Selena Gomez anapaswa kumshukuru Rema

Muktasari:
- Hiyo ni baada ya mafanikio makubwa ya wimbo wao, Calm Down (2022) ambao umevunja rekodi mbalimbali za mauzo duniani na kuongoza chati nyingi kubwa za muziki ikiwemo Billboard Us Afrobeats Songs.
Dar es Salaam. Staa wa Pop Marekani, Selena Gomez, 32, akiwa na miaka zaidi ya 10 katika muziki, ana mengi ya kushurukuru katika safari yake hiyo na mojawapo ni kukutana na mwanamuziki mwenzake kutokea Nigeria, Rema, 25, anayesimamiwa na Mavin Records.
Hiyo ni baada ya mafanikio makubwa ya wimbo wao, Calm Down (2022) ambao umevunja rekodi mbalimbali za mauzo duniani na kuongoza chati nyingi kubwa za muziki ikiwemo Billboard Us Afrobeats Songs.
Ikumbukwe Selena baada ya kupata umaarufu katika filamu, alijikita katika muziki na albamu yake ya kwanza, Stars Dance (2013) iliongoza chati za Billboard 200, huku wimbo wake wa kwanza ‘Come & Get It’ ukiingia 10 bora katika Billboard Hot 100.

Tayari ametoa albamu nyingine mbili ambazo ni Revival (2015) na Rare (2020), huku katika kundi lake la Selena Gomez & the Scene wakitoa albamu tatu ambazo zilitangulia kutoka.
Kwa sasa akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 418 katika mtandao wa Instagram, Selena amewahi kutajwa na Billboard kama mwanamke wa mwaka 2017, huku Time wakimtaja kuwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani kwa mwaka 2020.
Tukirejea katika muziki wake, kwa sasa ukitazama chaneli yake ya YouTube, utabaini ni video ya wimbo mmoja pekee ndiyo imetazamwa zaidi ya mara bilioni, nayo ni ya wimbo ‘Calm Down’ ambao alishirikiana na Rema.

Ikumbukwe takribani miaka minne baada ya kusainiwa na lebo ya Mavin Records, Rema alitoa albamu yake ya kwanza, Rave & Roses (2022) ambayo ilifanya vizuri ikishika namba 81 katika chati ya Billboard 200.
Ndani ya albamu hiyo ulikuwepo wimbo mmoja uliobadilisha historia na kuikuza zaidi chapa ya Rema kimataifa, wimbo sio mwingine bali ndio huo ‘Calm Down’ ambao uligeuka gumzo katika nchi nyingi barani Afrika.
Ukiwa bado wa moto, Rema alitoa toleo la pili (remix) na kumshirikisha Selena Gomez, ni kazi iliyofanya vizuri ikishaka namba tatu Billboard Hot 100 na namba moja U.S. Billboard Afrobeats Songs, chati iliyoanza miaka minne iliyopita kwa ajili ya muziki wa Afrika.

Huu ndio wimbo wa kwanza Afrika kusikilizwa (streams) zaidi ya mara bilioni 1 katika mtandao wa Spotify, na kwa ujumla video yake YouTube imetazamwa zaidi ya mara bilioni 1.1 ndani ya miaka miwili ikiwa ni video ya kwanza Afrika kufikia namba hizo.
Pia wimbo huo ulishinda tuzo ya MTV Video Music Awards 2023 huko Marekani katika kipengele cha Wimbo Bora wa Afrobeats, na Rema kusema alijua ungefanya vizuri na kumshuruku Selena kwa kushiriki katika kazi hiyo.
“Ninaamini kuwa kila kitu ninachofanya ni maalum, nyimbo tofauti zitasikika kwa watu tofauti, nilipoingia studio kwa kweli nilikuwa nikiimba ukweli wangu, nilifanya kile ambacho nilipaswa kufanya,” alisema Rema katika mahojiano na mtandao wa People.
Ikumbukwe Rema alianza muziki katika makanisani ya Alpha P, chapisho lake la video katika mtandao wa Instagram akiimba wimbo wa D’Prince, Gucci Gang (2018) lilivutia usikivu wa D’Prince na kusafirisha hadi Lagos na kumpa Rema ofa.

Na ofa yenyewe ni kujiunga na Jonzing World ambayo ni kampuni tanzu ya Mavin Records inayomilikiwa na Don Jazzy. Rema alikubali ofa hiyo na kisha kutoa wimbo wake, Dumebi (2019) ambao ulimpatia mashabiki wengi.
Mavins Records iliyoanzishwa Mei 2012 ikiaanza na wasanii kama Tiwa Savage, Wande Coal, Reekado Banks na Iyanya, kwa sasa inawasimamia kina Ayra Starr, Crayon, Johnny Drille, Ladipoe, Magixx, Boy Spyce, Bayanni na Lifesize Teddy.
Mbali na muziki, Selena ni mwigizaji na ndio kazi iliyomtambulisha duniani, alianza uigizaji kwenye kipindi cha runinga cha watoto, Barney & Friends mwaka 2002 hadi 2004, kisha kuibukia kipindi cha Disney, Wizards of Waverly Place.
Na hadi sasa amecheza filamu maarufu kama Cinderella (2008), Wizards of Waverly Place: The Movie (2009), Ramona and Beezus (2010), Monte Carlo (2011), Spring Breakers (2012), Majirani 2: Sorority Rising (2016), The Dead Don’t Die (2019) n.k