Snura awaziba midomo waliomtabiria kushindwa
Muktasari:
- Hilo ni jambo jema na limewafunga midomo ambao walimtabiria mabaya pindi alipotangaza kuachana na muziki pamoja na filamu, wakidai hataweza fikisha hata miezi miwili na kurudi katika kazi yake muziki.
Dar es Salaam. Moja ya habari njema inayopendwa kuzungumziwa ni ya aliyewahi kuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya hususani singeli na filamu, Snura Mushi kuwa ameishika dini vilivyo, ikiwa kwa sasa ametimiza mwaka na nusu.
Hilo ni jambo jema na limewafunga midomo ambao walimtabiria mabaya pindi alipotangaza kuachana na muziki pamoja na filamu, wakidai hataweza fikisha hata miezi miwili na kurudi katika kazi yake muziki.
Snura alipiga stori na Mwananchi na kusema hawezi kurudi nyuma kama baadhi ya watu walivyomtabiria, hivyo amewasamehe wote waliomtabiria kutofikisha miezi miwili kwenye uamuzi wake wa kumrudia Mungu.
“Mimi sijawahi kutetereka kama baadhi watu walivyokuwa wakinifikiria kuwa sitaweza kuvuka miezi hata miwili au mitatu kwa uamuzi wangu kumrudia Mungu na kuacha sanaa, niwaambie tu maji nishayavulia nguo lazima niyaoge, nilijipanga kabla ya kutangaza uamuzi wangu na ndio maana nimeweza hadi kufikisha huu mwaka na miezi yake, namuomba Mungu niendelee hivi hivi kwani Sina mpango wa kurudi nyuma,” amesema Snura.
Snura ambaye alianza kutamba kwenye sanaa ya uigizaji kisha kugeukia muziki, alitangaza kuacha rasmi muziki na shughuli za kisanaa na kujikita kwenye suala kumuabudu Mungu Julai 30, 2024.
“Nimeamua kuacha muziki kwa sababu ya nia ya kurudi kwenye njia ya haki, njia ya kumuabudu Mwenyezi”, amesema Snura siku alipotangaza kuacha muziki.