Ni Wema Day, atikisa mitandaoni
Muktasari:
- Tangu alipoweka video iliyoonesha kuwa na ujauzito na hatimaye picha ya mguu wa mtoto wa kiume, mitandao ya kijamii siku ya leo imetawaliwa na habari za Wema Sepetu.
Dar es Salaam. Wakati wa Mungu ni wakati sahihi, haya ndiyo maneno yaliyotawala leo kwenye kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii kufuatia taarifa za mrembo Wema Sepetu kupata mtoto.
Kwa muda mrefu kumekuwa na uvumi kuhusu mrembo huyo kuwa na ujauzito, lakini taarifa hizo hazikuthibitishwa hadi asubuhi ya leo alipoweka video kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Video hiyo ilimuonesha Wema (35) akiwa na rafiki zake wa karibu kwenye sherehe waliyoimuandalia katika safari yake ya kuwa mama.
Kwenye video hiyo, kwa mara ya kwanza Wema ameonekana akiwa mjamzito na hapo ndipo wengi walianza kuthibitisha uvumi uliokuwepo kwa muda mrefu.
Salamu za pongezi zilianza kumiminika kwenye chapisho hilo ambalo lilikaa kwa dakika chache kabla ya kuweka chapisho lingine lililoibua shangwe kwa wapenzi na mashabiki wa mrembo huyo aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2006.
Katika chapisho hilo Wema aliweka picha iliyoonesha mguu wa mtoto mchanga aliyevalishwa soksi za bluu, rangi hiyo ikiashiria kuwa mtoto ni wa kiume.
Tukio hili limegusa hisia za wengi kufuatia mrembo huyo kwa muda mrefu kutafuta mtoto, ambapo mara kadhaa kwenye mahojiano aliweka wazi kuhusu hitaji lake hilo.
“Hakuna kitu kinauma kama kukaa sehemu na watu wanaongelea watoto halafu wewe hauna mtoto. Naishia kuwasikiliza, siwezi kuwaambia wasiongee. Kuna muda nahisi mimi sitopata kwa sababu kama kuhangaika nahangaika sana. Nimechoka sana, nafikiri kitu kitakachonipa furaha labda kama nitafanikiwa kupata mtoto,” alisema Wema katika moja ya mahojiano aliyowahi kufanya.
Baada ya kupita muda mrefu bila kutimia kwa haja ya moyo wake, ilifika wakati Wema alitamka mwenyewe kuwa ameshakata tamaa na amekubaliana na ukweli kwamba hawezi kupata mtoto.
“Kwa wakati huu sitegemei kama nitashika mimba tena, imefika wakati nimekata tamaa, siwezi kupata mtoto na nimeshaambiwa hilo, hivyo nimekubaliana na hali hiyo. Huenda Mungu ameamua nisipate mtoto na siwezi kuhoji hilo, nitawapenda watoto wa ndugu zangu na rafiki zangu, maisha yanaendelea.”
Leo mambo yamebadilika, hatimaye Wema amepata mtoto na watu mbalimbali wamejitokeza kuweka maoni na salamu za pongezi, huku maneno ya baraka yakitawala kwenye maandiko ya wengi.
Ray C ameandika, “Pale dunia ilipoona mwisho, Mungu aliona mwanzo.”
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Dk Dorothy Gwajima ameandika, “Pongezi nyingi kwenu kwa baraka za mtoto, Mungu amlinde daima. Awalinde nanyi wazazi wake ili mumpe matunzo na malezi mema kwa utukufu wa Mungu wa mbinguni.”
Jokate Mwegelo ameandika, “Nimefurahi kuona hii. Mungu hajawahi kushindwa na anakuja pale ambapo kila mtu alishakukatia tamaa kwa sababu anataka ujue ni yeye ndiye anayeweza na anayesababisha.”
Naye Rhoda John ameandika, “Wakati wa Mungu ukifika haukuwa wa kuzuia. Mungu tunakutukuza sana kwa ajili ya hili, ukuu wako umeendelea kudhihirika katika nyakati ngumu ambazo Wema amepitia.”
“Maana halisi ya wakati wa Mungu. Happy for you Wema,” ameandika GaraB.
“Acheni Mungu aitwe Mungu, baraka zake ni za milele,” ameandika Faraja Nyalandu.
“Wanadamu tunapoona mwisho, Mungu ndiyo huwa anaanzia hapo, hongera sana Wema.”