R Kelly amtetea P Diddy akiwa gerezani

Muktasari:

  • Katika sauti ya R.Kelly ambayo amerekodiwa akiwa gerezani imesikika ikiwapa onyo wanaomcheka Diddy huku akidai kuwa wanaofanya hivyo hawajui kuwa yanaweza kuwakuta na wao wakati wowote. 

Mwanamuziki R.Kelly 4 ambaye kwa sasa yupo gerezani akitumikia kifungo cha miaka 30 baada ya kukutwa na hatia ya kuhusika kufanya unyanyasaji wa kingono kwa mabinti wadogo, wakati akifanya mahojiano na Wack100 kupitia (Club House) ametoa ushauri kwa baadhi ya watu wanaomcheka Diddy dhidi ya tuhuma anazopitia sasa.

Katika sauti ya R.Kelly ambayo amerekodiwa akiwa gerezani imesikika ikiwapa onyo wanaomcheka Diddy huku akidai kuwa wanaofanya hivyo hawajui kuwa yanaweza kuwakuta na wao wakati wowote. 

Amesikika akisema, "Hili jambo ni la kijinga, wapumbavu wapo tu huko wanacheka na kufanya utani wa vichekesho na kusema mambo yao kwenye redio, hawajui kuwa yanaweza kuwakuta muda wowote. Siamini kwenye huu upuuzi, unaweza kuniambia kuhusu [Puffy] au mtu mwingine yeyote, siwezi kuamini tena. Kwa sababu nipo kwenye hili, hivyo nafahamu walichofanya.” Amesema R. Kelly.

Kati ya watu ambao wamekuwa wakitoa maneno dhidi ya Diddy ni 50 Cent ambaye amewahi kuandika kupitia ukurasa wake  X kuwa:

"Sasa hivi siyo Diddy kafanya ni Diddy kamalizwa, huwa hawaji hivyo isipokuwa wamepata kesi."

Hii siyo mara ya kwanza 50 Cent  kutoa kauli na misimamo yake juu ya Diddy, kwani kila zilipokuwa zikiibuka tuhuma za mkali huyu 50 lazima atie neno kwa kugongelea misumari.