Tofauti ya Kajala na Paula iko hapa

Paula! Na mabinti wengine wa kizazi cha miaka ya 2000. Wana tofauti kubwa na Kajala na mabinti wa kizazi cha miaka ya 1990 kushuka chini. Na tofauti yao ipo katika malezi tu.

Ndivyo ilivyo hata kwa watoto wa kiume pia. Kuna malezi flani hivi ya kizazi cha 2000, ambayo msingi wake haupo kwa wazazi bali dunia kwa ujumla. Utandawazi umebeba kila kitu.
Neno: "Kama hujafunzwa na mamayo utafunzwa na ulimwengu." Liweke kinyume chake yaani leo ni: "Kama hujafunzwa na ulimwengu, utafunzwa na mamayo." Ulimwengu unamfunda binti kabla ya mama yake.

Nyakati za kina Kajala, ilibidi umalize 'fomu siksi'. Uende 'Jeikatii' 'ujimiksi' na walimwengu. Leo inabidi umalize chuo ndipo 'ujimiksi' na mama yako. Ndio! Binti toka 'nasare' yupo 'bodingi' kama yatima vile.

‘Anavunja ungo’ akiwa na walimwengu. Anafundwa mambo mengi ya kikeni akiwa na walimwengu. Mama anapewa taarifa tu. Hana analojua juu ya bintiye zaidi ya kwenda 'benki' kutoa pesa na kulipa ada. Kizazi cha Mama Paula yaani Kajala, waliishi na wazazi kama jeshini. Mtoto ukiamka tu na usiposalimia wakubwa unapigwa. Usiposalimia wageni ama wakubwa njiani unakula 'stiki' za kutosha.

Ukinawa kabla ya wageni unapigwa. Ukilia bila sababu unapigwa. Ukilia kwa sababu unapigwa. Ukinyanyuka wakati wa kula kabla ya wakubwa unapigwa. Wakubwa wakiwa wamekaa wewe ukasimana pembeni yao unapigwa.
Ukikaa wakati wakubwa wamesimama unapigwa. Ukitumwa dukani ukachelewa kurudi unapigwa. Ukichelewa kurudi toka shuleni unapigwa. Ukiwahi kurudi kutoka shuleni unapigwa.
Ukililia wageni wakati wanaondoka, wakitoka unapigwa. Kujipitisha pitisha wageni wakiwa wanakula unapigwa.
Ukijibu ovyo wakubwa unapigwa. Kutukana watu wazima, watoto au rika lako unapigwa.
Ukiwa mbishi bila sababu unapigwa. Ukiwa mbishi kwa sababu pia utapigwa. Ukipigwa ukalia unapigwa ili unyamaze. Ukipigwa ukanyamaza utapigwa ili ulie. Ukipigwa shuleni au mtaani ukasemelea nyumbani, unapigwa tena na wazazi.
Ukianza kula nyama kabla ya wakubwa unapigwa. Ukila kwa jirani ukabainika unapigwa. Ukinawisha wenyeji kabla ya wageni mkimaliza unaitwa chumbani unapigwa. Ukinawisha watoto kabla ya wakubwa unapigwa.
Ukikutana na mtu mzima usipompokea mzigo, unapigwa. Ukienda kusema kama umepigwa unapigwa tena. Mtu mzima akipita sehemu mnayocheza halafu mkamkaushia unapigwa. Usipokula unapigwa ukila sana unapigwa.
Ukienda kwa watu, ukaona kitu au stori, ukaileta nyumbani unapigwa. Ukipewa hela na mtu asiyemjua au anayemjua inategemea mazingira gani, unapigwa. Ukianza kuchagua chagua chakula unapigwa.
Ukianza kuwa na marafiki wasioeleweka unapigwa. Mtu mkubwa akikuchongea nyumbani hata kama cha uongo tu, unapigwa. Ukikaa na wakubwa halafu ukaanza kucheka bila sababu unapigwa.
Ukimuuliza mkubwa umetoka wapi unapigwa. Ukipigwa na kususa kula unapigwa. Ukiitwa ukaenda kimyakimya bila kuitikia unapigwa. Ukila halafu ukaendelea na michezo unapigwa.
Siku hizi mitoto hulelewa kama neno la siri la benki au simu. Ukipiga toto la mtu kesi yake ni kubwa. Wakati zamani unaweza kutandikwa na yeyote mradi mkubwa. Na mzazi wako anamsisitiza huyo mtu akupige sana.
Wakati zamani watoto waliishi kama watu wazima kwa heshima na tabia. Leo watoto wanaishi kama watu wazima kwa starehe na uzinzi. Kila kitu hii leo kimepinduka kama tetemeko la Libya.
Wakati mwingine wazazi wa kizazi hiki, tunahitaji kupewa moyo. Maana tunalea watoto wenye kujua ya wakubwa kuliko wakubwa. Anachanganya na ulimwengu akiwa bado mtoto, anarudi na 'kokteli' ya tabia.