Tamu na chungu ya michoro ya Tattoo

Napenda tattoo kwa sababu ni njia inayonifanya nijisikie vizuri, hasa ninapopitia changamoto zinazoniumiza moyo na kunikosesha amani, nikishachora huwa napata amani, na michoro yote iliyopo mwilini mwangu ina maana.

“Hakuna aliyewahi kunishinikiza au kunifanya niweke mchoro wowote mwilini mwangu na tattoo yangu ya kwanza nilichora nikiwa na miaka 16, ni mimi mwenyewe niliamua siku hiyo nachora na nikachora.”

Hayo ni maneno ya Zourha Malisa, mmoja wa wanawake wanaovutiwa na michoro mwilini maarufu kama tattoo, akieleza kuwa hakuna uhusiano wowote wa uhuni na mtu anayechora michoro hiyo.

Anaeleza kuwa mara zote amekuwa akitumia tattoo kama njia ya kuzungumza na moyo wake na huwa zinampa nguvu ya kupambana na changamoto anazopitia kwa sababu siku zote zinamkumbusha kuwa yeye ni imara.

“Nina tattoo sita mwilini na kila moja ina maana kwangu, nakumbuka mchoro wangu wa kwanza mwilini niliuchora nikiwa na miaka 16 baada ya kufeli kidato cha nne, nilipitia kipindi kigumu katika familia, sikuwa nafahamu nifanye nini, lakini siku moja nikiwa naangalia filamu nikamuona ndege tai.

“Nilivutiwa na uwezo wa yule ndege namna anavyoweza kuruka juu zaidi, ikanijia taswira kwamba hata mimi naweza kupambana kufika juu licha ya ugumu ninaopitia, nikachora tattoo ya yule ndege na nilipambana kuishi misingi ya huyo ndege, kwa kifupi alinipa hamasa,” anasema Zourha.

Pamoja na imani aliyonayo kwenye tattoo, mwanadada huyu si muumini wa kumshauri mtu kuchora bila kuwa na sababu ya msingi kwa sababu anaamini ni alama ambayo haiondoki kwa urahisim, mwilini.

“Binafsi huwa siamini kama tattoo ni urembo na ndiyo maana siwezi kumshawishi mtu yeyote achore, kwangu ni kitu chenye maana kubwa, huwezi kuweka mchoro mwilini kama huna sababu ya kufanya hivyo. Siwashauri watu kukurupuka kuchora kwa msukumo wa kitu au uhusiano halafu baadaye ufikie kuichukia au kutamani kuiondoa.”

Wakati Zourha akieleza hayo, mambo ni tofauti kwa Shani Mikidadi, yeye anaamini mchoro aliochora mkononi mwake miaka kadhaa iliyopita ni chanzo cha maisha yake kuwa magumu.

Shani anaeleza kwamba licha ya elimu ngazi ya digrii aliyonayo, anajikuta akikosa kazi kwa sababu ya mchoro huo unaoonekana na kuwapa taswira tofauti waajiri.

Shani anasema licha ya mama yake kumzuia kuchora mchoro huo, alipingana na kauli ya mama yake na hatimaye akaichora.

“Nimesoma, nina shahada ya biashara, nimekuwa nikitafuta kazi na ninapata bahati ya kuitwa kwenye usaili lakini nafahamu fika, nakosa kazi kwa sababu ya tattoo niliyonayo mkononi, inanifanya nionekane mhuni, ni miongoni mwa vitu ninavyojutia kuvifanya kwenye maisha yangu.”

Majuto haya hayapo kwa Shani pekee, Sauda Juma (50) anajutia michoro aliyoichora mwilini mwake akiwa na miaka 18, anakiri kuwa imechangia kwa kiasi kikubwa kumpotezea fursa nyingi kwa vile alionekana mhuni.

“Wakati nachora akili yangu ilikuwa imetawaliwa na utoto, maana nakumbuka dada yangu alinizuia ila sikutaka kumsikiliza, nikachora nyoka aina ya kobra kifuani na kwenye paja.

Kadiri miaka ilivyozidi kwenda ndiyo nikaanza kujutia, kuna wakati nilipata mwanamume akanitamkia wazi kwamba natamani kukuoa lakini hiyo michoro itanipa shida kwenye familia yangu. Kiukweli kile kitu kiliniumiza nikajikuta najutia uamuzi wangu,” anasema Sauda.

Hilo lilimfanya kufikiria kuiondoa michoro hiyo mwilini, ndipo alipokutana na ushauri kuwa utomvu wa korosho unaweza kutumika kuifuta, alijaribu njia hiyo lakini hakupata matokeo mazuri zaidi ya jeraha kubwa zaidi.

“Niliweka korosho baada ya kuambiwa utomvu wake unafuta, mambo hayakuwa kama nilivyotarajia niliishia kupata maumivu na ule utomvu ulinisababishia kidonda kikubwa na mchoro ukabaki kama ulivyo.”


Asemavyo mchora tattoo

Akizungumza na Mwananchi, mchora tattoo mkongwe, Yusufu Masasi almaarufu ‘Yuzo’, anasema historia ya tattoo ilianza miaka ya 1860 huko barani Asia, kipindi ambacho mabepari walichora na kutunza kumbukumbu zao za siri katika miili.

Utamaduni huu ukasambaa katika mabara mbalimbali, ikiwemo Afrika ambako vijana wengi wameingia kwenye uchoraji wa michoro hiyo.

Mchora tattoo huyu anaeleza kuwa katika miaka ya karibuni, kumekuwa na wimbi kubwa la wanawake kuchora tatoo kuliko wanaume, huku wengi wao wakichora kwenye sehemu ya mwili ambayo huonekana kwa urahisi.

