Mondi kabakisha kulinda brandi yake tu

Muktasari:

  • Mawazo ni moja ya mapini ya mwanzo ya Mondi. Baada ya balaa lile la kwanza kama Nenda Kamwambie, Mbagala na Nitarejea. Nataka kulewa, Moyo wangu na hili la Mawazo. Linatosha kumvisha nishani msela huyu.

Kama wivu ninao na roho yangu inaumia, kweli wapendanao ndiyo maadui zikitimia... Utu wangu na thamani, ina maana kweli hakuvijua... Licha ya burudani, ya mapenzi yangu akatimua... 

Mawazo ni moja ya mapini ya mwanzo ya Mondi. Baada ya balaa lile la kwanza kama Nenda Kamwambie, Mbagala na Nitarejea. Nataka kulewa, Moyo wangu na hili la Mawazo. Linatosha kumvisha nishani msela huyu.

Kuna unyama mwingi sana kwenye pini hili la Mondi. Hizi ndiyo ngoma ambazo wakati anatoka ziliwawehusha warembo mitaani. Hata wengine tusielewe dogo anapendewa nini? Kumbe anawagusa na wanamuelewa. 

Kuna hasira aliifuga muda mrefu sana Mondi. Alivaa moyoni, kichwani kwenye bandama hadi utosini. Hasira ambayo ilimfanya atimbe kwa Papa Misifa. Kisha kwa unyenyekevu mkubwa akamuomba ampige tafu. Mwana akakubali.

Hasira za Mondi alizofuga muda mrefu Mitaa ya Tandale pale Tanesco. Zilifanya asione haya kumvaa ‘Supa staa’ Davido, ampe shavu kwenye pili la Number One Remix. Yes! Hasira za maisha na ukwasi ukizitendea haki lazima zikupe pesa. 

Hasira za kukupa mzuka wa kazi. Hizo ndo zitakupa pesa, heshima, nidhamu na akili ya maisha. Ndiyo hasira zenye faida na maana. Sina hakika kama bado hasira hizo zina kambi rasmi kwenye ubongo na moyo wa Mondi. 
 
Cha msingi ni kufahamu kuwa Mondi ni msela ambaye pesa inamvisha ubishoo. Ama ni bishoo ambaye alizaliwa, kukulia na kuishi kinjaa njaa. Zile njaa njaa zake za udogoni pengine ziliificha tabia halisi ya kiumbe hiki. Huyu ni msela, bishoo, tajiri na staa.

Hasira za maisha. Ndo msingi mkuu wa Diamond. Ndio! Kuandika mashairi yenye kugusa nyoyo za waswahili. Kazipekue droo zako zenye nyimbo za miaka na nne nyuma. Kamsikiliza Diamond. Ngoma baada ya ngoma. Utanielewa vyede.

Utagundua Diamond alikuwa anaandika nyimbo za mapenzi zenye tofauti kubwa na wenzake. Wengiwao huimba mapenzi ya kufikirika. Mondi anaimba mapenzi ya kukugusa wewe na yule na wale pale.

Nenda Kamwambie, Mbagala, Nitarejea, Nataka Kulewa, Moyo wangu, Mawazo. Hizi ni silaha nzito. Kasikilize. Hata leo hii kuna daraja kubwa kati ya Diamond na wengine. Pale akiamua kuandika kwa ajili ya Wabongo tu. 

Achana na zile za melodi na midundo mizuri kwa ajili ya kimataifa. Mondi wa ‘Utanipenda’ ni tofauti na Mondi wa Jeje. Mondi wa Tetema siyo wa Kwangwaru. Katika Kwangwaru kafanya unyama kwa ajili ya Wabongo.

Lakini kwenye Tetema kuna unyama mwingi kwa ajili ya kimataifa. Ni mpishi anayejua nani ale nini na nani asile nini. Ndo maana kuna ngoma akizitoa akili za Mwananyamala, Bonyokwa na Kivule hazimuelewi. Nenda Mayote sasa. 

Any way! Nimesahau nilitaka kuongelea nini kuhusu Mondi. Lakini ndiyo hivyo kila kitu kwake Mondi ni stori, na kila kitu kwake ni pesa. Unatakiwa kuwa namna hii supa staa’ yeyote. Huwezi kuwa staa unayechagua lipi lisemwe juu yako. 

Kuna ‘taimu’ binafsi nakubaliana sana na wanyamwezi wangu wa kitaa. Ambao siku zote tukiwa kwenye ‘lokesheni’ na ‘code’ za bata. Wataniambia ngoma za Ngwair zinaashiria kuwa alizaliwa kabla ya wakati. 

Yaani 1982 haukuwa mwaka aliostahili kuzaliwa. Wanasema aliostahili kuzaliwa mwaka aliofariki 2013. Ukiuliza kwa nini, jibu lao ni kwamba aliimba mambo ya mbele ya wakati. Aliufanya muziki wake kuwa miaka 30 mbele yake. 


Mimi ni nani niwakatalie? 

Nawaunga mkono. Pia naongezea yangu kwamba hata Mondi hakupaswa kutoka 2009, alipaswa kutoka 2019. Muziki wake aliufanya kwa mtazamo wa dunia ya leo. Aliyofanya miaka 14 iliyopita yanafanywa leo na Marioo. 

Mondi kafanya kila kitu kwenye ‘keria’ yake. Wakati mwingine ukitia shaka juu ya uwepo wake kando ya Zuchu. Hebu kaa huko kwenu, jiulize pisi alizopita nazo mwamba. 


Kuna sampuli yoyote ambayo umewahi kuwa nayo wewe na kuimiliki? 

Hata binadamu kadiri unavyokua, baadhi ya vitu hutamani tena. Kama peremende, bembea, kuogelea beach, nguo za Eid au Xmass. Hata pisi ukipita nazo nyingi za kutosha huoni jipya tena unakaa popote pale ‘unapoinjoi laifu’. 

Katika umri wa Diamond, umaarufu wake na kipato chake. Alichobakisha pengine ni Ili kulinda ‘brand’ yake, pesa zake na kesho ya saana yetu. Kwa sasa hivi Mondi anastahili kulindwa. Hata wasaidizi wake wanapaswa kuwa na elimu kubwa izingatiwe.