Rihanna anataka mtoto wa kike

Muktasari:

  • Rihanna, 36, na mpenzi wake A$AP Rocky, 35, walithibitisha uhusiano wao mnamo Novemba 2020 wakiwa visiwa vya Barbados, tayari wamejaliwa watoto wawili, RZA aliyezaliwa Mei 2022 na Riot aliyezaliwa Agosti 2023

Staa wa Pop duniani na mshindi mara tisa wa Grammy, Rihanna ambaye ni mama wa watoto wawili wa kiume, amesema angetamani kupata watoto zaidi ila kiu yake sasa ni kupata mtoto wa kike.

Rihanna, 36, na mpenzi wake A$AP Rocky, 35, walithibitisha uhusiano wao mnamo Novemba 2020 wakiwa visiwa vya Barbados, tayari wamejaliwa watoto wawili, RZA aliyezaliwa Mei 2022 na Riot aliyezaliwa Agosti 2023.  

Hata hivyo, ukaribu wa wawili hao ulianza kuonekana hadharani mwaka 2012 walipotumbuiza remix ya wimbo ‘Love It’ katika tuzo za MTV VMA, baadaye Rocky akaonekana katika video ya wimbo wa Rihanna, Fashion Killa (2013).

Katika mahojiano yake na Interview Magazine ambayo yamechapishwa mapema wiki hii, Rihanna amefunguka mambo mengi kuhusu malezi na familia, huku akigusia kiu yake ya kupata mtoto wa kike.

“Sijui Mungu anataka nini, lakini ningependa kuwa na watoto zaidi ya wawili. Nijaribu kupata msichana wangu, lakini bila shaka akiwa ni mvulana mwingine, basi ni mvulana wangu mwingine.” alisema Rihanna.

Mwimbaji huyo wa kibao maarufu, (2007) alipoulizwa na mwanamitindo Mel Ottenberg anataka kuwa na watoto wangapi maishani mwake, Rihanna alijibu. “Kadiri Mungu anavyotaka niwe nao”

Vilevile Rihanna aligusia uhusiano wake na A$AP Rocky ulivyo na nguvu katika malezi. “Mtu anapokuona na kukuamini, na kufikiria kuwa unastahili kuwa mama wa watoto wake, ni hisia nzuri. Nilihisi hivyo hivyo kumhusu, nilijua angekuwa baba bora”.

Kauli ya Rihanna inakuja baada ya awali A$AP Rocky kuulizwa iwapo kuna wimbo wa ushirikiano kati yake na mama watoto wake watakuja kuutoa na kusema ushirikiano pekee watakaofanya ni kuleta watoto duniani na sio kwenye muziki.

“Nadhani tunafanya kazi nzuri sana katika kushirikiana, kuzaa watoto. Nadhani huo ndio ubunifu wetu bora hadi sasa. Hakuna kitu bora kuliko hicho huko nje.” alisema A$AP Rocky aliyetamba na ngoma, Praise The Lord (2018).

Utakumbuka Rihanna alipata umaarufu duniani baada ya kuachia albamu yake ya tatu, Good Girl Gone Bad (2007), iliyokuwa na nyimbo kali kama ‘Rehab’, ‘Hate That I Love You’ na ‘Umbrella’.