Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenye watoto, walioolewa ruhusa kushiriki Miss Universe 2025

Muktasari:

  • Mchakato huo, ambao kwa sasa uko katika hatua ya awali, unalenga kuwachuja washiriki 30 bora watakaoingia kambini kwa kipindi cha mwezi mmoja. Fainali ya shindano hilo inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa Septemba 2025

Dar es salaam. Mchakato wa shindano la kumsaka Miss Universe Tanzania kwa mwaka 2025 umeanza rasmi katika eneo la Mbezi Jogoo, jijini Dar es Salaam.

Mchakato huo, ambao kwa sasa uko katika hatua ya awali, unalenga kuwachuja washiriki 30 bora watakaoingia kambini kwa kipindi cha mwezi mmoja. Fainali ya shindano hilo inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa Septemba 2025.

Akizungumza na wanahabari wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Millen Prive Millen Magese, amesema shindano la mwaka huu limeweka historia kwa kuondoa baadhi ya masharti yaliyokuwa yakilalamikiwa na wanawake wengi nchini.

“Naomba niwatoe hofu, maana wadada wengi wamekuwa wakihofia kushiriki mashindano haya kutokana na vikwazo mbalimbali. Mwaka huu, kwa washiriki wote watakaochaguliwa kwenda kambini, mavazi yote yatatolewa bure. Lakini pia tumevuka mipaka ya zamani hata wanawake waliokwisha jifungua tunawakaribisha kushiriki,” amesema Millen.

Akaongeza kuwa hata wanawake walio kwenye ndoa sasa wanaruhusiwa kushiriki shindano hilo, ikiwa ni hatua ya kulifanya kuwa jukwaa jumuishi na lenye kutoa nafasi kwa wanawake wa makundi yote kuonesha vipaji vyao.

"Hii ni fursa ya pekee kwa wanawake wote, bila kujali hali zao za ndoa au familia. Tumeamua kuwa jukwaa la kweli la mabadiliko ya kijamii," amesisitiza

 
Aidha, aliwapongeza wazazi waliowaruhusu watoto wao kushiriki shindano hilo, akisema hatua hiyo ni ishara ya kuthamini vipaji vyao na kuwaamini katika safari ya kujitambua.

Kwa upande wake, Judith Ngusa, aliyeshinda taji la Miss Universe Tanzania mwaka 2024, aliwatia moyo washiriki waliokuwa wakijitokeza leo kwa ajili ya mchujo wa awali.

“Kushiriki tu kwenye mashindano haya ni hatua kubwa sana kwenye maisha. Unajifunza nidhamu, ujasiri, mitazamo mipya na hata jinsi ya kujitambulisha mbele ya jamii. Ni safari ya kujikuza, siyo tu kimwonekano, bali hata kiakili,” amesema Judith.

Naye David Malisa, ambaye ni mmoja wa waratibu wakuu wa mashindano hayo, amesema mchakato huo ulianza mapema mwaka huu katika mikoa mbalimbali, na sasa Dar es Salaam imepewa nafasi kuonesha uwezo wake.

“Tumehitimisha awamu za mikoani, sasa ni zamu ya Dar es Salaam. 

Tunatarajia kuona vipaji vipya na ushindani mkubwa kutoka kwa wanadada wa jiji hili,” amesema Malisa.

Mashindano ya Miss Universe Tanzania mwaka huu yanatarajiwa kuwa ya aina yake, si tu kwa kuvunja vikwazo vya kijamii, bali pia kwa kutoa majukwaa mapya ya kukuza vipaji na kukuza sauti ya wanawake katika jamii.