Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watanzania wanapenda sanaa lakini hawawajali wasanii

Muktasari:

  • Awali katika jamii mbalimbali za asili, wasanii waliheshimika na kulelewa na jamii yao kwa njia mbalimbali.  Wasanii maarufu waliweza kusafiri vijiji mbalimbali ambako walipokelewa na kukarimiwa kadri ilivyowezekana.

Dar es Salaam. Hakika jambo moja ambalo wasanii huja kugundua baada ya kuanza kutegemea sanaa kuendesha maisha yao, ni kuwa sehemu kubwa ya jamii ya Watanzania, wanapenda sanaa lakini hawajalii wasanii.


Awali katika jamii mbalimbali za asili, wasanii waliheshimika na kulelewa na jamii yao kwa njia mbalimbali.  Wasanii maarufu waliweza kusafiri vijiji mbalimbali ambako walipokelewa na kukarimiwa kadri ilivyowezekana.

Walikuwa ndio wenye kazi ya kuweka hadharani yaliyojificha mazuri au mabaya, walitoa ushauri, elimu na pia walikuwa kiungo muhimu kati ya walio hai na walio wafu, kutokana na aina mbalimbali za sanaa walizokuwa wakizifanya katika jamii.


Katika makabila mengine wasanii walikuwa ndio njia ya kuunganisha wananchi na viongozi wao. Katika kabila la Wahehe, chifu alikuwa na msemaji wake ambaye aliitwa Kilongumutwa. Huyu pamoja na kuwa na kazi ya kutangaza maamuzi ya Mutwa au chifu, pia alikuwa msanii mchekeshaji ambaye alikuwa akiruhusiwa hata kumtania Mutwa.  Mutwa akiwakosea wananchi, basi Kilongumutwa aliweza kutengeneza utani kuhusu jambo hilo ili Mutwa ajue aliyekosewa alivyojihisi. 


Utamaduni ulikuwa upo hata kwa wafalme wa Uingereza wa zamani, walikuwa na mtu aliyeitwa ‘court jester’, kazi yake ilikuwa ni kumchekesha mfalme na maswaiba wake, nae alikuwa akipitisha  vilio vya wananchi katika vituko vyake. Kwa njia ile Mutwa na mfalme walipata taarifa ya kinachoendelea kwa wananchi wao.


Wasanii wanamuziki, pia walikuwa na nafasi hiyo katika jamii zao. Wanamuziki walitunga nyimbo ambazo zilielezea kila kilichokuwa kikiendelea katika jamii, kizuri au kibaya. Wakaheshimika na kutunzwa na jamii zao kwa kazi hizo.


Maingilio ya jamii kutoka upande mwingine wa dunia, yalileta tafsiri mpya ya sanaa. Tafsiri ya sanaa ajira au biashara ikaanza kuenea. Teknolojia mpya kama santuri na redio, luninga na hatimae internet zikaongeza upana wa ajira katika sanaa na biashara ya sanaa, lakini vikapunguza  uwezo wa Sanaa na msanii kuelimisha jamii yake.


Biashara ya sanaa imebadilisha sana hali za msanii. Usanii unapimwa kwa ukubwa wa biashara ambayo itatokea, kwani hilo ndilo lengo halisi la kufanya biashara. Sanaa imeanza kupoteza ile sifa yake ya kuwa kielelezo cha utamaduni, kwani hiyo si kazi ya biashara. Bahati mbaya hata serikali nayo inauangalia utamaduni kama ajira na biashara.  


Na msanii sasa anathaminiwa kwa ukubwa wa kipato chake. Hebu fikiria serikali ianze kutangaza kuwa maji ni ajira maji ni biashara, moja kwa moja inajiondoa katika kutoa huduma ya maji, na hilo ndilo linaloendelea kwenye utamaduni na sanaa.


Si ajabu kabisa kuwa mabadiliko haya ya kuifanya sanaa ni biashara yameanza kufanya sanaa kuendeshwa kwa utashi wa kibiashara. Mifumo iliyokuwa imewekwa kutoa nafasi kwa sanaa kuwa ni moja ya vielelezo vya utamaduni inapotea taratibu. Ziko wapi kumbi zilizokuwa maarufu kwa maonyesho ya sanaa? Kulikuwa na kumbi za Manispaa, kumbi za Wilaya, kumbi za Umoja wa Vijana wa CCM, nyingi zimebadilishwa matumizi ili ziwe ‘vyanzo vya mapato’. 


Si ajabu kabisa kuzunguka mkoa mzima ukakuta hauna ukumbi unaomilikiwa na umma kuendeleza sanaa ambazo si za kibiashara. Sanaa kama vile michezo ya jukwaani au maonyesho ya ngoma za asili na kadhalika. Zile zinazoitwa kumbi za burudani, karibu zote ni sehemu za kuuzia pombe, hata maonyesho ya sanaa mbalimbali nia yake si kuendeleza sanaa bali kuuza vinywaji na vitafunio. Sanaa hutumika kama kivutio tu cha biashara.


Kwa kudharau Sanaa, utamaduni nao unadharaulika na kupotea. Si mara moja nasikia watu wakilaumu kizazi cha Gen Z kwa kukosa maadili, swali ni kuwa wapi watu hawa walifundishwa maadili? Unamdai mtu deni ambalo hujawahi kumkopesha.


Kwa tuliomo kwenye tasnia tunaiona hali ilivyo mbaya, na tunawaza hivi itakuwaje huko mbele kama juhudi za makusudi hazitatumika kugeuza mkondo. Kwa mtazamo wangu hali hii ilianza kujijenga 1995, ni miaka zaid ya thelathini, mwalimu muongoza maadili hajaonekana shuleni, Je ni wanafunzi wangapi wamemaliza shule bila somo hilo?
Katika kipindi hicho hicho ambacho sanaa inaitwa ni kazi na ajira, jamii imekuwa ikilelewa kuwa sanaa ni bure. Ukiingia baa, kinywaji na vitafunwa utalipia lakini  sanaa pale jukwaani utaipata bure.


Si ajabu kabisa watu kusambaziana bure maelfu ya nyimbo kila siku kwenye mitandao ya whatsapp na telegram. Vyombo va utangazaji vimegoma kulipia matumizi ya kazi za wasanii kwa miaka sasa. Ndio nasema tena, jamii ya Watanzania inapenda sanaa lakini haiwajalii wasanii.