Pongezi kwa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva lakini kuna haya!
Muktasari:
- Jambo jingine la kupongezwa ni mwonekano wa wasanii waliotumbuiza. Walivaa kwa heshima na ustaarabu, wakitoa mfano mzuri kwa kizazi cha sasa cha wasanii.
Dar es Salaam. Ninawapongeza waandaaji wa Tamasha la Miaka 30 ya Muziki wa Bongo Fleva lililofanyika Mlimani City tarehe 10 Julai 2026. Ukumbi ulijaa watu takribani 3,500, jambo linaloonyesha tamasha lilikuwa na mvuto mkubwa.
Jambo jingine la kupongezwa ni mwonekano wa wasanii waliotumbuiza. Walivaa kwa heshima na ustaarabu, wakitoa mfano mzuri kwa kizazi cha sasa cha wasanii.
Hata hivyo, yapo mambo yanayoweza kuboreshwa. Kwanza, waandaaji walipaswa kufanya utafiti mpana zaidi ili kuhakikisha wasanii wote waliokidhi vigezo wanashiriki. Wasanii kama Mb Dogg, Lady JayDee, TID, Wagosi wa Kaya na Sugu walistahili kuwamo kutokana na mchango wao mkubwa katika Bongofleva.
Pili, badala ya kuwakusanya wasanii wote katika tamasha moja, wangeweza kuwagawa katika matamasha tofauti au kufanya tamasha katika ukumbi wenye uwezo wa kupokea watazamaji wengi zaidi. Hii ingeongeza nafasi kwa mashabiki wengi kushuhudia maonesho hayo.
Changamoto nyingine ilikuwa muda mfupi wa kutumbuiza. Wasanii wenye nyimbo nyingi zilizopendwa walipewa dakika chache, jambo lililowakosesha mashabiki burudani ya kutosha.
Aidha, mpangilio wa wasanii kupanda jukwaani ulipaswa kuzingatia uzito wa majina yao. Kwa kawaida, msanii mwenye mvuto mkubwa ndiye hufunga tamasha. Wasanii kama Dully Sykes, Juma Nature, Afande Selle au hata Juakali wangefaa kupewa nafasi hiyo.
Kwa mtazamo wangu, kumpanga Dudu Baya kuwa msanii wa kufunga tamasha halikuwa uamuzi mzuri. Mbali na mijadala iliyomzunguka hivi karibuni, bado alikuwa anatoka kuugua na hakuwa amerudi katika kiwango chake bora.
Pia, ingawa wengi wa wasanii hawa ni wakongwe na kuimba kwa kutumia bendi kunaweza kuwa changamoto, maandalizi yangefanyika ili angalau baadhi ya nyimbo ziimbwe moja kwa moja. Nawapongeza waliojaribu kufanya hivyo, akiwemo Q-Chillah.
Kuhusu malipo, ingawa sijazungumza na msanii yeyote, uzoefu unaonyesha kuwa kutokana na idadi kubwa ya washiriki, huenda malipo hayakuwa makubwa.
Mara nyingi wasanii wamekuwa wakilalamikia malipo madogo katika matamasha, hivyo si ajabu ikiwa suala hilo litajitokeza tena. Ijapokuwa sijamuuliza msanii yeyote kapata shilingi ngapi katika hilo tamasha; ninaweza kutumia uzoefu wangu wa kufuatilia na kutafiti sanaa hii ya muziki wa Bongofleva na kusema neno linalotoa picha ya jumla.
Kutokana na wingi wa wasanii, upo uwezekano kwamba kiasi cha pesa walichopewa wasanii hao zaidi ya 30, si kikubwa hasa ukizingatia kwamba watu wanaoandaa tamasha wanahitaji pia wapate faida. Ushauri katika hili, upo sehemu inatofuata (sehemu ya 3.0).
Suluhisho la muda mrefu ni kwa wasanii hawa wakongwe kuunda umoja rasmi wenye uongozi na kuusajili.
Badala ya tamasha moja kubwa, wanaweza kuandaa matamasha katika mikoa mbalimbali na kugawana kushiriki kulingana na umaarufu wao katika maeneo husika. Pia wanaweza kuwashirikisha wasanii wa kizazi cha sasa ili kuongeza mvuto wa matamasha hayo.
Ninashauri wasanii hawa Wakongwe (wenyewe wakijiita Wachonga) waunde umoja wao wenye uongozi thabiti na wausajili. Kisha wafanye mambo yafuatayo wenyewe:
Wasimamie uandaaji wa matamasha ya muziki wenyewe. Waandae mapendekezo (proposals) ya kuomba ufadhili wa matamasha kutoka makampuni mbalimbali.
Wasiandae tamasha moja kisha wakashiriki wote kama hili la 10 Julai 2026; waandae matamasha maeneo (mikoa au wilaya) mbalimbali. Wasanii wagawane kushiriki matamasha hayo;
Matamasha hayo yasifungwe kutumbuizwa na Wakongwe peke yao; bali wawaombe wasanii wa sasa (wadogo zao) wawaunge mkono bila malipo yoyote au bila malipo makubwa.
Matamasha hayo yakifanywa kwa utaratibu na kuwa endelevu, yanaweza kuenea nchini kote na hata katika nchi jirani kama Kenya na Uganda ambako pia wana mashabiki wengi.
Vilevile, wanaweza kuanzisha chombo chao cha habari, wakianza na YouTube na baadaye redio au televisheni. Kwa kuwa tayari wana watu wenye uzoefu wa utangazaji kama Soggy Doggy na TID, hatua hiyo itarahisisha kutangaza kazi zao na shughuli za umoja.
Mwisho, ni muhimu kuanzisha mfuko wa akiba ya uzeeni. Sehemu ya faida ya matamasha, kwa mfano asilimia 10, inaweza kuwekwa katika mfuko huo ili kuwasaidia wanapostaafu muziki au wanaposhindwa tena kufanya maonesho.
Nipo tayari kushirikiana nao katika kufafanua mapendekezo haya, ikiwemo kusaidia kuandaa mapendekezo ya kuomba udhamini wa matamasha yao.
Issaya Lupogo (PhD) Mhadhiri Mwandamizi wa Kiswahili Chuo Kikuu Mzumbe anapatikana kupitia 0712143909