Ujue upande wa pili wa Navy Kenzo

Muktasari:

  • Nahreel anayeunda kundi la Navy Kenzo na mwenzake Aika, kupitia Academy hiyo wanachukua vijana wadogo wenye vipaji vya kusakata soka na kuwapatia mafunzo ikiwa ni sehemu nyingine ya biashara yao ukiachana na muziki

Dar es Salaam. Msanii na mtayarishaji muziki Bongo, Nahreel amesema Navy Kenzo Academy imelenga kukuza vipaji vya soka na kuviuza nje katika ligi za ushindani mkubwa lakini hiyo haifanyi kuacha kuwasaidia wasanii kupitia lebo yake ya muziki, The Industry.

Nahreel anayeunda kundi la Navy Kenzo na mwenzake Aika, kupitia Academy hiyo wanachukua vijana wadogo wenye vipaji vya kusakata soka na kuwapatia mafunzo ikiwa ni sehemu nyingine ya biashara yao ukiachana na muziki.

Kundi la Navy Kenzo lilianzishwa Aprili 2013 ingawa walikuwa pamoja kimuziki toka mwaka 2008, walipokuwa wanasoma India, walianza kufanya vizuri katika kundi la Pah One na baadaye kuondoka na kuanzisha Navy Kenzo.

Jina hilo limekutanisha maneno mawili toka nchi mbili tofauti, kwanza ni ‘Navy’ neno la Kiingereza lenye maana ya Jeshi, pili ni ‘Kenzo’ neno lenye asili ya Japan likiwa na maana ya Busara, Afya na Akili.

Kabla ya kufikia uwekezaji katika soka, Navy Kenzo walianza katika muziki kupitia lebo yao, The Industry ambapo mwaka 2016 waliwasaini wasanii watatu kwa mpingo ambao ni Seline, Wildad na Rosa Ree.

Ni wazi walikuwa wamejipanga na kudhamiria kwa sababu wasanii wote video zao za mwanzo zilifanyika Afrika Kusini, ila Oktoba 2017 Rose Ree alitangaza kuachana na The Industry, na wenzake pia waliondoka wakati huo.

Hata hivyo, hadi sasa Rosa Ree ni kipaji ambacho Navy Kenzo wanajivunia kukiibua, ameshatoa albamu moja, Goddest (2022) na hivi karibuni ameshinda tuzo kutoka The Orange Awards kama Msanii Bora wa Kike wa Hip Hip.

Msanii wa mwisho kusainiwa The Industry ni The Great Eddy ambaye alisaini Aprili 2021 na kutoa EP yake, Small Bad Wolf akiwa ni msanii wa kwanza wa lebo hiyo kufanya hivyo, pia alishiriki kwenye albamu ya Navy Kenzo, Story Of The African Mob.

Akizungumza na gazeti hili, Nahreel amesema anaangazia zaidi vipaji vya vijana wadogo kwa sababu ni rahisi kuvikuza na umri wao unatoa fursa kuja kuwa wachezaji wakubwa ndani na kimataifa baadaye.

“Lengo ni kuandaa wachezaji kuja kuwa ‘professional players’ kucheza nje ya nchi na ndani, ndiyo maana unakuta tunachukua vijana hadi chini ya umri wa miaka 17 ili niweza kuwapelekea sehemu maana umri wa miaka 17, 16 wanauzika kirahisi,” amesemea.

“Pia nipo na watoto wa miaka 13  hadi 17, muda   mwingine nina vijana wawili watatu wa miaka 19 siyo mbaya, lakini  13  hadi 17 ndiyo ninao wengi,” amesema Nahreel.

Utaratibu wa Navy Kenzo Academy kupata watoto wa kuwaingiza mafunzoni huwa na utaratibu wa mzazi kupiga simu na kuomba mtoto wake kuingizwa mafunzo hayo kwa kulipa kiasi fulani cha ada, ambapo utaratibu wa mazoezi hufanyika mara mbili kwa wiki muda wa jioni baada ya masomo.

Nahreel ambaye ni shabiki wa Yanga SC amesema ameamua kuwekeza katika Navy Kenzo Academy kwa sababu anajua masuala ya mpira kwani ameucheza kabla ya muziki uliompatia umaarufu mkubwa.  
“Siwezi kuacha kusaidia wanamuziki lakini mimi pia napenda mpira, kabla sijaingia kwenye mambo ya muziki nilikuwa nacheza mpira sana, kwa hiyo ni sehemu yangu nyingine ambayo ninaiweza vizuri, na ni biashara nyingine ambayo naitengeneza” amesemea.  

Mwaka juzi kupitia Academy hiyo walianzisha mashindano, Navy Kenzo Cup 2021 U15 ukiwa ni mwendelezo mara baada ya mwaka 2018 kupitia Navy Kenzo Foundation kuandaa mashindano mengine, Navy Kenzo Cup.

Akiwa kama Prodyuza Nahreel amefanikiwa kufanya kazi na wasanii kama Vanessa Mdee, Joh Makini, Diamond Platnumz, Mwana FA, Nikki wa Pili, AY, Izzo Biznes, Gnako, K.O, Roma n.k.

Mwaka 2010 wimbo kwanza aliotengeneza Nahreel ulishinda tuzo, ni wa Joh Makini, Stimu Zimelipiwa ulioshinda KTMA kama Wimbo Bora wa Hip Hop, na aliutengeneza wakati anasoma India, Punjab College alipochukua shahada ya Computer Science.

Nahreel ambaye alianza muziki mwaka 2003 akiwa kama Prodyuza alianza kufanya kazi studio ya Kama Kawa Records, Home Time Records, Switch Records kisha The Industry Studio ambayo wanaimiliki Navy Kenzo.

Hadi sasa Navy Kenzo wamefanikiwa kutoa albamu tatu AIM (Above Inna Minute) (2016), Story Of The African Mob (2020) na Most People Want This (2023), huku wakashinda tuzo za TMA, Soundcity MVP, EATV Awards, Hipipo, WatsUp Awards.