Rose Manfere Miss World, mitandao ya kijamii ilivyohatarisha maisha yake

Muktasari:

  • Rose ambaye aliwakilisha warembo wote nchini kwa mwaka 2020, amesema alipoamua kuingia kwenye mashindano hayo ilimbidi asimamishe masomo akiwa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Ardhi Dar es Salaam, ili aweze kulitumikia taji kwa juhudi zote

Inaaminika mshika mawili moja humponyoka na hicho ndicho Miss Tanzania 2020 Rose Manfere, hakutaka kimkute wakati akianza safari yake ya kulisaka taji la urembo.

Rose ambaye aliwakilisha warembo wote nchini kwa mwaka 2020, amesema alipoamua kuingia kwenye mashindano hayo ilimbidi asimamishe masomo akiwa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Ardhi Dar es Salaam, ili aweze kulitumikia taji kwa juhudi zote.

“Nilivyoingia Miss Tanzania nilisimama kimasomo kwa mwaka mmoja ili nipate muda, lakini nilikuja kurudi tena shule mwaka 2021,” anasema.

Hatosahau tukio hili
 

Changamoto humkuta kila binadamu kwa upande wake Rose anasema kati ya changamoto ambayo hawezi kuisahau katika maisha yake ni alivyozuiwa kwenda kuiwakilisha Tanzania Miss World 2021, kwani ilimsababishia matatizo ya afya ya akili.

“Kipindi Miss Tanzania wametangaza kwamba sitaingia Miss World hiyo ni changamoto ambayo nimepitia na ni kubwa sana, lakini namshukuru Mungu nilikabiliana nayo, ilifika wakati nikasema kama sitakiwi kuendelea kuishi. Ilikuwa ni ngumu hadi wakati mwingine kuamka kuendelea na maisha,”anasema.

Anaeleza kilichokuwa kikimuumiza zaidi na kumpa matatizo ya afya ya akili ni kutokuwa na uhakika kama atakwenda Miss World ama hatoenda, huku kingine kikiwa mitandao ya kijamii.

“Kilichokuwa kinaniumiza ni kutoelewa kama naenda Miss World ama siendi, kwa sababu upande wa Basata wanasema hivi na upande wa Organization wanasema hivi, ile ilikuwa inaniathiri sana nilitaka kuwa na uhakika nini tamko la mwisho.

“ Vitu vilikuwa vimesambaa kwenye mitandao watu wanaongea wanavyotaka kwa hiyo kulikuwa na kitu kama aibu, nikikutana na watu nilikuwa nahisi kila mmoja ananijua ananiongelea vibaya, ndiyo vitu vilivyokuwa vinaniumiza  hata nikimuona mtu anafurahi mimi nakuwa sina amani, inaniumiza,”anasema.

Mbali na aliyopitia katika maisha hata alivyorudi chuo  mwaka 2021, anasema changamoto bado ilikuwa inaendelea.  

“Ilitokea natakiwa kurudi  shule mwaka 2021  baada ya vile vitu vyote kuvipitia, ilikuwa ni kazi ngumu kuirudisha akili shule ikabidi nianze kupambana  kwa sababu mwaka mzima nilikuwa nimekaa nyumbani kwenye maisha ya shida na taabu.

“Akili yangu ilikuwa haipo sawa haikuwa na uwezo wa kuzingatia kwenye kitu fulani, ilikuwa imepita muda lakini kuweza kuirudisha akili, kusimama kwenye kitu kimoja ilikuwa ngumu sana, naweza nikaingia darasani naelewa kinachofundishwa vizuri lakini nikitoka sielewi tena nilikuwa nahisi kama ubongo unacheza,” anasema.

Licha ya changamoto hizo anasema alikutana na watu wakamsaidia  kuwa kawada hadi akafanikiwa kumaliza chuo mwaka 2023.

“Uzuri nilikutana na watu, walinipa ushirikiano mzuri chuo, walinikubali kama nilivyo na mimi nikawatengenezea mazingira kwamba mpo na Rose na siyo Miss Tanzania  kwa hiyo walinipokea kama nilivyo, wakaanza kunilazimisha tusome haikuwa rahisi lakini walinisaidia sana, pia walimu walijaribu kwa nguvu kuniweka kwenye mstari wa masomo”,anasema.

Kilichosaidia afya yake ya akili

“Kwanza nilikubali kwamba napitia wakati mgumu na ninaumia kwa hiyo nikaanza kujiuliza nini nataka kwa sababau ukiwa kwenye matatizo ya afya ya akili unakuwa unaathirika hata nje, nilikuwa naumwa najiuliza nataka nini kwenye haya maisha.
“Nilianza kutafuta njia, nikamuona therapist, wazazi wangu wananipa ushauri , kuwa karibu na Mungu, kupitia madaktari nakumbuka Dk Isaac Maro alinisaidia sana haikuwa rahisi”,anasema.

