Unataka kuchora tattoo? Msikilize Boshen

Muktasari:
- Boshen ambaye alianza kazi ya uchoraji tattoo miaka kumi iliyopita, kipaji chake kilianza kuonekana tangu akiwa shule ya msingi kwa kuwachorea wanafunzi wenzake picha mbalimbali. Wakati akizungumza na gazeti hii amesema uhuni siyo muonekano, ni tabia ya mtu.
Dar es Salaam. Mtaani wapo wenye mitazamo ya kuwa tattoo ni uhuni, na wengine wakikazia kwamba mwanamke mwenye tattoo siyo wa kuoa na kumweka ndani, huku kwa upande wa wanaume wenye michoro hiyo mara nyingi huonekana wahuni na wababaishaji.
Mitazamo yote hii juu ya watu hao imekanushwa na mchora tattoo maarufu Tanzania , Bryson Peter maarufu kama Boshen, kwa kusema kuwa tattoo ni michoro kama mingine na ni sanaa ambayo haina uhusiano wowote na uhuni kama watu wanavyodhani.

Boshen ambaye alianza kazi ya uchoraji tattoo miaka kumi iliyopita, kipaji chake kilianza kuonekana tangu akiwa shule ya msingi kwa kuwachorea wanafunzi wenzake picha mbalimbali. Wakati akizungumza na gazeti hii amesema uhuni siyo muonekano, ni tabia ya mtu.
Boshen amesema ili mtu aweze kuwa mchoraji mzuri wa tattoo ni lazima awe na kipaji cha kuchora, pia katika utendaji ni lazima awe na vifaa vya kisasa. Huku akitaja kuwa hiyo ndiyo sababu kubwa ya watu wengi kumfuata awapatie huduma hiyo.
“Kuna watu wanatumia vifaa ambavyo siyo vya kisasa, sindano wanarudia, kuna wengine wanachemsha mimi kazi zangu huwa nafanya asilimia mia vifaa vipya, natumia natupa, kwa hiyo kama mchoraji unatakiwa uwe na uelewa wa hii kazi na uipende”. Amesema.

Boshen anasema vifaa vya kuchorea tattoo ni gharama na Tanzania havipatikani hivyo wakati wa kuviagiza huchukua muda kufika, kwa upande wake inamlazimu kuwa na akiba ya kutosha kwa kuwa amekuwa akipata kazi mpya kila mara.
Ametaja bei ya boksi la sindano za kuchorea tattoo ni Sh 100,000 ndani yake lina sindano 50, wino na vifaa vingine pia huviagiza nje ya nchi.
“Kuna wino wa aina nyingi, unaweza kununua, China unauzwa na kwenye mataifa tofauti tofauti lakini mimi nachukua vifaa vyangu vyote Marekani, maana naangalia ubora, kwa kuwa Marekani vinakuja vitu vyenye ubora mkubwa.”
Tattoo za kuziogopa
Kutokana na kuwepo kwa baadhi ya watu wanaopenda vitu vya bei rahisi amewataka kuwa makini na tattoo za bei hizo kwa sababu nyingi huwa na madhara.
“Tattoo mbaya ni zile za bei rahisi sana, zinakuwa na madhara unaweza ukachora ukakuta mkono umetutumka au pamoja na maumivu yote na bado mchoro ukafutika kutokana na vifaa kuwa vya bei rahisi ambavyo havikidhi vigezo.”
Tattoo kuhusishwa na magonjwa ya ngozi
Anaeleza kuwa anayechorwa tattoo na kupata magonjwa kama vile saratani hutokana na maeneo ambayo anakwenda kuchorwa kwani wapo baadhi ya wachoraji ambao hutumia vifaa ambavyo havijapitishwa kwa ajili ya ngozi.
Hivyo wanaotumia vitu tofauti ndiyo wanaweza kusababisha magonjwa huku akitaja baadhi ya vifaa visivyofaa kama wino wa ngisi.
“Vitu ambavyo havijathibitishwa ni hatari, vitu tunavyotumia sisi vimethibitishwa kwa hiyo kupata madhara siyo rahisi,” amesema.

Anayozingatia kabla ya kumchora mtu
Boshen amesema hatua anazofuata kabla ya kutoa huduma ya kumchora mtu, kwanza ni kuelewa kitu mteja anachotaka kuchora na kumshauri pia.
“Ni muhimu tushauriane unataka kuchora kitu hiki kwa nini? au mbona kitu hiki ni kikubwa, kwa sababu kuna watu wanawachora wapenzi wao, lazima nishauri ndiyo nianze kazi, sisi ni binadamu kuna kugombana, umeshamchora na tatoo haifutiki kirahisi, utafanyaje, lazima mambo yote hayo tujadiliane”. Ameeleza mchoraji huyo.
Asivyotakiwa kufanya mtu baada ya kuchora tattoo
Boshen anaeleza kuwa endapo mtu akichora tattoo anatakiwa asikae sana juani wala kuogelea kwa muda wa wiki tatu, kwa sababu tattoo ni kama kidonda hivyo huharibika.
Hata hivyo, zipo stori nyingi kuhusiana na maumivu anayopata mtu akiwa anachorwa Boshen ameeleza maumivu hayo huwa ya muda wa kuchorwa baada ya hapo kila kitu kinakuwa sawa .
“Tattoo ina maumivu huwezi kumdanganya mtu kuwa haiumi, maumivu yake yanaweza kuvumilika ukimaliza tu yanaondoka na siyo makali sana kama wengi wanavyosema, lakini kwa kuwa ni ishu inayogusa ngozi lakini iwe hivyo”. Amesema.
Changamoto anazokutana nazo
Anasema kwenye mahusiano yake mara nyingi mwanamke wake haamini kama kweli kazi zake huwa zinaenda salama, kutokana na baadhi ya wateja hasa wa kike kuchorwa maeneo nyeti ikiwemo kwenye makalio.
“Ninachopitia ni kwamba kwenye mahusiano yangu mara nyingi mwanamke wangu anakuwa haamini kama kweli nilimaliza kazi salama kutokana na mazingira ya kazi, hivyo changamoto ni kumuaminisha kuwa hakikutokea kitu kingine nje ya kazi, mimi najielewa na kitu ninachofanya kwa hiyo changamoto hazinisumbui.”Amesema

