili ilianza kufifia na hasa baada ya afya ya Dr Nico nayo kuanza kuyumba. Agosti 1985 hali ya Dr Nico ilikuwa mbaya sana kiasi cha Rais Mobutu kutoa amri ya mwanamuziki huyo kusafirishwa kwenda kutibiwa Ubelgiji. Muda mfupi baada ya kupokelewa hospitali ya St Luc ya Brussels, Nicholaus Kasanda wa Mikalay akakata roho, ilikuwa tarehe 22 Septemba mwaka 1985.
Hakika mpaka leo upigaji gitaa la solo wa Dr Nico haujapata mpinzani, kuna wakati Wakongo walifikia mpaka kumuita Mungu wa gitaa. Lala Pema Nicholaus Kasanda.