Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwisho wa safari ya MC Pilipili

Muktasari:

  • Umauti humkuta mtu bila kufahamu siku wala saa atayoiaga dunia. Na wahenga wanasema kifo ni fumbo na pengine binadamu angefahamu siku yake ya kufa basi  hakuna ambaye angefanya maendeleo

Dar es Salaam. Kila binadamu aliyetoka kwenye tumbo la mwanamke, siku zake za kuishi zinahesabika yaani nafsi yake lazima itaonja umauti. Hivyo ndivyo ilivyo na inavyoaminika pia katika imani zote.

Umauti humkuta mtu bila kufahamu siku wala saa atayoiaga dunia. Na wahenga wanasema kifo ni fumbo na pengine binadamu angefahamu siku yake ya kufa basi  hakuna ambaye angefanya maendeleo.

Ndugu jamaa na marafiki huangua vilio kwa kumpoteza mpendwa wao kwani hutambua fika kuwa ndiyo mwisho wa kuonana kwamba hawatamwona tena mpendwa wao. Hivyo basi hata kwa wapenzi wa burudani hawatamwona tena mchekeshaji na mshereheshaji Emmanuel Mathias  ‘MC Pilipili’ ambaye alipoteza maisha Jumapili Novemba 16, 2025 akiwa jijini Dodoma.

Kama ambavyo ucheshi wake ulikuwa ukigonga nyoyo za mashabiki wake. Ndivyo mshangao na huzuni ilivyogonga vichwa vya waliompenda huku wakijiuliza nini kimemkuta mchekeshaji huyo?  Wakati wengi wakitahamaki swali hilo lilijibiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lilipotaja chanzo cha kifo chake kuwa kilitokana na kipigo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyela alisema wameshirikiana na madaktari katika kuufanyia uchunguzi mwili wa MC Pilipili na kubaini kuwa kifo chake hakikuwa cha kawaida 

“Ni kweli, tumeshirikiana na wataalamu ambao ni madaktari. Mwili ule tumebaini ulikuwa na alama zinazoonyesha kulikuwa na shida ambayo ni kipigo. Maana alama zile hazikuwa za kawaida, hivyo tumeanzisha uchunguzi mara moja kujua nini kilitokea na tungeomba yeyote mwenye taarifa za siri juu ya jambo hilo atupatie,” alisema Hyela.

Kauli ya Kamanda Hyela ilizalisha swali jingine la je, nani kahusika kuondoa uhai wa Pilipili? Hayo tuwaachie Jeshi la Polisi ambalo lipo kwenye uchunguzi. Fahamu zaidi kuhusu MC Pilipili.

Pilipili alizaliwa Mtaa wa Airport, Dodoma mjini Oktoba Mosi, 1985 akiwa mtoto wa pili wa Mathias Matebe na Mariam Matebe. Alianza elimu ya  msingi katika Shule ya Uwanja wa Ndege ambapo alisoma hadi darasa la nne na kuhamia Ipagala ambako alimalizia 2000.

Akiwa shule ya msingi alijihusisha na masuala ya uchoraji, uimbaji na hata kucheza muziki ingawa alikuwa na ndoto za kuwa mwandishi wa habari. Baaada ya kumaliza darasa la saba alijiunga na Sekondari ya Dodoma 2001 ambapo ndoto za uandishi wa habari zilianza kufunikwa taratibu.

Akiwa sekondari kama ilivyo kawaida huwa kuna masomo ya kuchagua kutokana na tabia yake, mwalimu Kilela ambaye sasa ni marehemu alimshauri achukue somo la Sanaa za Jukwaani ambalo alilipenda na kufaulu kuliko mengine.

Tangu hapo alipenda sanaa hali iliyokifanya kipaji chake cha uchekeshaji kukua na baadaye kuwa ushereheshaji (MC) katika matukio mbalimbali wakati akiwa shuleni. Aliendelea na kazi ya ushereheshaji hata alipoanza masomo ya kidato cha tano na sita katika Sekondari ya Jubilee mkoani Dodoma.

