Anko Kitime: Historia ya bendi za Iringa kuanzia miaka ya 80
Muktasari:
- Wakati huo ilikuwa kama ni utamaduni kila bendi mpya ilijitahidi kuwa na vyombo aina ya Ranger FBT au Orange, aina hii ya vyombo ilikuwa ni kutoka Italia.
Dar es Salaam. Katikati ya miaka ya 1980, wafanyakazi wa kiwanda cha kuchonga almasi cha Iringa, Iringa Diamond Cutting Company, walichanga fedha na kununua vyombo vya bendi. Fedha hizo ziliweza kununuliwa kwa seti nzuri sana ya vyombo aina ya Yamaha kutoka Japan.
Wakati huo ilikuwa kama ni utamaduni kila bendi mpya ilijitahidi kuwa na vyombo aina ya Ranger FBT au Orange, aina hii ya vyombo ilikuwa ni kutoka Italia.
Kupatikana kwa vyombo hivyo kukawezesha kuzaliwa kwa bendi ya Tancut Almasi Orchestra. Wanamuziki wa kwanza wa Tancut Almasi Orchestra wengi walikuwa wenyeji wa Iringa, kati yao wakiwamo Juma Msosi, Mamado Kanjanika, Hashim Kasanga baadae John Kitime.
Uongozi wa kiwanda cha Iringa Diamond Cutting Company, ulimuita mwanamuziki Ndala Kasheba kwa muda nae alikaa kwa muda mfupi sana na bendi hiyo, lakini masharti yake ya kuajiriwa na bendi yaliushinda uongozi. Lakini Kasheba ndie aliyewaita Kasaloo Kyanga, Kyanga Songa na Mafumu Bilali kujiunga na Tancut Almasi Orchestra.
Tancut Ilikuja kuwa kati ya bendi bora nchini. Katika mashindano ya bendi yaliyoitwa Top Ten Show, bendi hii ilichukua moja ya zawadi zawadi za juu katika kila ‚category‘ iliyokuwa inashindaniwa.
Kulikuwa na category tatu, wimbo wowote wa bendi, wimbo ambao umetokana na muziki wa asili wa kabila lolote Tanzania, na kila bendi ililazimika kutunga wimbo ulioitwa Nakulilia Afrika.
Katika uhai wake bendi hiyo ilirekodi nyimbo zake katika mitindo mbalimbali, ilianza na mtindo iliyouita Mangala Dance, kisha Fimbo Lugoda, Kinye Kinye Kisonzo na hatimaye Mbuguswa dance.
Bendi ilirekodi nyimbo nyingi sana, nyingine bado zinapigwa na bendi mbalimbali hadi leo. Kati ya hizo nyimbo hizo kulikuweko na Masafa Marefu, Nimemkaribisha nyoka, Kashasha, Ngoma za Afrika, Butinini na nyinginezo nyingi.
Bendi ya Tancut ilisambaratika mwanzoni mwa miaka ya 90 kutokana na kufungwa kwa kiwanda cha Diamond Cutting Company.
Wanamuziki kadhaa waliotoka Tancut Almasi Orchestra iliyokufa walikuja kuanzisha bendi iliyoitwa Ruaha International Orchestra. Jina hilo lilitokana na utamaduni wa wakati huo wa vikundi vya muziki kujiwekea kisifa cha ‘International‘.
Kulikuwa na Dar es Salaam International Orchestra, Dodoma International Orchestra, Tanga International Orchestra, Rukwa International Orchestra na kadhalika. Bendi ilikuwa mali ya mfanyabiashara Batista Mtandi na iliongozwa na Kalala Mbwebwe.
Ruaha International ilikuwa na nyimbo zilizokuja kupendwa sana nyingi zikiwa tungo za Kalala Mbwebwe, nyimbo kama Fanta wangu na Lutadila zilijulikana Afrika ya Mashariki nzima hasa kwa kuwa Kalala alizirekodi tena Nairobi na kuweza kutengeneza santuri.
Bendi nyingine iliyowahi kuweko Iringa ilikuwa ni VICO Stars. Bendi hii ilikuwa mali ya Kanisa Katoliki la Mshindo ambalo linaongozwa na shirika la Consolata.
Vico ilikuwa kifupi cha Vijana Consolata. Japokuwa bendi hii iliwahi kuwa na wanamuziki wakubwa kama Anania Ngoliga, malengo ya bendi hii haya kuwa ya kibiashara hivyo haikudumu muda mrefu, wala hakuna kumbukumbu kuwa ilirekodi nyimbo.
Mfanyabiashara mmoja maarufu alianzisha hoteli aliyoiita Living Light Hotel. Hoteli hii nayo ilianzisha bendi yake iliyoitwa Living Light Band. Pia wanamuziki maarufu waliwahi kupita katika bendi hii lakini nayo haikuweza kufikia umaarufu mkubwa na ilikufa mapema sana, bila hata kurekodi nyimbo zozote.
Kwa sasa Iringa kuna bendi kadhaa lakini bendi hizi kama ilivyo kwa bendi nyingi za siku hizi, hazionekani kuwa na malengo ya kurekodi, au kuchukua nafasi yake katika orodha ya bendi kwa kutunga nyimbo zao na kurekodi.
Asilimia kubwa ya bendi zimejikita katika kurudia nyimbo ambazo zimekwisha rekodiwa zamani. Na zile bendi ambazo zinatunga nyimbo zao, zimejikita kuiga kila kitu kwenye makundi yanayoongozwa na wanamuziki kama Fally Ipupa.
Na hakika huiga kila kitu kuanzia mavazi, staili ya kuimba na hata staili za kupiga. Unaweza ukaingia katika bendi ziko miji mitatu tofauti ukadhani ni bendi ileile.
Uigaji wa namna hii sio mgeni kabisa, katika miaka ya 60 bendi nyingi za Tanzania kama ilivyo leo zilikuwa zikiiga kila kitu kutoka Kongo, mpaka pale serikali ilipoingilia na kuzishauri bendi kuacha kuiga.
Matokeo ya ushauri huo na muziki wa Tanzania kupanda chati sana katika miaka ya 70 na 80. Kazi hii ilirudishwa nyuma tena kuanzia miaka ya 90 hasa radio za FM zilipoanza kuwa maarufu, kwani zilirudisha tena ‘promosheni’ ya muziki wa nje kwa nguvu kubwa.