Ugomvi wa Mavokali na Kago kumbe ni kiki

Muktasari:

  • Kago ameiambia Mwananchi kama kuna mtu anataka kutumia msemo huo anatakiwa afuate utaratibu wa kumtafuta waongee vizuri ili wafanye biashara kwa sababu msemo huo ameusajili kisheria

Dar es Salaam. Mchekeshaji aliyejizolea umaarufu kutokana na msemo wake wa ‘Bado hujasema’ Theodoro Emmanuel maarufu kama Kago, ametoa angalizo kwa wenye mpango wa kutumia msemo wake bila kupata kibali maalumu kutoka kwake.

Kago ameiambia Mwananchi kama kuna mtu anataka kutumia msemo huo anatakiwa afuate utaratibu wa kumtafuta waongee vizuri ili wafanye biashara kwa sababu msemo huo ameusajili kisheria.

Hata hivyo, Kago hakuacha kufafanua ugomvi uliotokea mwezi mmoja uliopita kati yake na msanii wa Bongo Fleva, Mavokali baada ya msanii huyo kutumia msemo huo kwenye wimbo wake, unaoitwa ‘Hamjasema’

Staa huyo amesema yote yaliyotokea kati yake na Mavokali ilikuwa ni mpango wa kusukuma wimbo huo uweze kufanya vizuri.

“Watu walishindwa kuelewa lile sakata la Mavokali kuchukua msemo wangu ilikuwa ni staili ambayo iliandaliwa kwa ajili ya kuupeleka wimbo mbali ,” anasema Kago.
Chanzo cha msemo huo:

Kago anasema msemo huo aliupata akiwa 'location' na timu yake baada ya rafiki yake wa karibu kuongea na simu akimwambia aliyekuwa anaongea naye kuwa bado hajasema, ndipo alisikia akaona huo msemo anaweza kuutumia katika kazi zake.

“Msemo wa ‘bado hujasema’ ulipatikana pindi tulikuwa 'location' nilikuwa na rafiki yangu anaitwa Prosper Maulus alikuwa anaongea na simu akawa anamwambia aliyekuwa anaongea naye kuwa bado hujasema, ndiyo nikaona ina kitu nikaanza kuitumia,” anasema.

Ikumbukwe kuwa kupitia msemo huo Kago aliweza kupata madili mengi ikiwemo la kwenye tangazo la debi ya Simba na Yanga, iliyofanyika Novemba 5, 2023.