Siku 1,460 za Queen Darleen nje ya studio

Muktasari:

  • Kwa mara ya mwisho Queen Darleen kusikika ndani ya Bongo Fleva ilikuwa ni Aprili 1, 2020 alipoachia video ya wimbo wake ‘Bachela’ ambao amemshirikisha Lava Lava, huku Aby Dady na Rash Don wakihusika katika utayarishaji.

Mwimbaji wa Bongo Fleva na ‘First Lady’ wa WCB Wasafi, Queen Darleen rasmi ametimiza miaka minne sawa na siku 1,460 akiwa nje ya Bongo Fleva kitu ambacho ni mara ya kwanza kuonekana kwa wasanii waliochini ya rekodi lebo hiyo.  

Kwa mara ya mwisho Queen Darleen kusikika ndani ya Bongo Fleva ilikuwa ni Aprili 1, 2020 alipoachia video ya wimbo wake ‘Bachela’ ambao amemshirikisha Lava Lava, huku Aby Dady na Rash Don wakihusika katika utayarishaji.

Darleen, 38, alisainiwa WCB Wasafi hapo Juni 2016, akiwa ni msanii wa kwanza wa kike katika lebo hiyo ya Diamond Platnumz ambapo alimkuta Harmonize, kisha Rayvanny na Rich Mavoko wakaja baadaye.

Tangu kuanza kusaini wasaniii mwaka 2015, hajawahi kutokea msanii wa WCB Wasafi kukaa zaidi miaka minne bila kutoa kazi mpya au hata kushirikishwa na msanii mwingine wa ndani ya lebo hiyo, ndio mara ya kwanza hilo linatokea.

Kinachoshangaza wengi ni kwamba Queen Darleen bado ni msanii wa WCB Wasafi kwa mujibu wa tovuti rasmi ya lebo hiyo lakini amekuwa kimya, huku akifuta picha zote katika ukurasa wake wa Instagram.

Hadi sasa Queen Darleen ametoa nyimbo saba pekee chini ya Wasafi akiwa ndiye msanii pekee aliyetoa nyimbo chache zaidi kuliko yeyote yule licha ya kuwepo katika lebo hiyo kabla ya Rayvanny, Rich Mavoko, Lava Lava, Mbosso, Zuchu na D Voice.  

Lakini tangu kusainiwa kwa Zuchu ndani ya WCB Wasafi hapo Aprili 2020, akiwa kama msanii wa pili wa kike, Queen Darleen hajatoa wimbo wowote, tunaweza kusema ameamua kumpisha Zuchu moja kwa moja.
Kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu chini ya WCB Wasafi, Zuchu amesharikiana na 
Diamond katika nyimbo tatu, Litawachoma (2020), Cheche (2020) na Mtasubiri (2022), lakini Queen Darleen hajawahi kufanya kolabo yoyote na Diamond!.

Wasanii wote waliomkuta WCB Wasafi wamefanya kazi nyingi na Diamond na kuwatangaza vizuri ila kwa Queen Darleen kufanya kazi na Diamond ni hadi pale wanaporekodi wimbo wa lebo kama Zilipendwa (2017) na Quarantine (2020).

Hata hivyo, Septemba 2013 kabla ya kusaini WCB Wasafi, Queen Darleen alizungumzia suala la kufanya kazi na Diamond na kusema anamchukulia kama mdogo wake, hivyo akifanya naye wimbo kwa wakati huo atapoteza maana nzima ya undugu wao.

“Kila siku akija namwambia bado, bado kufanya wimbo na mimi, najua kwamba yupo juu zaidi yangu lakini ‘still’ kwangu yupo chini sababu mimi ni Dada yake na ananiheshimu.” alisema Queen Darleen.

Hadi sasa huyu ndiye msanii pekee WCB Wasafi ambaye hajatoa albamu wala EP wakati wenzake wamefanya hivyo, mfano Lava Lava (Promise EP), Zuchu (I Am Zuchu EP), Mbosso (Khan EP & Definition of Love Album) na D Voice Swahili Kid (Album).

Kwa mujibu wa Darleen, alikuwa ni mfanyakazi wa kawaida ndani ya WCB Wasafi na alikuwa akilipwa mshahara kama wafanyakazi wengine na Diamond alikuwa ameshiriki kubadilisha maisha yake kwa asilimia kubwa.

“Kabla ya kusaini Wasafi maisha yangu yalikuwa yameshabadilika, Diamond tayari alikuwa ameshanibadilishia maisha yangu, nilikuwa nafanya kazi mbalimbali ndani ya WCB na nilikuwa nalipwa, kama zile ‘behind the scenes’ nilikuwa nazisimamia.” alisema.

Na kwa kipindi chote, Darleen ndiye msanii pekee wa WCB Wasafi ambaye hajafanya kolabo na msanii yeyote wa kimataifa, yaani hajawahi kushirikiana na msanii kutoka nje ya Tanzania.

Mathalani, Diamond (Ne-Yo, Marekani), Harmonize (Burna Boy, Nigeria), Rayvanny (Maluma, Colombia), Rich Mavoko (Patoranking, Nigeria), Lava Lava ( KRG The Don, Kenya), Mbosso (Reekado Banks, Nigeria) na Zuchu (Innoss’B, Nigeria).

Ikumbukwe Darleen alivuma zaidi kimuziki alipoachia wimbo wake, Wajua Nakupenda (2006) chini ya G Records akimshirikisha Staa wa Kings Music, Alikiba. Baadaye alikuja kutamba tena na wimbo, Maneno Maneno (2011) ulioshinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2012 kama Wimbo Bora wa Ragga & Dancehall.