Sauti za Busara kuanza leo na vipaji vya nyumbani

Unguja. Baada ya miaka 19 ya mafanikio, leo Ijumaa Februari 10, katika eneo la Ngome Kongwe, Stone Town, litashuhudia tamasha la 20 tangu kuanzishwa kwake.

Kikundi cha DCMA Young Stars, ambao ni watoto wadogo wenye vipaji kutoka shule tofauti visiwani Zanzibar watatumbuiza wakiwa na wanamuziki na walimu kutoka Chuo cha Muziki cha Dhow Countries cha visiwani hapa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf Mahmoud leo ni siku ya kwanza kati ya siku tatu za kusherehekea muziki wa Kiafrika na utofauti wa kiutamaduni huku wasanii mbalimbali kutoka barani Afrika wakipamba katika majukwaa mawili.

Mbali na majukwaa mawili ndani ya Ngome Kongwe, kwa mara ya kwanza, tamasha hilo pia Jumamosi Februari 11, litaandaa maonyesho kadhaa ya bila malipo wakati wa mchana katika Mji wa Fumba, mradi ulio chini ya CPS.

Akizungumza visiwani Zanzibar, Mkurugenzi wa tamasha hilo, Yusuf Mahmoud amewataka Watanzania kujumuika na wageni wengi ambao tayari wamefika kutoka kila pembe ya dunia kushuhudia na kushiriki katika tamasha hilo la kipekee.

"Leo, tunaanza kwa uzoefu wa kipekee na wa ajabu wakati Zanzibar ikiandaa siku tatu zitakazobeba asilimia 100 ya muziki wa Kiafrika. Tunajivunia kwa mwaka huu kuadhimisha tamasha la 20, tukiwa na orodha bora zaidi ya wanamuziki itakayowaridhisha wahudhuriaji kutoka katika kila kona ya dunia,” amesema Mahmoud.

Mahmoud amesema miongo miwili ya burudani imefanya Sauti za Busara kuwa moja ya matamasha yanayoheshimika zaidi ya muziki wa Kiafrika lililooendelea kufanyika, hata katika miaka yote ya changamoto ya janga la Uviko-19.

“Kwa miongo miwili sasa, tumeonyesha uthabiti na wepesi katika kusaidia wasanii, huku tukisisitiza nguvu na ushawishi wa muziki itumike kukemea maovu katika jamii yetu.Kwa kutambua ukweli kwamba Afrika ni bara kubwa lenye historia na tamaduni tofauti na matarajio ya pamoja, onyesho la mwaka huu linafanyika chini ya kaulimbiu ‘Utofauti Wetu ni Utajiri Wetu.” amesema.

Kwa upande wa Meneja wa tamasha hilo, Journey Ramadan aliwataja baadhi ya wasanii waliowahi kupamba jukwaa la Sauti za Busara, “Tumeandaa matamasha na kuwa na mamia ya vikundi, lakini kuna wale ambao wameacha gumzo kwa mfano, mwanamuziki mkongwe kutoka Zanzibar Marehemu Bi Kidude, Sampa The Great (Zambia), Nneka (Nigeria), Bassekou Kouyate (Mali), Blitz the Ambassador (Ghana), Sarabi (Kenya), Samba Mapangala (DRC), Ba Cissoko (Guinea), Sholo Mwamba, Saida Karoli na Jagwa Music (Tanzania). "Wanamuziki hawa walipendwa na karibu kila mtu,” amesema Journey Ramadhan.

Tamasha la mwaka huu lisingewezekana bila ufadhili wa Fumba Town- CPS, ambao walikuja kuokoa tamasha hili baada ya wafadhili wa awali kujiondoa kutokana na mazingira yaliyokuwa yamegubikwa na sintofahamu.

Akizungumza katika , Mkurugenzi Mtendaji wa CPS-Fumba Town, Sebastian Dietzold alisema wanajivunia kuwa sehemu ya tamasha kubwa zaidi la muziki barani Afrika ambalo kwa miaka mingi limeacha kumbukumbu za kudumu.

"Jinsi Sauti za Busara inavyoleta watu mbalimbali kutoka nchi mbalimbali kusherehekea muziki wa tamaduni mbalimbali, Fumba Town pia inawaleta pamoja watu kutoka nchi na tamaduni mbalimbali kununua na kufurahia nyumba za makazi na likizo za bei nafuu Zanzibar," amebainisha.