Pilipili alifanya kazi ya uchekeshaji na ushereheshaji katika nchi mbalimbali kama Kenya, Rwanda, Uganda na Afrika Kusini hali iliyomsaidia kujitangaza ndani na nje ya nchi kwani mashirika na kampuni mbalimbali zilikuwa zikimwita sana kuongoza sherehe na matukio.

Hata hivyo nyota yake kwenye sanaa iliwaka kisawasawa, licha ya miaka ya hivi karibuni kuyumba kidogo huku yeye mwenyewe akidai kifo cha mama yake kilichotokea mwaka 2020 ndicho kilimsababishia msongo wa mawazo hadi kushindwa kufanya kazi kama zamani.

Lakini mwaka 2025 ulikuwa mzuri kwake kwani alianza kurudi tena kwenye chati

Licha ya shughuli hizo za sanaa pia MC Pilipili alikuwa mchungaji ambapo kanisa lake lilifahamika kama Love Church. Katika moja ya mahojiano aliyowahi kufanya  na Mwananchi mwaka 2024 alisema wokovu aliuanza tangu akiwa darasa la nne, Dodoma.

“Nilibatizwa kwa maji mengi na nikaendelea kusali nilipofika kidato cha kwanza nilianza kuwa mwalimu wa watoto kanisani kwa miaka mitano. Baadaye nikawa mchungaji wa vijana na kisha nikawa msaidizi wa mchungaji, kilichokuwa kinazuia nisiwe mchungaji kamili sikuwa nimeoa kipindi hicho.

“Nilivyokuwa kidato cha kwanza nilikuwa kiongozi wa Ukwata humo ndipo nimehubiri sana nilifikia hatua ya kujaza watu kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma nikamleta Rose Muhando, Fanuel  Sedekia na Upendo Kilahiro,” alisema katika mahojiano hayo.

Aliongeza kuwa alivunja rekodi ya somo la dini kwa Dodoma akapata nafasi ya kwenda kusimamia shule za kanisa kama mwalimu wa masomo ya dini.

“Mimi unavyosikia mwalimu siyo wa hesabu au Civics ni wa masomo ya biblia kwa madarasa ya mitihani kuanzia form two, four na six hata ukimsikia Mon Centrozone anasema mimi mwalimu wake ni kwenye masomo ya dini, hayo Civics nilianza kufundisha baadaye,” alisema.

Aidha, Pilipili alikuwa na Stashahada ya Uchungaji kabla ya umauti alikuwa  anaendelea na masomo, akiitafuta shahada ya uchungaji kwenye Chuo cha Biblia kilichopo Kawe kiitwacho Shalom Bible College.

Utakumbuka enzi za uhai wake Pilipili alifunga ndoa na mwanadada Philomena Thadey (Qute Mena). Ndoa hiyo ilifungwa Juni 29, 2019, na kuwashangaza wengi kutokana na namna ambavyo Pilipili alikula kiapo chake mbele ya mchungaji kuwa tofauti na wengi walivyo tegemea.

Kama ilivyo kawaida ya taratibu za kufungishwa ndoa kanisani. Pilipili aliulizwa kama anampokea Philomena Thadey kuwa mkewe kwenye shida, raha na magonjwa lakini cha kushangaza kwa Pilipili ilikuwa tofauti. Alikubaliana na baadhi ya vipengele alivyoulizwa isipokuwa njaa, shida na magonjwa.

Ndani ya ndoa yao walibarikiwa mtoto wa kike aitwaye Elphina. Aidha katika baadhi ya mahojiano MC Pilipili aliwahi kueleza kuwa na watoto watatu wote wa kike akiwataja kwa majina ya  Mariam, Brianna na Elphina ambao alidai kuwapenda na kuwajali sana.

Tunaweza kuita mwisho wa enzi za Pilipili ambaye mwili wake ulizikwa Novemba 20,2025. Jina lake litakumbukwa daima kwenye ulimwengu wa ushereheshaji na uchekeshaji nchini. Apumzike kwa amani.