Ndani ya Boksi: Wanyamwezi japo tumezaliwa Tizii

Bongo Fleva chanzo chake ni muziki wa kufokafoka toka Unyamwezini (hip-hop). Taratibu baada ya ‘mabroo’ wa kitambo kuchana sana mistari. Baadaye miaka ya 2000 jamii kwa mapana yake ikaupokea rasmi muziki huu.

Mwanzo waliaminia zaidi wanamuziki wa kuchana (ku-rap) kwa sababu ndiyo wenye muziki. Lakini kwa kutojua ama kwa kujua, baadhi ya ‘vilaza’ wakaanza kuifuta ‘identiti’ ya neno Bongo Fleva katika muziki wa rap Bongo.

Wakaamua tu kwa akili ya kibangebange, kuwa kufokafoka ndiyo hip-hop kuimba ni Bongo Fleva. Wakatuaminisha kuwa msanii wa kuchana ukijitoa Bongo Fleva ni matusi. Wakajitenga na Bongo Fleva nayo ikajitenga.

Ajabu ni kwamba waanzilishi wa neno Bongo Fleva, hawakutunga kwa ajili ya muziki wa kuimba. Walilitunga kwa ajili ya muziki wa kufokafoka, kwamba ni hip-hop katika ladha ya Bongo. Zile ndafu za kuijua sana hip-hop hazikuelewa.

Neno Bongo Fleva lilipoanza kutamba miaka ya 90 mwishoni. Hakuwepo Dully wala TID, hakuwepo Ruta Bushoke wala Q Chilla. ‘Hau kamzi mnawasusia ‘identiti’ yenu wakuja? Kifupi ni kwamba Bongo Fleva ilipoteza maana yake.

Mwanzo vijana walianza kuiga muziki wa hip-hop toka Marekani. Kuanzia jinsi ya kuimba, uvaaji, majina hadi utembeaji. Licha ya joto kali la Dar, lakini haikuwa ajabu kukuta kijana kutupia koti zito na mzula kichwani kama ‘Faza Krimasi’.

Ukiuliza. Utasikia ‘Noti Bai Necha’ sijui Snoop Dogg. Ndiyo maana hata majina ya wasanii wa zamani hayakuakisi Ubongo. ‘Imajini’ Nigga J, Ganstars With Matatizo (GWM) Hard Blasters, 2 Proud, Niggaz 2 Public nk. Unyamwezi mtupu yaani!

Hata kizazi cha pili kiliendelea na hulka za Umagharibi tupu. Kina Jaymoe, FA, Ngwair na wengineo. Ngoma zao za mwanzoni kama hawakubeba ‘wazo’ la Unyamwezini basi wamepita nayo hata swaga tu.

Yes! Unyamwezi uliendelea kutawala akili za vijana wetu. Katikati ya miaka ya 2000 ndipo Unyamwezi ulianza kutoka kwenye bongo zetu na kuanza kupita na njia zetu. Lakini pamoja na hilo kamwe hatukuacha kuiga.

Kuiga kuliendelea na safari hii tukahamia kwa Wanaijeria. Tukaanza kuona ujanja ni ‘Unaija’. Wakati miaka kadhaa nyuma Bongo Fleva iliteka Afrika, ghafla wasanii wetu wakawa wafuasi wa ‘Wanaija’. Tukajidogosha mbele ya kina Davido.

Tukawa ‘Wanaija’ japo tumezaliwa Tmk. Utaratibu huu ukaendelea kwa kasi ya ajabu kama maoni ya wadau kule bungeni na sheria za uchaguzi. Yes! Madogo wakaja na Amapiano. Huko ndiyo tumetuama kabisa.

Hii ndiyo imekuwa kubwa kuliko, yaani amapiano ya Kibongo-bongo linapigwa na kuchezwa kifundi kuliko lile la Wazulu. Tumeiga kupitiliza mpaka wao ndiyo wanatuiga sisi kwa sasa. Kifupi tunasubiri kuiga kitu kipya.

Mwaka jana tumeshuhudia ngoma za Whozu na Madee zikila kitanzi. Makosa yao yaliyofanya wale kitanzi kwa yale mataifa tunakoiga kila kitu chao wala sio makosa. Lakini, hapa kwetu ni kosa la kimaadili.

Sio bahati mbaya sana ila wamenogewa kuiga. Wanaiga kila kitu na kupata mafanikio. Waliiga nyimbo, waliiga majina, wakaiga swaga mpaka uvaaji. Sasa wanaiga hadi dhambi za magharibi. Wanaona ni sawa tu.

Wimbo wa Madee hata jina la wimbo naogopa kuandika. Lakini yeye alikaa na wana akawapa mistari wakamsifia sana. Akaenda studio ‘produza’ akamwambia mzuka tena hili ni ‘hiti songi’. Wakarekodi na kumpa mtu wa video naye akapitisha.

Koooote ngoma ilionekana ya maana. Ni Basata tu na sisi wengine ndiyo tunaona wimbo haufai. Inawezekana tumepitwa na wakati. Au Madee na watu wake wa karibu wanaendeshwa na mimoshi flani amazing.

Kitambo sana, Khamis Mwinjuma a.k.a Mwana FA, Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo. Kwenye goma lake na Noorah la Unanitega, ana mstari wake huwa naupenda kinyama. Nikilipuka sana lazima niutaje.

Nikienda sehemu nikikuta mazingira flan  matamu. Pisi na mabishoo kibao lazima niutaje. Mwana FA anakuambia: Wanyamwezi japo tumezaliwa Tizii. Yaani Umarekani mwingi hata kama ni mkazi wa Katoro au huko Kigoma ndani ndani, ila na wewe upo.