Usiyoyajua kuhusu A.K.A za wasanii
Muktasari:
- Si ajabu kukuta msela mfukoni hana hata mia lakini kichwani ana matumaini ya kuwa Diamond. Mwonekano wao sasa vyeni shingoni, mitindo ya nywele, hereini masikioni pamba kali na mikogo mingine, bila kusahau wakati wa kujitambulisha. Utasikia naitwa Fidodido A.K.A Fido.
Dar es Salaam. Siku hizi karibia kila nyumba ina msanii. Kama siyo wa kuimba basi atakwambia anajua kuigiza. Kama ilivyo mtaani kwenu na kwetu ni hivyo hivyo, kwa wachache wanao jipambania kutoboa kwenye tasnia hizo huwa na swaga mbalimbali za kistaa.
Si ajabu kukuta msela mfukoni hana hata mia lakini kichwani ana matumaini ya kuwa Diamond. Mwonekano wao sasa vyeni shingoni, mitindo ya nywele, hereini masikioni pamba kali na mikogo mingine, bila kusahau wakati wa kujitambulisha. Utasikia naitwa Fidodido A.K.A Fido.
Ni nadra sana kukuta wanatumia majina yao kamili lazima kuwe na A.K.A ya kuwapeleka mjini. Na kweli kwa baadhi yao majina hayo ya A.K.A huwabadilishia maisha. Swali ni je wanafahamu chimbuko na maana ya A.KA? Fahamu zaidi.
A.K.A ni kifupi cha maneno ya Kiingereza “Also Known As”, ambayo tafsiri yake ya Kiswahili ni “Anayejulikana pia kama” au “Maarufu pia kwa jina la.
Awali A.K.A ilianza kutumika katika maandishi ya kisheria nchini Marekani na Uingereza karne ya 20, hasa katika kesi ambapo mtu alihusishwa na majina tofauti. Katika rekodi za kisheria A.K.A ilikuwa muhimu sana kwa kutambua wahalifu waliokuwa wakitumia majina bandia ili kuficha utambulisho wao halisi.
Hivyo, kifupi hiki kilikuwa na umuhimu katika kumbukumbu za kisheria, uchunguzi wa uhalifu, na ufuatiliaji wa wahusika mbalimbali.
Hata hivyo kadri muda na mabadiliko katika jamii yalivyoendelea kutokea, A.K.A ilianza kupenya katika sanaa kwa kuanzia kwenye muziki wa Hip-Hop wasanii wengi wakaanza kutumia na hadi sasa imesambaa kwa watu mbalimbali.
Mastaa na A.K.A zao
Nandy - The African Princess
Ukitazama video mbili za nyimbo za mwanzo zake Nandy, Nagusagusa (2016) na Wasikudanganye (2016), utabaini kwanini aliamua kujipa a.k.a ya The African Princess kwani katika video hizo amevalia mavazi ya kiafrika hasa vitenge.
Jina hilo liliendelea likibeba jina la albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018), kisha likaja kutumika katika lebo yake, The African Princess Label huku pia akilitumia katika mitandao ya Instagram na YouTube.
AY - Mzee wa Commercial
Tangu akiwa kundi la S.O.G. na East Coast Team, AY amekuwa akibadili ladha ya muziki wake kwa lengo la kufika mbali kama kimataifa na huko ndipo ikazaliwa a.k.a ya Mzee wa Commercial.
Hata hivyo, a.k.a hakuibuni yeye, bali P-Funk Majani ndiye aliyempa jina hilo baada ya kuona AY anamudu aina mbalimbali za muziki kuanzia rap hadi reggae, kitu ambacho pia kimepa fursa nyingi kiuchumi.
Mimi Mars - Chugga Queen
Katika nyimbo zake nyingi anajitambulisha kama Chugga Queen, a.k.a ni kwa lengo la kumtambulisha yeye anatokea wapi na heshima yake ipo vipi huko kwao ambapo ni Arusha.
Ikumbukwe Mimi Mars aliingia kwenye muziki baada ya kusainiwa Mdee Music, rekodi lebo inayomilikiwa na dada yake Vanessa Mdee ambaye a.k.a yake ni Vee Money, mwanamuziki aliyetoa albamu moja, Money Mondays (2018).
Mbosso - Khan
Kwa mujibu wa Mbosso, yeye anapenda sana kusikiliza nyimbo za Kihindi na ndio sababu baadhi ya nyimbo zake kuwa na mahadhi hayo na ndio sababu ya kujipa a.k.a ya Khan, jina lenye asili ya India.
Alichofanya Mbosso hakina tofauti sana na kile cha Nandy, kwani naye Mbosso hajaishia kuitumia Khan kama a.k.a pekee, bali ameshatoa Extended Playlis (EP) iitwayo Khan (2022), huku akifungua lebo, Khan Music.
P-Funk - Majani
Mwanzoni mwa miaka 1990 alitumia jina la DJ Skills of Pain wakati huo akicheza tu muziki na kuimba pamoja na kurap, ila alipoanza utayarishaji muziki likazaliwa jina la P-Funk ambalo kwa sehemu limetoholewa kutoka katika jina lake la Paul.
Katikati ya umaarufu wa kazi yake, akaipata a.k.a ya Majani kutoka kwa wasanii waliokuwa wanarekodi Bongo Records. Kwa mujibu wa P-Funk, jina la Majani lilikuja kutokana na kupendelea kula mboga za majani mara kwa mara.
Nikki Mbishi - Dr. Unju
Pengine Nikki Mbishi aliyevuma na ngoma yake, Play Boy (2011), ndiye rapa wa kizazi hiki aliyejipachika a.k.a nyingi zaidi, miongoni mwa hizo ni Baba Malcom, Babu Bomba, Dr. Unju, Zohan, Juke Box, Otingo Taniboy, Sam Magoli, Telabyte n.k.
