Waandishi wa nyimbo wapewa mbinu

Muktasari:
- Kutokana na hayo wapo baadhi ya waandishi ambao wamekuwa wakiwatupia lawama wasanii kwa kutowataja ama kutoweka wazi kuwa wimbo husika uliandikwa na mtu fulani.
Dar es Salaam, Imekuwa kawaida kuona wasanii wakipewa maua yao pindi ngoma zao zikifanya vizuri, lakini sifa wanazopewa wasanii hao ni tofauti na wanazopata waandishi wa nyimbo.
Kutokana na hayo wapo baadhi ya waandishi ambao wamekuwa wakiwatupia lawama wasanii kwa kutowataja ama kutoweka wazi kuwa wimbo husika uliandikwa na mtu fulani.
Akizungumza na Mwananchi, mwanamuziki na mwandishi wa nyimbo, Soggy Doggy Anter ambaye sasa hivi amejikita katika masuala ya utangazaji amesema waandishi wa nyimbo wameweka mbele sifa kuliko kazi.
“Ninachokiona kwamba ni ufahamu tu kwa sababu muziki wetu haujawa rasmi tumekuwa tukifanya vitu kwa sifa hasa sisi waandishi yaani mfano leo hii msanii ambaye hajatoka halafu akambiwa na Diamond amuandikie ngoma yeye hatowaza kama ninayemwandikia ni msanii mkubwa na ana pesa yeye ataona ujiko kwamba amemwandika nyimbo msanii mkubwa halafu anasubiri wimbo ukisha-hit unakuta mwandishi anajitokeza,” amesema Soggy.
Aidha amewataka waandishi wa nyimbo wajiongeze ambapo amesema kabla ya kumuandikia mtu nyimbo kuwe na mkataba.
“Kwahiyo wasanii wanaoandika nyimbo wajiongeze, kabla ya kumuandika wimbo kuwe na mkataba waandikishiane, niliwahi kusikia baadhi ya wasanii wakidai kuwa hawatowaandikia tena wanamuziki nyimbo, sasa kama Mungu kakupa karama ya kuandika kwa nini usiandike ila hakikisha unapoandika malipo yawepo kwa maandishi ili kuepuka kulalamika au kulia,” amesema.
Hata hivyo kwa upande wa mwanamuziki Kayumba Juma ameeleza kuwa wasanii wanatakiwa wakumbuke wanaowaandikia huku akidai kuna muda waandishi wanatakiwa waandike nyimbo kama zawadi.
“Mimi huwa nawaandikia wasanii lakini nawapa kama zawadi tu, sasa ni yeye muimbaji kunipa umiliki au laa halafu kitu kingine ambacho kinaficha hawa waandishi siku hizi wasanii wameendelea walio wengi wanavipawa vya kuandika tungo zao wenyewe,” amesema.
Mbali na hayo, kwa upande wa Hamadai kutoka kundi la The Mafiki amesema waandishi wa sasa ni wanamuziki wachanga wanaojitafuta.
“Siku hizi waandishi wanaowaandikia nyimbo wasanii ni wanamuziki wachanga ambao wanajitafuta kupitia kumuandika msanii mkubwa ndiyo maana kumekuwa na malalamiko ila ki-fair kabisa mtu unatakiwa utoe heshima kwa aliyekuandikia, huenda yeye alifaya bure hata kama hajapata pesa kwako basi apate kwa watu wengine,” amesema Hamadai.
Utakumbuka wasanii kama Marioo, Kontawa, Jay Melody siku za nyuma waliwahi kusema hawatowaandikia tena nyimbo wasanii wengine.
Licha ya hayo yote inaelezwa kuwa wakati mwingine msanii huwa na makubaliano ya kimkataba na mwandishi kutotaja jina baada ya kulipwa pesa.