Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Safari ya Shetta kimuziki kabla ya uongozi

Muktasari:

  • Shetta, mkali wa kibao cha Hatufanani (2018), hadi anakuja kushika nafasi hiyo ya uongozi tayari jina lake lilikuwa chapa inayojiuza katika muziki kupitia nyimbo zake mahiri na maarufu zilizozungumzia mapenzi, starehe na maisha kwa ujumla.

Dar es Salaam. Wikiendi iliyopita nilimuona Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Juma maarufu kama Shetta akitumbuiza katika show ya kuadhimisha miaka 30 ya Bongofleva, kisha nikakumbuka safari yake ya muziki ilivyokuwa.


Shetta, mkali wa kibao cha Hatufanani (2018), hadi anakuja kushika nafasi hiyo ya uongozi tayari jina lake lilikuwa chapa inayojiuza katika muziki kupitia nyimbo zake mahiri na maarufu zilizozungumzia mapenzi, starehe na maisha kwa ujumla.


Hata hivyo, haikuwa rahisi kuwa Shetta kwani katika safari ya muziki alilazimika kushirikiana na watu mbalimbali ili kutimiza ndoto yake, miongoni mwao ni Pancho Latino, Mona Gangster, Belle 9 na Dully Sykes, ambao walisaidia jina lake kufika kwenye masikio ya mashabiki wengi wa Bongofleva.


Vilevile makundi kama Misifa Camp na Dar Stamina, ni baadhi ya nguzo muhimu zilizomfikisha Shetta katika hatua aliyopo leo kimuziki, ingawa kwa sasa amejikita katika siasa ambapo pia ni diwani wa kata ya Mchikichini.



Mbali na mtindo wake wa kurap, Shetta alipendwa na wengi kwa uwezo wake wa kuchagua wasanii wa kushirikiana nao, jambo lililosaidia nyimbo zake nyingi kufanya vizuri kwa muda mrefu. Tunaweza kusema kila kolabo aliyofanya imekuwa na nafasi yake katika Bongofleva.


Alianza kurekodi muziki akiwa bado mwanafunzi wa shule ya msingi, ni katika studio aliyokuwa akiifanyia kazi Miikka ‘Mwamba’ Kari, mtayarishaji muziki kutokea Finland ambaye alikuja nchini kwa mara ya kwanza mwaka 1993.
Miikka Mwamba ambaye aliwatoa wasanii kama Daz Nundaz, Saida Karoli, Banana Zorro, Dully Sykes na wengineo, alikuja nchini kwa ajili ya kufanya mafunzo kwa vitendo (field) baada ya kuhitimu Chuo Kikuu aliposomea sanaa.


Sasa Shetta alipata nafasi ya kurekodi kwa Miikka Mwamba akiwa darasa la nne, na katika hatua hiyo za mwanzo, aliyekuwa mwimbaji na kiongozi wa bendi ya The African stars (Twanga Pepeta), Ali Choki ndiye aliyemsaidia Shetta kulipia kugharama za kurekodi.


Vilevile Shetta aliwahi kuwa dansa wa Dully Sykes chini ya Misifa Camp lakini alipoanza kuimba ndipo kipaji chake kilipoanza kuonekana zaidi na kumfanya ajulikane na mashabiki wengi kupitia kundi la Dar Stamina.
Hatimaye Shetta alikuja kutoka kimuziki kupitia wimbo wake, Nimechokwa (2011) ambao ulitayarishwa na Mona Gangster pamoja na Pancho Latino, huku Belle 9 akishirikishwa ambapo alikipa ladha nzuri kiitikio cha wimbo huo wa rap.


Lakini awali Shetta alishatoa wimbo, Me na Play (2010) akimshirikisha Mwana FA (Hamis Mwinjuma) ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo. Ngoma hiyo iliyotayarishwa AM Records, ilikuja kupata remix yake ambapo Godzilla, Belle 9 na Nikki Mbishi waliongezeka.


Baada ya Shetta kutamba na ngoma, Nimechokwa (2011), muda mfupi baadaye alivuma na wimbo wake mwingine, Madananda (2011) awamu hii akiwashirikisha Tundaman na Dully Sykes. Ni wimbo ambao Dully Sykes alishiriki kuutayarisha katika studio yake ya Dhahabu Records, sasa studio 4.12, huku akishirikiana na Pancho Latino.


Hivyo kati ya watayarishaji muziki wenye mchango mkubwa katika safari ya Shetta ni pamoja na Pancho Latino ambaye sasa ni marehemu. Enzi za uhai wake Pancho alifanya kazi Dhahabu Records, kisha baadaye akaja kuhamia B’Hits (sasa Bxtra) kwa Hermy B.



Kwa mujibu wa Shetta, baada ya kuachia wimbo huo (Madananda), ndipo kwa mara ya kwanza alianza kufanya show kwa bei ya zaidi ya Sh1 milioni kutoka Sh400,000. Kuanzia hapo kila kitu kilibadilika kwake kuanzia kimuziki hadi kiuchumi.


Nyimbo zake nyingine zilizofanya vizuri ni pamoja na Nidanganye (2012) na Kerewa (2014), zote akimshirkisha Diamond Platnumz. Nyingine ni Sina Imani (2013) akiwa na Rich Mavoko, na Shikorobo (2015) akishirikiana na Kcee kutokea Nigeria.


Kwa mara ya mwisho Shetta alifanya vizuri zaidi na wimbo wake, Hatufanani (2018) akiwa na Mr. Blue na Jux huku Kimambo Beats akihusika upande wa utayarishaji. Huu ndio wimbo wa Shetta uliofanya vizuri zaidi YouTube (most viewed) ambapo video yake imeshatazamwa mara milioni 6.4.


Baada ya hapo Shetta alitoa kazi chache kutokana alianza kufanya miradi ya kijamii kupitia shirika lake liitwalo SAWA ambalo linalenga kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Kisha akaingia kwenye siasa na sasa ni diwani wa kata ya Mchikichini, na Meya wa Jiji la Dar es Salaam.