Nenda C-Pwaa, utakumbukwa kwa mengi

Muktasari:

Msanii wa Bongo fleva, Ilunga Khalifa maarufu C-Pwaa hatunaye tena  amefariki dunia na atazikwa leo jioni Jumapili Januari 17,  2021.

Dar es Salaam. Msanii wa Bongo fleva, Ilunga Khalifa maarufu C-Pwaa hatunaye tena  amefariki dunia na atazikwa leo jioni Jumapili Januari 17,  2021.

Mara ya kwanza kumsikia na kuanza kumfuatilia ilikuwa mwanzoni mwa  miaka ya 2000 akiwa katika kundi la Park Lane lililoundwa na yeye pamoja na  Ismail Sadick maarufu Suma Lee ambaye alitamba na nyimbo za  Hakunaga na Chungwa.

Nyimbo ya Nafasi Nyingine na Aisha za kundi hili zilinikonga sana na kujikuta naziimba kila ninapokuwa peke yangu.

C-Pwaa  amekulia Tanga, lakini mama yake ni Msukuma na baba yake ni Mrangi.

Wazazi wake walitengana akiwa darasa la pili mwaka 1990, aliishi na baba yake Mbeya kabla ya kwenda kuishi na mama yake Tanga.

Kipaji chake ni kuchora, unaweza kusema baba yake kuwa DJ kulimfanya ashawishike kuanza kufanya muziki.

Ndoto yake ya kuimba ilianza huko Mbeya akiwa kidato cha pili na alikiwa vizuri katika somo la Kiingereza na alipata daraja la kwanza kidato cha nne.

C-Pwaa alikutana na Suma Lee mkoani Tanga wakati akienda kumsalimia mama yake mwaka 2000.

Alimkuta Suma Lee akiwa na kundi la Park Line crew na baadaye wakajiunga na kuanza safari yao ya muziki.

Walitamba sana Tanga na baadaye wakaenda Dar es Salaam na kutoa wimbo wa Aisha na Nafasi Nyingine kisha kutoa album.

Kundi hili halikudumu sana lilivunjika kila mmoja kuanza kufanya muziki mwenyewe.

Ndio ukawa mwanzo wa kutamba kwani alitoa wimbo wa Pwaa na baadaye Problem.

Alianza kutambulika kimataifa baada ya kufanya wimbo wa Action akimshirikisha Dully, Ngwea na mwanamuziki  kutoka Jamaica, Ms Trinity.

Bila shaka wengi walihisi aliyeimba wimbo huo si Mtanzania kabisa na kwa bahati nzuri teknolojia ilikuwa imeanza kukua hivyo haikua tabu kuupata katika mitandao mbalimbali ikiwemo YouTube.

C-Pwaa alikuwa miongoni mwa wasanii wa kwanza kufanya video ya gharama kubwa, baada ya kusafiri yeye na timu yake kwenda Afrika Kusini kufanya video ya wimbo wa Mmmh.

Wimbo wa mwisho kuusikiliza ni ule wa Fire aliowashirikisha marehemu Ngwea na Chege ambao ulitoka mwaka 2020.