“Ninachoona wanawake wengi wanachora kwa ajili ya urembo wakitaka kuonyesha, ndiyo maana michoro yao mara nyingi huwa sehemu zinazoonekana kama shingoni, mapajani na kiunoni.

“Licha ya kuwa hii ndiyo kazi yangu, lakini nitumie fursa hii kuwashauri vijana kama wanataka kuchora wazingatie mfumo wa maisha ili kuzuia kujutia baada ya kuchora tatoo kwa sababu maisha yanabadilika kila uchwao. Kama huna uhakika na unachokifanya, tafuta ushauri kabla ya kuchora tatoo ili usije kujutia baadaye,”

Kuhusiana na hali ya watu kufuta tattoo, Yuzzo anasema anapata pia watu wengi wanaotaka kufuta michoro, hasa wanawake.

“Wengi wanaokuja kufuta ni wanawake na sababu ni kwamba walifanya machaguo sio sahihi, wamekutana na michoro mingine, hivyo wanataka kubadilisha, sababu ya pili ni wale walioandika majina ya wapenzi wao sasa mapenzi yanapoisha wanakuja kufuta.

Hata hivyo, mtaalamu huyu anatahadharisha kuwa kufuta tatoo kuna madhara makubwa kuliko kuchora, kwa sababu wakati wa kufuta hutumika mionzi mikali.

Mionzi huunguza sehemu ya tatoo na kutengeneza lengelenge linalotoa maji na wino hivyo kuacha jeraha linalobakia kama kovu. Kuna baadhi ya tatoo hazifutiki mara moja, bali hufutwa kwa zaidi ya mara tatu ndiyo iishe.


Madhara ya kiafya yanayoweza kujitokeza

Daktari bingwa wa ngozi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mike Mboneko anasema uchoraji wa tattoo huchangia kwa kiasi kikubwa maambukizo ya homa ya ini kutokana na baadhi ya wachora tattoo kutozingatia usalama wa afya za wateja.

Mbali na ugonjwa huo, pia hupata maambukizo ya ngozi kwa haraka kutokana na sehemu ya iliyochorwa tattoo kuwa wazi kurahisisha bakteria kupenya na kuleta madhara.

“Miongoni mwa kesi za kansa ambazo hutokana na uchoraji tattoo ilikuwa ni moja kwa mtu mwenye ulemavu wa ngozi. Kwa sasa kumekuwa na wimbi la wachora tattoo mitaani, hali inayohatarisha usalama wa afya za wachorwaji, hivyo anashauri wachora tattoo kuzingatia taratibu za kiafya ili kuzuia maambukizo ya homa ya ini na HIV,” anasema Dk Mboneko.


Kimaadili ya utumishi wa umma ikoje

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Rainer Budodi anasema mtumishi wa umma haruhusiwi kuwa na tattoo inayoonekana.

Kwa mujibu wa kanuni za maadili na utendaji kazi kwa mtumishi wa umma na waraka namba 6 wa utumishi wa umma wa mwaka 2020 umeeleza kwa uwazi kuhusu unadhifu.

“Katika suala la unadhifu imeelekezwa kwenye kipengele (b), ina sehemu yenye makatazo ambayo hatakiwi kuwa navyo mtumishi wa umma, ikiwemo tattoo na michoro mingine ya kudumu katika sehemu za mwili ambazo zinaonekana,” anasema Bulilo.


Mitazamo ya wanajamii

Licha ya mtindo huu kupendwa na vijana wengi kwenye jamii, kumekuwapo na mitazamo hasi kuhusu kuweka michoro mwilini na kuhusisha na kulegalega kwenye malezi.

Euphrasia Mambwe anasema siku hizi wazazi wamejisahau, hasa katika suala zima la malezi, wakishindwa kuzungumza na watoto wao, matokeo yake wanaangukia katika kufanya mambo yasiyofaa kwa kufuata mkumbo.

"Ni vyema tukawaasa vijana wetu ulimwengu waliopo wao, sio tuliokuwa sisi wa kina Bi Kidude na Siti binti Saad, sasa hivi ulimwengu wa utandawazi sio kila kitu cha kuiga, vijana ndio wazazi wa kesho, hatuwezi kuwaamulia nini wafanye, hasa katika utu uzima.

“Malezi yetu ndiyo yatawaongoza nini wafanye, kwa wakati gani na nini matarajio ya baadaye.

“Tatoo siyo mbaya, ila ubaya unaletwa na misingi yetu ya utamaduni na mfumo wa maisha kwa ujumla. Pia wanaochora tattoo wawe tayari kihisia ili wasijutie baadaye baada ya kufanya hivyo,” anasema Euphrasia.

Kwa upande wake Kelvin Ayoub anasema tattoo ni uhuni na unamfanya anayechorwa kupoteza sifa za kupata baadhi ya fursa, ikiwemo ajira za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Sijui kwa nini vijana hawajifunzi, Ronaldo hana tattoo sehemu yoyote mwilini, ni kutokana na baadhi ya kampuni anazofanya nazo biashara kuwa na masharti ya kutokubaliana na uchoraji wa tattoo. Hata hapa nchini Tanzania kazi za Serikali haziruhusu mtu awe na tattoo, labda kwa kificho, mfano jeshini hachukuliwi mtu aliyechora tattoo,” anasema Kelvin.

Naye Andrew Lyaunga anasema ifikie hatua watu waone tattoo ni urembo, wanaochora wasibaguliwe na wanaofikiria kuchora waachwe waamue wenyewe kutoka katika nafsi zao na sio kushawishiwa.