Anko Kitime: Zama za uhusiano wa siasa na muziki zinapotea
Muktasari:
- Kikundi maarufu cha taarabu cha Egyptian Musical Club kwa mfano, kilishiriki kwa hali na mali katika harakati za kusaka Uhuru. Chama cha TANU kilikuwa kikiazima hata vipaza sauti na spika kutoka kundi hili kwa ajili ya mikutano yake.
Dar es Salaam. Katika zama hizi mwanamuziki au kundi la muziki kujikita kushirikiana na chama cha siasa inaonekana kama kuna mshkeri, lakini historia inatukumbusha kuwa muziki ulikuwa sehemu kubwa na muhimu katika kupigania Uhuru wetu.
Kikundi maarufu cha taarabu cha Egyptian Musical Club kwa mfano, kilishiriki kwa hali na mali katika harakati za kusaka Uhuru. Chama cha TANU kilikuwa kikiazima hata vipaza sauti na spika kutoka kundi hili kwa ajili ya mikutano yake.
Egyptian Musical club iliwahi hata kusindikizana na Mwalimu Nyerere kwa safari zake za kampeni ya kusaka Uhuru.
Kuna wakati Mwalimu Nyerere alipopigwa marufuku na serikali ya kikoloni asitoe hotuba hadharani, Egyptian Musical Club wakawa wanamualika kwenye maonyesho yao ili aweze kuzungumza na wapenzi wa club hiyo.
Kikundi kingine maarufu cha Taarab kilichofanya mengi wakati wa kutafuta Uhuru kilikuwa ni kikundi cha Alwatan Musical Club, matawi ya TANU ya Dar es Salaam yalipenda sana kukitumia kikundi hiki kufanya michango ya kuendesha chama.
Kulikuweko na kundi jingine la muziki lililoitwa Tanganyika Sports Musical Club, kundi hili lilifanya safari za maonyesho nje ya Dar es Salaam na katika maonyesho yao wanachama wapya wa TANU walisajiliwa, na sehemu ya mapato ya viingilio vya maonyesho vikawa mchango kwa ajili ya TANU.
Kati ya wanawake maarufu waliofanya kazi kubwa ya kuhamasisha kujiunga na TANU , alikuwa Bibi Titi Mohamed. Kwa kutumia ngoma kikundi chake cha ngoma aliweza kupata wanachama wapya wa TANU 5000 katika mwaka mmoja.
Kikundi chake nacho kilikusanya michango kwa ajili ya TANU na ngoma ya Lele mama ilitumika sana kuhamasisha watu kuhudhuria mikutano ya TANU na kuchangia uhai wa chama chao.
Nchi nzima kulikuwa na wanamuziki wakitunga nyimbo kwa kutumia ngoma za asili na muziki wa dansi na Taarab kuhamasisha watu kuungana na kudai Uhuru. Mwanamuziki Frank Humplick ambaye baba yake alikuwa mzungu kutoka Austria na mama yake Mchaga na alijulikana zaidi kama kijana wa Kichaga aliwahi kutunga wimbo ulioitwa I am a democrat , wimbo huu uliokuwa ukielezea kishahiri mambo yatakavyokuwa Uhuru ukipatikana, wimbo huu ulimchukiza sana mkoloni.
Amri ilitolewa kuwa santuri za wimbo huu zisakwe nyumba kwa nyumba na kuvunjwa. Askari walipita majumbani na kuvunja santuri zenye wimbo huo. Wimbo huu ulikuwa mmoja wa nyimbo zilizotumika kabla ya mikutano aliyokuwa akihutubia Mwalimu Nyerere wakati huo.
Katika mikoa ya kusini wanamuziki kama Mzee Moses Nnauye walianzisha vikundi vya muziki kuhamasisha kudai Uhuru na ujumbe uliwafikia vizuri wananchi wengi.
Hatimaye tarehe Desemba 9, 1961, tulipata Uhuru. Wanamuziki wa kila aina ya muziki walitunga nyimbo zilizoongelea furaha ya kupata Uhuru na nyimbo nyingine zikawa zinaongelea ndoto za wananchi baada ya uhuru, kauli mbiu wakati huo ikiwa ni Uhuru na Kazi.
Mahusiano ya muziki na siasa yaliongezeka sana baada ya Tanzania kuamua kuwa nchi ya Kijamaa, serikali kwa kujua uwezo na kazi iliyofanywa na wasanii, iliwekeza sana katika sanaa. Kulikuweko na Maafisa Utamaduni wa Wilaya na Mkoa ambao hata bajeti yao ilitoka serikali kuu.
Maafisa utamaduni wakahamasisha kuanzishwa vikundi vya muziki wa aina mbalimbali mpaka vijijini, mashirika ya umma yalihamasishwa kuanzisha vikundi vya sanaa, na ndipo kukawepo vikundi vyaa sanaa vya Taifa, vikundi vya sanaa majeshini ambapo huko ndani yake kukawa na vikundi vya taarab na dansi.
Mashirika kama Bima, DDC, URAFIKI na mengine mengi yakawa na vikundi vya Sanaa maarufu, Kurugenzi za mikoa Dodoma na Arusha nazo zikaanzisha vikundi, bila kusahau Women Jazz Band bendi ya vijana wa kike wa TANU Youth League, na baadae Umoja wa Vijana wa TANU nao ukawa na bendi yake maarufu Vijana Jazz band.
Vikundi vyote hivyo vilishiriki sana katika kuimba nyimbo mbalimbali za siasa, na maendeleo. Pamoja na bendi na vikundi vya taarabu, wasanii maarufu walikuja kupatikana akina Mzee makongoro , Mzee Mwinamila, John Komba na kadhalika.
Zama hizi ziko tofauti sana, unaweza kuhisi kuwa umuhimu wa sanaa umesahaulika mengi yamebadilika. Hakuna tena sehemu za Sanaa zinazomilikiwa na serikali. Majumba yale ya community center yamepotea kwa kubadilishwa matumizi.
Viwanja zilipokuwa zinachezwa ngoma za asili kila mwisho wa wiki zimepotea. Si ajabu kabisa kusikia kauli mbiu za ‘ Sanaa ni biashara’. Kipengele cha Sanaa ni biashara ni kipengele kidogo cha Sanaa, ambayo kwanza ni utambulisho wa jamii.
Siku hizi ni nadra kusikia wimbo wa kuelimisha ukisikika katika vyombo vya utangazaji, zinasikika tu nyimbo ambazo ni za ‘kibiashara’. Na biashara haijali maadili wala utamaduni, biashara huelewa fedha tu.