Waigizaji msiigize namna ya kuishi

Muktasari:

  • Lakini kabla ya kuanza somo hili, waulize watu ishirini swali moja: “maisha ni nini?” Kila mmoja atakujibu kivyake; “Maisha ni mapambano”, “Maisha ni kitendawili” “Maisha ni safari”... Hao ni watatu, kumi na saba waliobaki nao wana majibu yao.Vuta picha kuwa umepata matrilioni ya shilingi kupitia bahati nasibu ya dunia.

Maisha si mazoezi wala majaribio. Ni jukumu kamili ulilolipokea na unaloendelea nalo. Hadithi ya “Naenda kutafuta maisha” sio ya kweli kwa sababu babu yako uliyemwacha kijijini naye anaishi, na Mungu bariki ataishi zaidi ya wewe unayeendelea kuyatafuta. 

Lakini kabla ya kuanza somo hili, waulize watu ishirini swali moja: “maisha ni nini?” Kila mmoja atakujibu kivyake; “Maisha ni mapambano”, “Maisha ni kitendawili” “Maisha ni safari”... Hao ni watatu, kumi na saba waliobaki nao wana majibu yao.Vuta picha kuwa umepata matrilioni ya shilingi kupitia bahati nasibu ya dunia.

Mawakala wakakutengenezea maisha kama ya bilionea wa Ulaya. Kila wiki helikopta inakutembeza kandokando ya Milima ya Everest, Victoria Falls, Ngorongoro Crater, Taj Mahal na kwenye piramidi la Giza kule Misri kwa ajili ya kufaidi maisha, pia kujisahaulisha ‘machungu’ uliyoyapitia kabla hujakamata bingo.

Ziara hizo ziambatane na menyu na malazi katika hoteli za Wellington na migahawa ya MacDonald’s. Tiketi za misimu ya michuano ya Mabingwa wa Ulaya na Italia na fainali za NBA. 

Pia mara mojamoja si mbaya ukapelekwa kucheka na mastaa wa Hollywood. Utaopoa wenza wa kutosha wenye hadhi za akina Jenifer Lopez au Rihana, na kadhalika.

Hakika ziara yako itaisha ukiwa jela au umeshakufa kwa sababu hayo maisha si ya kwako. Kondoo wote wana ngozi ya kawaida, yenye vitundu vya hewa. Lakini wa Australia kajazwa sufu zaidi ya yule wa Gongolamboto ili kumkinga na baridi kali. Wanyama wengine wenye ngozi kama zetu ndio wana jeuri ya kutembea huku kwenye joto kama jiko la mkaa.

Kila jamii duniani ina namna ya kujiakisi. Inajirekebisha pale inapopoteza uelekeo na kujihami dhidi ya tamaduni zisizofaa.

Hata siku moja usitegemee kumkuta tajiri wa Wahindi Wekundu kule New Mexico au bilionea wa Kimaoris huko New Zealand akitembelea Cadillac badala ya gari la farasi. 
Hadi hivi leo matajiri wenye visima vya mafuta kandoni mwa Jangwa la Sahara hutumia ngamia katika safari zao za starehe.

Kwa vile katika maisha halisi watu hao husafiri kwa ngamia, kwenye maigizo yao pia huigiza na ngamia. Sababu kuu ni kuiakisi jamii yao kwa kutumia kioo halisi. 
Cadillac isingehimili ulaini wa ardhi yao kama awezavyo ngamia, na isingeweza kuishi bila maji kama ngamia mwenye tangi orijino la kuhifadhia maji ya kunywa na kuoga kwa mwezi mzima.

Hivi ndivyo Mungu alivyoumba viumbe na mazingira yao. Kama utapenda utanunua kioo kilichochorwa picha yako, utajiangalia kila asubuhi kujiridhisha na unadhifu wa picha lakini ukitoka kwenye kioo unabaki kuwa yuleyule mwenye makunyanzi. Huna tofauti na mpiga tungi anayelewa ili asahau deni lake.

Kioo muhimu cha kuakisi mwenendo wa mwanadamu ni fasihi, na sehemu kubwa ya fasihi ni sanaa. Kwa bahati tuna wasanii wengi sana wanaofanya sanaa nyingi mno katika kila pembe ya dunia. Fikiria kama Tanzania tu ina ngoma, muziki, ushairi, ngonjera, uchoraji, uchongaji, ufinyanzi, ushonaji, sarakasi na nyingine nyingi usizozikumbuka haraka, je huko Uarabuni, Uchina na Uajemi. Zipo nyingine za aina ngapi tusizokuwa nazo hapa?

Kama vile uonavyo maajabu ya mtende kuota jangwani, kadhalika kuna maajabu ya sanaa kule ambazo hujapata kuziwazia. Na zote zinalenga kukosoa, kufundisha na kuendeleza utamaduni wa watu na maisha yao halisia. 

Kule Jangwani unaweza kutoiona Ferrari wala Benzi kwenye muvi nzima, lakini ukashangaa kuona picha hilo limeorodheshwa kwenye vinyang’anyiro vya muvi bora za dunia.      

Lakini sisi ambao madaktari wetu wanagombea daladala, kwenye muvi zetu ndio wanaomiliki majumba makubwa kando ya bahari na kumiliki magari ya Posh na Buick matatu matatu.

Kutokana na kuendekeza muonekano huo wa hali ya juu, huko mitaani wasanii wetu wamekuwa wakiazima magari ya kifahari na kukodi pamba za bei mbaya ili waonekane kama kwenye kideo.

Tunawaona wengi huku uswazi ambao baada ya kuigiza kama mmiliki wa ghorofa la ufukweni, akawa akitoka chumbani kwake Tandika kama anayekimbia mvua, ati kwa kuogopa kuonekana na mashabiki zake. Vurugu za kurikwesti usafiri zimekuwa nyingi kutoka magari ya kifahari hadi kwenye bajaji.

Hii ni sababu mojawapo inayozorotesha soko la sanaa yetu. Baadhi ya waigizaji wetu (nimesema baadhi) wanaiga filamu zilizokwisha kuchezwa Ulaya na Marekani, wanaiga mpaka tamaduni za huko na kuondoa uasilia wetu. Wakiona katika maigizo ya wenzetu baamedi anamiliki gari, na wao wanataka kukopi bila kuzingatia uhalisia. 

Angalau basi waige kisa (maana wanadamu tunashabihiana), wakakicheza kwenye maisha yetu ya kawaida. Unapomuibia mwenzio majibu kwenye mtihani, epuka kunakili jina lake.