Utakumbuka Rose hakufakiniwa kwenda kuiwakilisha Tanzania Miss World 2021, nchini  Puerto Rico kutokana na kile kilichodaiwa kuwa alikiuka baadhi ya masharti ya mkataba  badala yake alichaguliwa mshindi wa pili Juliana Rugimisa, kuwakilisha Taifa katika  mashindano hayo.

Muziki anauweza

Kama ilivyofanywa na baadhi ya warembo baada ya kunyakua taji la Miss Tanzania ama kushiriki mashindano hayo wanajikita kwenye tasnia nyingine ikiwemo muziki na maigizo, Rose anasema ana kipaji cha uimbaji na anaweza kuingia kwenye fani hiyo.

“Mimi nina vipaji vingi siyo kama najisifu kwenye movie nimewahi kufikiwa, lakini kwenye muziki watu wameanza kuniona tayari,  siwezi kujua maisha ya mbele yatakuwaje lakini naweza kuingia kwenye movie au muziki lakini naweza kuonekana naimba na nikiingia kwenye muziki wa Bongo Fleva,”anasema.

Kwenye siasa kamtaja Jokate

“Ukiingia kwenye Miss Tanzania jamii ni kitu ambacho hauwezi kuepuka, kupitia Chama cha Mapinduzi CCM kimeweza kunisaidia kuifikia jamii kwa karibu.

Naweza kuingia kwenye siasa kuwa mheshimiwa fulani lakini kwa sasa siwezi kuzungumzia sana kwa sababu ndiyo kwanza  najifunza, uongozi unataka uwe ngangari,  nimekuwa nikimuangalia zaidi Jokate Mwegelo  kwenye upande huo,” anasema.

Haukosi vitu hivi kwenye pochi ya Rose

Kama ilivyo kawaida kwa baadhi ya wanawake kutembea na pochi iliyojaa vitu vingi, hata vile visivyotumika kwa wakati huo mrembo huyu amesema kwa upande wake vipo vitu ambavyo havikosekani kwenye pochi yake.

“Mimi kitu cha kwanza ambacho huwezi kukikosa ni taulo za kike ‘pads’, cha pili, lip gloss  za aina mbalimbali, na simu yangu.”
Make up siyo ishu

Anasema make-up kwake siyo ishu kwani anaweza kwenda sehemu yoyote bila kujiremba  na amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara lakini kitu ambacho hawezi kuacha kukifanya ni kupaka kilainishi midomo ‘lip gloss’.

“Lip gloss, kwa sababu lips zangu zinakauka sana kwa hiyo nisipopaka mara kwa mara  nakuwa najisikia vibaya yani hata nikitoka nyumbani sijapaka nyingine ipo kwenye gari kwa hiyo inaninyimaga amani sana.

“Lakini upande wa make-up mimi siyo mtu wa kupaka sana kwa sababu naenda sehemu yoyote bila kupaka na mwisho tu jana nilikuwa na mizunguko yangu sijapaka,”anasema.

Anatumia mkwanja mrefu kwa ajili ya vitu hivi

“Nguo ambayo ilikuwa ya bei ukiachana na ninazovaa ni ile niliyovaa wakati wa kuvua taji ya zamani kidogo lakini ilikuwa ya bei sana nilinunua Sh 2 milioni.

“Kiatu cha bei nilichowahi kununua ni cha Sh 1.5 milioni, nilikivaa kwenye steji ya kumtafuta mrembo wa Miss Tanzania 2022, kina kamba kamba zimezunguka mguu kupanda juu.
“Nywele kidogo ni kipengele kwa sababu bei zake zipo juu lakini ipo ambayo nilinunua 5 milioni,” anasema.

Kupunguza kilo mtihani

Baadhi ya wanawake wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kwa ajili ya kupunguza uzito na vitambi, kutokana na hilo Rose amesema hilo ni jambo gumu na linahitaji kufanywa kwa muendelezo.

“Kwanza kwa warembo ambao wana mwili mkubwa wanatamani kuwa wembamba ni kazi ngumu sana kufanikiwa.

 “Nawaelewa sana ambavyo wanahangaika kufanya vitu ikiwemo kunywa dawa, lakini ushauri wangu   wanatakiwa kufanya mazoezi , kupunguzo  mlo, kunywa maji mengi yanasaidia sana”,anasema

Kwa upande wake anasema kilo nyingi ambazo amewahi kufikia ni 60 lakini kwa sasa ana 57.

Ushauri wake

“Kwanza wasichana wanatakiwa wasikilize sauti zao halafu jaribu, thubutu usikae na kitu anza, ukiweza kufanya kitu kimoja kinaweza kukufungulia vitu vingine, mfano mimi nilikuwa naimba lakini kupitia Miss Tanzania ndiyo nikajua naimba kweli, wanawake na wasichana waangalie fursa walizonazo, kila kitu kinawezekana kwa juhudi na mikakati”anamalizia.