Rayvanny aliheshimisha Taifa Kombe la Dunia
Muktasari:
- Rayvanny alikuwa miongoni mwa wasanii waliopata nafasi ya kutumbuiza katika tamasha hilo maalumu linaloambatana na shamrashamra za Kombe la Dunia ambapo maelfu ya mashabiki kutoka mataifa mbalimbali walikusanyika kufurahia burudani na kusherehekea fainali hizo.
Canada. Msanii wa Bongo Fleva, Rayvanny ameendelea kupeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa baada ya kushiriki onyesho kubwa la muziki pamoja na nyota wa Canada na India, Nora Fatehi katika tamasha la 'FIFA World Cup Fan Festival' lililofanyika usiku wa kuamkia leo jijini Toronto, Canada.
Rayvanny alikuwa miongoni mwa wasanii waliopata nafasi ya kutumbuiza katika tamasha hilo maalumu linaloambatana na shamrashamra za Kombe la Dunia ambapo maelfu ya mashabiki kutoka mataifa mbalimbali walikusanyika kufurahia burudani na kusherehekea fainali hizo.
Rayvanny na Fatehi wakifanya onyesho la pamoja na moja ya nyimbo ambazo waliimba ni pamoja na Tetema. Wasanii hao walionesha maelewano mazuri jukwaani huku wakiwafanya mashabiki kushiriki katika burudani hiyo.
Katika moja ya sehemu za kuvutia za onyesho hilo, Rayvanny na Fatehi waliwasihi mashabiki waliokuwa ukumbini kuonesha mapenzi yao kwa jiji la Toronto na tamasha hilo kwa kushangilia kwa nguvu, jambo lililosababisha umati mzima kulipuka kwa shangwe.
Mwitikio wa mashabiki ulionyesha jinsi tamasha hilo lilivyofanikiwa kuwaleta pamoja watu kutoka tamaduni, mataifa na lugha tofauti.
Kwa Rayvanny, ushiriki wake katika tamasha hilo ni mwendelezo wa juhudi zake za kuutangaza muziki wa Tanzania katika majukwaa makubwa ya kimataifa.
Katika miaka ya karibuni, msanii huyo amekuwa akifanya maonesho katika nchi mbalimbali duniani, hatua iliyomsaidia kupanua wigo wa mashabiki wake na kuifanya Bongo Fleva kuendelea kupata nafasi katika soko la kimataifa.
Mafanikio hayo yanaongeza kwenye rekodi ya Rayvanny ya kushiriki matukio makubwa. Ikumbukwe kuwa Julai, 2025 alitumbuiza katika sherehe za ufunguzi wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), mashindano yaliyofanyika kwa mara ya kwanza kwa mfumo wa ushirikiano wa nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.
Mbali na Rayvanny na Fatehi, jukwaa hilo pia lilipambwa na mastaa wengine wa muziki duniani akiwemo Michael Buble, Alessia Cara, Alanis Morissette, Jessie Reyez, Elyanna, Vegedream, Sanjoy na William Prince.