Katika hizo, a.k.a Unju ndio amekuwa akiitumia sana katika nyimbo zake na hata kwenye baadhi ya kurasa zake za mitandao ya kijamiii.
TID - Mnyama
Tangu ameanza muziki na kundi la Black Gangsters mwaka 1997, TID amekuwa na a.k.a nyingi kama Mzee Kigogo, Warioba na Mnyama ambayo baadhi ya wasanii wenzake akiwamo Stamina wamewahi kuikosoa kupitia nyimbo zao.
Jina la Mnyama alipewa nchini Kenya ikiwa ni kipindi kifupi tangu atoke jela hapo mwaka 2008. Jina hilo lilikuja kutokana na mtindo wake wa maisha akiwa kama mwanamuziki mwenye kipaji, mcheshi na mtukutu pia.
A.K.A za Wanyama
Wakati TID akijiita Mnyama, kuna wasanii wengi Bongo ambao wameamua kujipa majina ya wanyama hasa wa mwituni ili kuonyesha ni kiasi gani ni wakali kimuziki au jinsi chapa zao zilivyo za kutisha na za kipekee mbele ya wakali wengi.
Wasanii na a.k.a zao za wanyama ni Harmonize (Tembo), Mr. Blue (Nyani Mzee), Diamond Platnumz (Simba), Rayvanny (Chui), Young Lunya (Mbuzi), Country Boy (Fisi), Dudu Baya (Mamba), Afande Sele (Simba Dume), Fid Q (Mzee Mbuzi) n.k.
Mwasiti - Kipepeo Mweusi (The Black Butterfly)
Staa huyu aliyetoka na kibao chake, Niambie (2006) chini ya Tanzania House of Talent (THT), alijipa a.k.a Kipepeo Mweusi (The Black Butterfly) kama njia ya kujivunia rangi yake,
Ikumbukwe Mwasiti, mwanamuziki wa kwanza wa kike kutajwa kuwania vipengele vitano katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), pia EP yake ya kwanza iliyotoka mwaka 2021 ipewa jina la The Black Butterfly.
Dully Sykes - Mr. Misifa
Jina la Misifa, Dully Sykes alipewa na mama yake maana alipokuwa mdogo alikuwa kiherehere sana, mathalani anaweza kununuliwa nguzo za sikukuu ila akazivaa kabla ya hata ya sikukuu yenyewe na kwenda kuwaringia wenzake.
Hata hivyo, waliokuja kulileta jina hilo katika muziki ni Zig Zag Crew baada ya kwenda nyumbani kwa kina Dully na kumsikia mama yake akimuita Misifa, ndipo nao wakaanza kumuita hivyo, basi Dully akaona isiwe tabu bora ajiite tu Mr. Misifa.
Kuna Hawa Pia
Lady Jaydee (Komando Jide), Marioo (Toto Bad), Anjella (The Black Queen), Billnass (Nenga), G Nako (Warawara), Linah (Ndege Mnana), Joh Makini (Mwamba wa Kaskazini), Navy Kenzo (Mob), Professor Jay (Wamitulinga) na S2kizzy (Zombie).
Wengine ni Chege (Top Shatta), Alikiba (King Kiba), Lulu Diva (Sexy Diva), Juma Nature (Kiroboto), Young Killer (Msodoki), Witness (Kibonge Mwepesi), Chid Benzi (Chuma), One The Incredible (Uno), Inspector Haroun (Babu), Jux (African Boy) n.k.
Maoni ya wadau
Akizungumzia umuhimu na vitu vya kuzingatia kabla ya kutafuta A.K.A Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Dk Herbert Makoye anasema A.K.A ni kama jina la biashara hivyo ni vyema msanii akatafuta la kuvutia.
“Unatafuta jina ambalo litavuta biashara yako. Hakikisha una jina ambalo linaweza kutamkika kwa haraka. Ndiyo maana wasanii wengine hata majina yao tunakuwa hatuyajui.
“AKA lazima iwe na mvuto kwa audience itamkike na kukumbukwa kwa urahisi. Iwe haimkosei mtu yoyote kwa sababu yapo majina ambayo ni matusi kwa jamii fulani msanii achague jina ambalo halitaleta mfadhaiko kwa kundi lolote,” anasema.
Hata hivyo kwa upande wake msanii wa muziki wa Hip-Hop P Mawenge anasema majina ya kisanii yamekuwa msaada mkubwa kwao kwani yanafanya kazi zao za kisanaa ziwe nyepesi.
“Sisi tunafanya biashara ya muziki ambao inazingatia sana ubunifu kupitia majina haya ya A.K.A imekuwa rahisi sana kwetu kuuza na kujitofautisha katika jamii.
“Hata mbali na muziki kupitia biashara zetu nyingine ambazo tumekuwa tukizifanya ukweli kabisa zimekuwa zikifanya vizuri kutokana na umaarufu wa majina yetu ambayo ni ya A.K.A,” anasema.
Naye msanii Dully Sykes anasema msanii ni lazima ajitofautishe na watu wengine kwa sababu amebeba sanaa.
“Ukisema msanii maana yake sanaa yote ipo mikononi mwako kwa hiyo ni jukumu lako pia kuhakikisha kila unachofanya kinavutia mashabiki kuanzia mwonekano wa mavazi hadi jina.
“A.K.A kwetu si majina tu bali ni sehemu ya kujikuza na kujitangaza kibiashara ndiyo maana wapo baadhi ya watu wanayalinda majina yao kwa udi na uvumba kwa sababu A.K.A hiyo imeshageuka kuwa pesa kwa hiyo ni kuzingatia tu ubunifu na misingi katika kutafuta A.K.A,” amesema Mr Misifa.