Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Muziki wa dansi una zaidi ya miaka 120 sasa

Muktasari:

  • Bendi hii ilianza mwaka 1964 ikiwa mali ya chama cha wafanyakazi kilichoitwa NUTA, hivyo na bendi nayo ikaitwa NUTA Jazz Band. Muda mfupi baada ya kuanza iliweza kuwa na ubora na kuwa kati ya bendi maarufu nchini na nchi jirani. Chama cha NUTA kilibadilishwa na kuwa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania, maarufu kwa kifupisho chake – JUWATA- na bendi nayo ikabadilishwa jina na kuitwa JUWATA Jazz Band. Umahiri wa wanamuziki wa bendi hii, uliendeleza kazi nzuri iliyoanzishwa na NUTA Jazz Band.

Dar es Salaam. Mwaka huu 2026, bendi moja wapo kongwe na ambayo bado iko jukwaani inatimiza miaka sitini na mbili wa kuwa jukwaani mfululizo bila kuwahi kuvunjika, nayo ni bendi ambayo sasa inaitwa Msondo Ngoma Music Band.


Bendi hii ilianza mwaka 1964 ikiwa mali ya chama cha wafanyakazi kilichoitwa NUTA, hivyo na bendi nayo ikaitwa NUTA Jazz Band. Muda mfupi baada ya kuanza iliweza kuwa na ubora na kuwa kati ya bendi maarufu nchini na nchi jirani. Chama cha NUTA kilibadilishwa na kuwa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania, maarufu kwa kifupisho chake – JUWATA- na bendi nayo ikabadilishwa jina na kuitwa JUWATA Jazz Band. Umahiri wa wanamuziki wa bendi hii, uliendeleza kazi nzuri iliyoanzishwa na NUTA Jazz Band.


 Na bendi ikaendelea na umaarufu chini ya mtindo wao Msondo Ngoma.  Baade bendi ilipitia majina ya TFTU na OTTU Jazz Band kutokana na taasisi iliyokuwa ikimiliki bendi kubadili majina. Kwa sasa bendi ni mali ya wanamuziki wenyewe na inaitwa Msondo Ngoma Music Band. Bendi bado iko katika nafasi ya juu ya bendi bora nchini.


Bendi nyingine kongwe ambayo bado iko hai ikiendelea na maonyesho yake, ni Mlimani Park Orchestra, maarufu kama wana Sikinde Ngoma ya Ukae. Mlimani Park Orchestra ilianzishwa mwaka 1978, kwa hiyo bendi hiyo kwa sasa ina umri wa miaka arobaini na nane.  Bendi hii iliyoanzishwa ikiwa na wanamuziki kutoka Dar es Salaam  Internationa Orchestra, na baadae wanamuziki kadhaa wa JUWATA Jazz Band wakaongezeka, nayo imekuwa katika nafasi za juu za bendi pendwa nchini na nchi jirani toka ilipotoa album yao ya kwanza.


Mlimani Park Orchestra mwanzo kabisa ilikuwa mali ya kampuni ya umma iliyoitwa Tanzania Transport and Taxi Services. Band na ukumbi ambao ulikuwa masikani ya bendi vilikuja kuchukuliwa na Dar es Salaam Development Corporation (DDC), na bendi ikabadilisha jina na kuanza kuitwa DDC Mlimani Park Orchestra. Kwa sasa bendi ni mali ya wanamuziki wenyewe na imerudia jina lake la awali la Mlimani Park Orchestra.


Bendi nyingine kongwe ambayo kwa sasa imekuwa na maonyesho machache kutokana kufiwa baadhi ya wanamuziki wake wakongwe ni Kilimanjaro Band, maarufu Wananjenje. Bendi hii mwaka huu inatimiza miaka 52. Kilimanjaro Band ilianzia Tanga ikiitwa The Lovebugs, baadae ikabadili jina kuitwa The Revolutions. Bendi hii ilipoenda Uingereza, jina hilo likawa haliitambulishi kuwa ni bendi ya Kitanzania ndipo ilipobadili jina na kuanza kuitwa The Kilimanjaro Band.


Pamoja na umri mkubwa bendi hizi, wala hazikuwa waanzilishi wa muziki wa dansi Tanzania. Historia ya muziki wa dansi ilianza enzi za utawala wa Wajerumani mwanzoni mwa karne ya 20, hivyo kwa kweli muziki wa Dansi kwa sasa una umri wa zaidi ya miaka mia moja na kumi.

Muziki huu ulianza kwa mtindo ulioitwa Beni Ngoma. Huu ulikuwa muziki wa vijana wa enzi hizo za Wajerumani , ambao ulipigwa kwa kuiga muziki wa brass band wa wanajeshi wa jeshi la Wajerumani. Muziki huu ulipata umaarufu kiasi cha kuwa ulikuwa ulipendwa kuanzia kusini mwa Somalia hadi kaskazini mwa Msumbiji.


Utawala wa Waingereza ulijaribu sana kuupiga marufuku muziki huu, lakini haukufa na bado masalia yake yapo katika baadhi ya ngoma za kiasili kama Malipenenga ya Wanyakyusa na Mganda wa Wamanda. Na bado ni maarufu sana nchini Malawi.


Muziki wa dansi wa Tanzania ulianza zama zile ambapo umeme haukuweko, na hivyo basi vyombo vilivyokuwa vikitumika havikuwa vinatumia umeme, na unaendelea mpaka sasa ambapo ni mwanzo wa zama za akili unde.


Katika miaka nyuma karibu kila mji ulikuwa na bendi moja au zaidi. Na pia kulikuweko wapiga magitaa makavu wengi, ambao walipewa jina la wapiga magitaa ya Bosko, kutokana na mpiga gitaa maarufu kutoka Kongo aliyeitwa John Mwenda Bosco. Hawa walikuwa maarufu sana katika vilabu vya pombe za asili.


Bendi ambazo hazikuwa za Dar es Salaam lakini zilikuwa maarufu ni nyingi sana, labda nizitaje chache. Mkoa wa Morogoro pengine ndio ulikuwa na bendi nyingi zaidi, zikiwemo,  Cuban Marimba Band, Morogoro Jazz Band, Kilosa Jazz Band, Sukari Jazz Band,  Ulanga Jazz Band, TK Lumpopo Band, Malinyi Jazz Band, Kilombelo Jazz Band, Mzinga Troupe, Les Cuban Band, Mahenge Jazz Band, Kwiro Jazz band.


Kule Tanga kulikuwa na Atomic Jazz Band, Yanga Nyamwezi Jazz Band ambayo baadae ilikuja kuitwa Jamuhuri Jazz Band, Bandari Jazz Band, Watangatanga Band, Amboni Jazz Band, Tanga International Orchestra. Moshi kulikuwa na Zaire Success, Bana Afrika Kituli, PTS Jazz Band, Black Beatles, Mkulima Jazz Band, Moshi Secondary Jazz Band (MOSESCO), Moshi Technical Jazz Band. Kule Arusha kulikuwa na Arusha Jazz band, Kurugenzi Jazz Band, Crimson Rage, The Ambassador, Orchestra National na kwa mtindo huu nchi nzima kulikuwa na bendi na zilikuwa bendi pendwa haswa.