Veta yaandaa mitaala ya sanaa
Muktasari:
- Akizungumza wakati wakiingia makubaliano ya ushirikiano na taasisi inayojishughulisha na vipaji vya sanaa, Tanzania House of Talent (THT), Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Anthony Kasore amesema mamlaka hiyo imetengeneza mitaala inayohusika na sekta ya sanaa, hivyo kuongeza idadi ya mitaala ya sekta 12 hadi 13.
Dodoma. Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, (Veta) imeandaa mitaala ya mafunzo kwenye sanaa ikiwemo uandaaji wa muziki na filamu, lengo likiwa ni kurasimisha ubunifu na vipaji kwa vijana walioingia katika sekta hiyo.
Akizungumza wakati wakiingia makubaliano ya ushirikiano na taasisi inayojishughulisha na vipaji vya sanaa, Tanzania House of Talent (THT), Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Anthony Kasore amesema mamlaka hiyo imetengeneza mitaala inayohusika na sekta ya sanaa, hivyo kuongeza idadi ya mitaala ya sekta 12 hadi 13.
Amesema kabla ya kutengeneza mitaala katika sekta hiyo walifanya utafiti wa soko la ajira ambapo ilibainika kuwa watendaji wengi wanafanya kazi zao kwa kutumia vipaji, ubunifu na ujuzi ambao wamepata.
“Katika kuweka vyema tukaona ni vizuri ujuzi huu utambulike na tukaandaa hiyo sekta, tumeenda kutizama vitu vyote vinavyohusika na hiyo sekta. Katika kuitazama tunakuja na mitaala,” amesema Kasore.
Ametaja mitaala hiyo ni film production (uandaaji wa filamu), art and design (uchoraji na ubunifu), Event planning and managements (kuandaa matukio na kuyasimamia), music production (uandaaji wa muziki).
“Tutazidi kuja na mitaala mingine ambayo itawezesha vijana na wananchi kuingia katika hii sekta na kutambulika na kufanya kazi mbalimbali ambazo zitawezesha kuingiza kipato chao pamoja ili kuwa ajira za staha,” amefafanua Kasore.
Amebainisha kwamba katika kufanikisha hilo waliona haja ya kushirikiana na taasisi inayojishughulisha na vipaji vya sanaa, Tanzania House of Talent (THT) kutokana na kuwa na watu ambao wamekuwa wakitengeneza na kuboresha ujuzi wao.
Mkurugenzi Mkuu wa THT, Kemilembe Mutahaba amesema wameingia katika ushirikiano huo ili taasisi yake iweze kutumia mitaala iliyotengenezwa na Veta na kuwafanya vijana watakapomaliza masomo wapate vyeti vinavyotambulika.
“Mara nyingi THT imekuwa ikiwapa mafunzo vijana lakini tunakuwa hatuna vyeti tunavyoweza kutoa ambavyo ni vya Serikali, tunashukuru kwa hilo. Tumekaa na vijana kwa muda mrefu ambapo kuna masomo Veta wanafundisha ambayo pia vijana wanaweza kuyasoma,” amesema Mutahaba.
Naye Mkurugenzi wa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi Veta, Dk Abdalla Ngodi amesema kabla ya kuandaa mitaala wanatafuta taarifa za soko la ajira lengo likiwa ni kubaini ujuzi unaohitajika viwandani (soko la ajira).
Amesema katika eneo la sanaa walianza kufanya utafiti mwaka 2022/2023 na kubaini vijana wanaofanya ni wengi lakini halijarasimishwa kupata vyeti vya elimu ya wanachokifanya.
“Hili ni eneo linaloheshimika lakini halitambuliki kama taaluma nyingine, baada ya kupata taarifa hizo tuliita wataalam mbalimbali vyuo vikuu, VETA kwenye watu wanaotambulika na sekta ya sanaa tukakaa tukafanya uchambuzi wa mahitaji yanayotakiwa kabla ya kutengeneza mitaala,” amesema Ngodi.
Dk Ngodi amesema maboresho ya mitaala ya elimu inayozingatia ujuzi ikiwemo eneo hilo la sanaa itaanza Januari 2025 mara baada ya kupata ithibati kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi (NACTVET).
Amesema walengwa ni wale waliomaliza darasa la saba ambao hawajaingia katika mfumo rasmi wa elimu, sekondari hadi chuo.
“Sisi tuna utaratibu wa kutambua ujuzi uliopatikana katika mazingira yasiyo rasmi, unaweza kwenda kwenye gereji ukakuta fundi mahiri kabisa lakini hajapita katika mfumo rasmi. Sisi huwa tunafanya utaratibu wa kutambua ujuzi alionao na kubaini mapungufu aliyonayo,” amesema.
Wenyewe wafurahia
Muandaaji wa filamu, Leah Richard Mwendamseka maarufu Lamata amesema kuanzishwa kwa mafunzo hayo kutasaidia kukuza na kuongeza ufanisi katika sekta hiyo ya sanaa.
“Walikuja hapa (Veta) kutuhoji kabla ya kuanzisha kozi hiyo, hili ni zuri. Itasaidia katika kukuza industry (sekta),” amesema Lamata.
Naye Neema Ndepanya ambaye ni muongozaji filamu, amesema ni kitu kizuri kwa sababu watu wengi wanafanya bila kuwa na ujuzi wa kitaaluma, hivyo itasaidia kukuza tasnia hiyo.
“Wengi wetu wanafanya kwa kuwa wana kipaji cha kufanya hivyo, kuja kwa haya mafunzo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza hii tasnia,” amesema Ndepanya.