Utakumbuka kuwa Boshen alikuwa mume wa marehemu mwanamuziki Haitham, aliyefariki dunia Septemba 1, 2023 baada ya kupata matatizo kwenye mfumo wa upumuaji.
Boshen, ameeleza wateja wake wengi ni wanawake, hivyo kuna wakati anakutana na vishawishi kutoka kwao, huku akisimulia aliwahi kupigiwa simu na mteja kwa ajili ya kazi lakini alipofika akakutana na mambo tofauti.
“Nimewahi kupigiwa simu na mteja njoo sehemu fulani nahitaji tattoo nikafika hadi eneo la tukio nilipofika yule dada akaniambia hana shida ya tattoo shida yake ni mimi, kwanza alinikata nilichukia, mimi nimeenda, nimetoka nyumbani nimefika na vifaa nikajua naenda kuokota yeye ananiletea mapenzi, nilikasirika sana, hizo ni baadhi ya changamoto za kazi yangu.” Amesema
Mwitikio wa uchoraji tattoo kwa Tanzania
Amesema mwitikio kwa Tanzania kwenye uchoraji tattoo ni mkubwa kwa sababu wengi wanachora na wapo wanaotamani kuchora hasa wanawake.
Licha ya kuchora tattoo za aina nyingi anasema za maneno (majina na ujumbe), ndiyo zinachorwa sana kwa Tanzania.
Uraibu wa tattoo upo hivi..
Kuna simulizi kuwa tattoo ni kama ulevi mwingine mtu akianza moja, basi inakuwa ngumu kuacha badala yake huendelea kuongeza, siku hadi siku, Boshen amejibu hilo na kusema ni kweli.
“Ni kweli tattoo ina uraibu, lakini ikiwa mbaya mtu anaweza asiwe ‘adiktedi’, ila ikiwa nzuri ndiyo uraibu unavyoanza kwamba kila mtu akiona atakwambia kuwa tattoo yako ni nzuri na ikiwa hivyo lazima mtu ataongeza na ukiongeza moja, utaongeza na ya pili.” Amesema Boshen.
Ametaja bei ya tattoo, amesema ndogo anachora kwa laki moja, lakini tattoo ambayo amewahi kuchora kwa bei kubwa kuliko zote ni ile ya milioni tano ambayo alimchora Prophet Passion Java kutoka Zimbabwe.
Tattoo siyo kitu cha kukurupuka
Boshen anasema uchoraji wa tattoo siyo kitu cha kukurupuka ni kitu cha kukaa na kufikiria, kuwa itakuwa na madhara na faida gani siyo kuchora kwa sababu ya mihemko na mikumbo.
“Alikuja mtu na hela yake kwa macho yangu nikaona ni mdogo sana nikamwambia siwezi kufanya hiyo kazi, alienda akachorwa sehemu nyingine nikapokea simu kwa baba yake alidhani nimemchora mwanaye. Iilikuwa tatizo nililiona lakini kuna mtu akaangalia hela akamchora”. Amesema
Boshen anasema maadili ni kitu cha kuangaliwa kwa wachoraji tattoo siyo kuchora watoto wadogo ambao hawajafikisha miaka kumi na nane kwa sababu ni kumuharibia malengo.
Kati ya wasanii waliowahi kuchorwa tattoo na Boshen ni Harmonize, Kajala, Clatous Chama, Young Dee, Adam Mchomvu, Dulla Makabila, Barnaba, Oxlade na wengine wengi.
Licha ya hayo daktari bingwa wa ngozi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mike
Mboneko, anasema uchoraji wa tattoo huchangia kwa kiasi kikubwa maambukizi ya homa ya ini kutokana na baadhi ya wachora tattoo kutozingatia usalama wa afya za wateja.
Mbali na ugonjwa huo, pia hupata maambukizi ya ngozi kwa haraka kutokana na sehemu iliyochorwa tattoo kuwa wazi kurahisisha bakteria kupenya na kuleta madhara.
“Miongoni mwa kesi za kansa ambazo hutokana na uchoraji tattoo ilikuwa ni moja kwa mtu mwenye ulemavu wa ngozi. Kwa sasa kumekuwa na wimbi la wachora tattoo mitaani, hali inayohatarisha usalama wa afya za wachorwaji, hivyo nashauri wachora tattoo kuzingatia taratibu za kiafya ili kuzuia maambukizi ya homa ya ini na HIV,” anasema Dk Mboneko.