Ndani ya Boksi: Zuchu kwenye anga za Tx Moshi
Muktasari:
- Hii ni mistari ya wimbo wa Mume wangu Jerry. Uliimbwa na Hassan Rehan Bitchuka. Sikinde Ngoma ya Ukae ya moto. Tunaongelea DDC Mlimani Park ikiwa imejaza mastaa wa kweli.
Dar es Salaam. “...Mume wangu Jerry kusema kweli, nimechoka na visa vyakooooooo. Sitovumilia kamwe kutokana na mwenendo wakooo. Nitashindwa.
...Kila nisemalo kwako ni baya
Kila nitakachofanya kwako ni kibaya...
...Juzi, juzi umenipiga kukuomba utulie nyumbani...
...Sijui tuishi vipi? Raha ya mume ni kusikilizana... Nipe chochote kile... kama hatukuelewana ni kazi bureee...”
Hii ni mistari ya wimbo wa Mume wangu Jerry. Uliimbwa na Hassan Rehan Bitchuka. Sikinde Ngoma ya Ukae ya moto. Tunaongelea DDC Mlimani Park ikiwa imejaza mastaa wa kweli.
Nginde likiwa ‘fulu’ muziki kweli. Mtiti kutoka DDC Kariakoo, DDC Magomeni Kondoa hadi DDC Mlimani Park. Pale geti la kutokea na kuingilia Mlimani City upande wa Survey.
Ukisoma ujumbe wa wimbo huu kwa kizazi hiki. Ngumu kuamini kama uliimbwa na mwanaume. Sauti ya kiume, ukapendwa na kina mama na kina baba. Ikawa ‘hiti songi’.
Kwanini? Kina Zuchu walikuwa wachache. Wale waliokuwapo walijikita na muziki wenye testi za kike kama taarabu. Masela kina Cosmas Chidumule walikosa pisi kali kwenye jukwaa lao.
Walikuwapo wachache kama vile Tabia Mwanjelwa na Kida Waziri wa Vijana Jazz na ngoma ya Wifi Zangu. Wengi walikuwa katika vikundi vya taarabu. Hali hii ilifanya bendi za dansi zikose sauti ya kike.
Kida Waziri anakuambia;
“Kwanza mngeniuliza, kipi ananipendea? Na mapenzi hayana dawa. Kida nifanye nini? Oooh nifanye nini? Naelewa mazoea, yana tabu... lakini nitajitahidi ili kusahau...”
Lakini pini nyingi washua wetu hawakuona hatari ‘kukava’ zile mishe za kike. Mfano ngoma ya Asha Mwanasefu ya Msondo Ngoma. Alipotakiwa kuimba Asha Mwanasefu kuna sauti ya Tx Moshi Wiliam.
Halafu ngoma zilibamba kinoma. Watoto wa kike walichelewa sana kuamka. Wakongo kama Mbilia Bell na Yondo Sister. Kwa Bongo kuona dem jukwaani ilikuwa ni adimu kinyama.
Siyo muziki tu. Zamani karibu kila sekta mademu walikuwa adimu. Dunia ilikuwa ya kimfumo dume kinoma. Kila mchongo ulifanywa na masela. ‘Nao dezi’ michongo mingi imeshikwa na madem.
Hivi sasa madem hujaa kwenye mabaa kuliko masela. Wanajaa viwanja vya mpira, wanajaa kwenye biashara. Hata mawinga wa kitaa cha Kariakoo wengi madem. Kitu pekee kilichojaza masela ni jela.
Hivi sasa kimuziki madem wapo wengi kinyama. Hakuna noma tena kama zamani. Wazazi wale waliokatazwa kufanya muziki na baba zao. Wao ndo wanahimiza watoto wao wafanye muziki.
Hii ni kufuatia mabadiliko chanya ya Bongo Fleva. Wasanii wa kike kama Lady Jaydee, mafanikio yao yamechangia madem kukomaa na gemu. Namba za wasanii wa kike na kiume zinalingana hata kiuchumi.
Kuna Zuchu na Nandy. Kwa sasa hawa ndo topu topu topu klasi wa sasa. Wana ngoma kali, mikoko mikali na mali. Majina makubwa ndani na nje ya mipaka ya Bongo.
Na mashabiki wengi kinoma.
Ila kuna kitu kimoja kwa Zuchu. Anatenga sana masela. Ngoma zake nyingi sio rafiki kwa midomo ya kiume. Yaani ngoma zake kwa ujumla ni ngumu kumkuta msela akiimba. Labda aimbie chumbani.
Mfano;
“Baba chanja baba chanja eeeh¡! Chukua vyote chukua... kulaa! itafune nganjanganja... eeeh! Chakua mwaya chakau... kulaa! Ujibusti na karanga... eeeeh! Tuliza na kitumbua... kulaa!”
‘Imejini’ msela anaanzaje kuimba mistari ya hivi?
Kuna namna Zuchu anabeba kijiji chake kwa mistari hii. Wanawake wanahusudu kwa sababu hunata na nafsi zao. Anaimba kwa niaba ya pisi kali, anakuwa sehemu yao kupitia mistari yake. Wanaume hawahusiki.
Nenda kafuatilie mistari ya Zuchu kuanzia leo. Haina urafiki kabisa na masela lakini anapendwa na masela. Kwa sababu jumbe zake zinawakataa masela, lakini lugha anayotumia ya kisela.
“Filimbi nitapuliza kuita ndege waje... (Mh!!). Kuitwa ndege waje (Mh!)... Raha zimefululiza kwako natokaje? Hadi Bububu umepitiliza tuko kwa Bibi Paje (Mh!!)... Taratibu unaniliza Baba...”
Hii ni moja ya ‘vesi’ ambayo sela yeyote hatakiwi kuiimba hata kwa bahati mbaya. Hizi maneno zinanikumbusha Khadija Kopa na pini lake la Tx Mpenzi. Ni wazi vya kurithi hupitiliza mpaka kwa Bibi Paje.
Uandishi wa Zuchu unanipa jibu kwamba haandikiwi. Ili uandike kama Zuchu lazima uwe jinsia kama ya kwake. Kuna namna masela wanadata naye kwani anawagusa.
Yaani anaimba vitu vya kike ambavyo masela hawavisikii kwenye vinywa vya madem zao. Zuchu ana eneo lake la peke yake na analijulia sana. Nendo You Tube kasikilize Tz Mpenzi wa Bi Khadija Kopa.