Ubabe wa Zuchu katika tuzo, digital streaming
Muktasari:
- Zuchu, mziwanda wa gwiji wa muziki wa Taarab nchini, Khadija Kopa, hapo Aprili 8, 2020, ndipo ukurasa wake mpya kimuziki ulifunguliwa baada ya kutambulishwa na rekodi lebo hiyo akiwa ni msanii wa saba.
Dar es Salaam. Ikiwa ni miaka zaidi ya sita tangu Zuchu alipotoka kimuziki chini ya WCB Wasafi, mwanamuziki huyo wa Bongofleva ameendelea kuonyesha ukubwa wake ndani na nje akiweka rekodi mbalimbali kupitia kazi zake.
Zuchu, mziwanda wa gwiji wa muziki wa Taarab nchini, Khadija Kopa, hapo Aprili 8, 2020, ndipo ukurasa wake mpya kimuziki ulifunguliwa baada ya kutambulishwa na rekodi lebo hiyo akiwa ni msanii wa saba.
Utambulisho wake uliambatana na EP yake ya kwanza, I Am Zuchu (2020) ambayo ilikuja na wimbo wake maarufu ‘Wana’ uliotayarishwa na Laizer Classic, huku video ikiongozwa na Director Kenny chini ya Zoom Extra.
Kufanya vizuri kwa EP hiyo, kulipelekea Zuchu kushinda tuzo ya African Muzik Mag-azine Awards (AFRIMMA) kutoka Marekani kama Msanii Bora Chipukizi 2020, na baadaye alishinda tuzo ya pili kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki 2022.
Kufuatia kurejea Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) tangu ziliposimama 2015, Zuchu ndiye msanii aliyeshinda mara nyingi zaidi licha ya kutoshiriki katika msimu wa kwanza ila hiyo miwili ya mwisho alifanya kweli akishinda tuzo saba kwa ujumla.
Wanaomfutia Zuchu kushinda tuzo nyingi za TMA tangu msimu wa 2021, ni Alikiba (6), Harmonize (6), Diamond (5), Nandy (4), Young Lunya (4), Marioo (4) na Phina (4) ambaye ni mshindi wa Bongo Star Search (BSS) 2018.
Hivyo tangu kurejea tena TMA, Zuchu ndiye msanii wa kike aliyeshinda tuzo nyingi kwa usiku mmoja, msimu wa 2022 alishinda tuzo tano ikiwa ni sawa na 20 Percent 2011 na Alikiba 2015 & 2021, na wote hawa wanaifukuzia rekodi ya Diamond aliye-shinda tuzo saba 2014.
Huyu ndiye mwanamuziki wa kwanza wa kike Tanzania kuchaguliwa kuwania tuzo za MTV Europe Music Awards (EMAs) ambazo hutolewa kila mwaka barani Ulaya.
Aliwania kipengele cha Msanii Bora Afrika 2021 akishindana na Ayra Star (Nigeria), Black Sherif (Ghana), Tems (Nigeria) Musa Keys (Afrika Kusini) na Burna Boy (Ni-geria) aliyeibuka mshindi.
Mnamo Desemba 2021, video ya wimbo wake, Sukari (2021) iliandika rekodi kama video ya muziki iliyotazamwa zaidi YouTube Afrika mwaka huo ikitazamwa zaidi ya mara milioni 60, huku ikifuatiwa na ile ya Wizkid na Tems, Essence (2021) ili-yotazamwa mara milioni 53.
Ikumbukwe Sukari ndio video ya kwanza kutoka kwa msanii wa solo Tanzania na Af-rika Mashariki kwa kutazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube ikifanya hivyo Machi 2024, kisha ikafuata Jeje (2020) yake Diamond Platnumz hapo Agosti 2024.
Kabla ya hapo, video za nyimbo zote zilizotazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 100 ni zile ambazo walishirikiana wasanii kuanzisha wawili, nazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019) na Waah! (2020) zake Diamond, na Kwangwaru (2018) yake Harmonize.
Ingawa aliyakuta majina mengi makubwa katika Bongofleva, kwa sasa Zuchu ndiye msanii wa kike aliyetazamwa zaidi (most viewed) YouTube kwa muda wote ambapo kazi zake kwa ujumla zimeshatazamwa zaidi ya mara bilioni 1.2.
Kwa ujumla Zuchu anashika nafasi ya nne Tanzania nyuma ya Harmonize (bilioni 1.5), Rayvanny (bilioni 1.9) na Diamond Platnumz (bilioni 3.7) ambaye ni namba mbili Afrika kwa kutazamwa zaidi YouTube nyuma ya Burna Boy (bilioni 3.9) kutokea Ni-geria.
Huyu ni mwanamuziki wa pili Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuwa na wafuasi (subscribers) wengi YouTube akiwa nao milioni 4.8, akiwa ametanguliwa na mshindi wa Grammy mara mbili kutokea Afrika Kusini, Tyla ambaye ana milioni 5.9.
Akiwa na albamu moja, Peace and Money (2024), Zuchu ndiye mwanamuziki wa kike Tanzania aliyesikilizwa (most streamed) zaidi katika mtandao wa Boomplay Music, tayari nyimbo zake zimesikilizwa zaidi ya mara milioni 450.1 huku akipata wafuasi 163,000 katika jukwaa hilo.
Kwa ujumla Zuchu anashika nafasi ya pili kwa kusikilizwa zaidi Boomplay nyuma ya Diamond, kisha nafasi ya tatu ni Rayvanny, Mbosso, Jay Melody, Marioo, Alikiba, Nandy na Jux, mshindi wa Trace Awards 2025 kama Msanii Bora wa Kiume.
Ikumbukwe albamu yake hiyo ilishirikisha wasanii kadhaa wa kimataifa akiwemo mkali wa Afrobeats kutokea Nigeria, Yemi Alade ambaye kipaji chake kiliibuliwa na shindano la uimbaji la Peak Talent Show 2009.