Nani atavaa suti ya James Bond? Mbio za kumrithi Daniel Craig zashika kasi
Muktasari:
- Takribani miaka 15 sasa mwigizaji Daniel Craig wa Uingereza alijulikana zaidi kwa kuicheza nafasi ya James Bond katika filamu za kisasa za mfululizo huo, sasa kijiti kimefikia tamati, na mchakato wa kumsaka Bond mwingine ukianza. Ambapo kwa wengi, Daniel Craig anahesabiwa kuwa mmoja wa waigizaji waliofanikiwa zaidi kuicheza nafasi ya James Bond katika historia ya filamu.
Mchakato wa kumtafuta mwigizaji atakayechukua nafasi ya James Bond umeanza rasmi chini ya kampuni ya Amazon MGM Studios, huku mastaa mbalimbali wakitajwa kuwania nafasi hiyo maarufu duniani.
Takribani miaka 15 sasa mwigizaji Daniel Craig wa Uingereza alijulikana zaidi kwa kuicheza nafasi ya James Bond katika filamu za kisasa za mfululizo huo, sasa kijiti kimefikia tamati, na mchakato wa kumsaka Bond mwingine ukianza. Ambapo kwa wengi, Daniel Craig anahesabiwa kuwa mmoja wa waigizaji waliofanikiwa zaidi kuicheza nafasi ya James Bond katika historia ya filamu.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa kutoka MGM, usaili huo unaendelea kwa usiri mkubwa, kama ilivyo desturi ya filamu za James Bond, ambapo majina ya washiriki huwa hayatangazwi hadharani hadi hatua za mwisho za mchakato.
Nafasi ya James Bond imeendelea kutajwa kuwa moja ya uhusika wenye hadhi kubwa zaidi katika tasnia ya filamu ya Hollywood. Mbali na malipo makubwa, mhusika anayepata nafasi hiyo hujizolea heshima, ushawishi na fursa nyingi za kimataifa.
Kwa kawaida, mwigizaji anayechaguliwa huingia mikataba ya filamu kadhaa za Bond, jambo linalomwingizia mapato makubwa, marupurupu na umaarufu wa kimataifa. Kutokana na faida hizo, nafasi hiyo imekuwa ikijulikana kama “golden ticket” ya Hollywood.
Taarifa zinaeleza kuwa waigizaji mbalimbali kutoka Uingereza na Marekani, wakiwamo nyota waliothibitisha uwezo wao na vipaji vinavyochipukia, tayari wameanza kufanya majaribio ya siri kwa lengo la kupata nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa tetesi zinazosambaa katika mitandao ya kijamii, baadhi ya majina yanayotajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na James Norton, Tom Hardy, Regé-Jean Page, Idris Elba, Aaron Taylor-Johnson, Henry Cavill na Aaron Pierre.
Mchakato huo unadaiwa kuwa mkali kutokana na studio kulenga kupata mtu mwenye sifa zote zinazohitajika kuubeba mhusika huyo maarufu. Katika hatua za majaribio, waandaaji hawatazami uwezo wa kuigiza pekee, bali pia kile kinachoitwa “Bond presence” mvuto, kujiamini na uwezo wa kuonekana kama James Bond mbele ya kamera.
Kwa miongo kadhaa, James Bond amebebwa na waigizaji wakubwa katika historia ya filamu, akiwamo Sean Connery, Roger Moore, Pierce Brosnan na Daniel Craig, ambaye alihitimisha safari yake kupitia No Time to Die.
Kila mmoja ameacha alama yake katika historia ya Bond kwa kuupa mhusika huyo sura tofauti kulingana na wakati wake. Kwa upande wa Daniel Craig, aliwasilisha Bond wa kisasa zaidi, mwenye nguvu na simulizi zenye uzito mkubwa, tofauti na taswira ya awali ya jasusi mwenye ucheshi mwingi na tabasamu la mara kwa mara.