Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wimbo wa Remmy wageuka wa kuombea hela

Muktasari:

  • Kundi la Orchestra Makassy wakati huo lilikuwa na miamba ya muziki Mzee Makassy mwenyewe, Mosese Fan Fan, Dr Remmy Ongala, Aimala Mbutu, Issa Nundu, Ramadhani Kinguti, Kyanga Songa,  Andy Swebe, Hemedi Mganga, Kulwa Milonge, Keppy Kiombile na wanamuziki wengine wengi  wazuri, ilikuwa inatisha kuwa mmoja kati ya miamba hawa

Mwaka 1984 niliacha ghafla bendi ya Orchestra Mambo Bado, haukuwa mpango wa muda mrefu, niliamua tu ghafla kuacha bendi baada ya kurudi safari ya maonesho tuliyokwenda kuyafanya mkoani Tanga.

Nikiwa nyumbani sijaamua niende kujiunga na bendi gani, binamu yangu Andy Swebe ambaye pia alikuwa mpiga gitaa la bezi katika kundi la Orchestra Makassy  akanifuata nyumbani na  kunieleza kuwa natakiwa na bendi yake, hilo lilikuwa jambo la heri sikuwa na kipingamizi  na kesho yake nilifika Kinondoni Moscow nyumbani kwa mzee Makassy tayari kabisa kujiunga na kundi hilo maarufu.

Kundi la Orchestra Makassy wakati huo lilikuwa na miamba ya muziki Mzee Makassy mwenyewe, Mosese Fan Fan, Dr Remmy Ongala, Aimala Mbutu, Issa Nundu, Ramadhani Kinguti, Kyanga Songa,  Andy Swebe, Hemedi Mganga, Kulwa Milonge, Keppy Kiombile na wanamuziki wengine wengi  wazuri, ilikuwa inatisha kuwa mmoja kati ya miamba hawa.

Fan Fan alikuwa ametunga nyimbo zake mbili na mazoezi makali yalikuwa yanaendelea. Fan Fan akiwa kwenye solo, Mzee Aimala Mbutu kwenye second solo, Mzee Hemedi Mganga kwenye  gitaa la rhythm, nyuzi zilikuwa zinalia kwa uhakika.

Bahati mbaya sijawahi kusikia nyimbo hizo kama zilikuja kurekodiwa na Fan Fan mwenyewe, moja kati ya nyimbo hizo nakumbuka ziliitwa Bolingo Maladi, kwa haraka unaweza kutafsiri kuwa mapenzi ni maradhi.

Nilianza kazi Orchestra Makassy, nikiwa nadandia kupiga gitaa la rhythm katika nyimbo chache lakini hasa nilikuwa muimbaji wa nyimbo za Kiingereza, wimbo nilioanzia kazi ulikuwa ni Reggae Night wa Jimmy Cliff.

Dr Remmy Ongala na Mosese Fan Fan wakati huo walikuwa wametokea bendi ya Super Matimila. Dr Remmy alikuwa karudi nyumbani kwani mara baada ya kuingia nchini kutoka Kongo, bendi yake ya kwanza ilikuwa Orchestra Makassy. Na ndipo kwa mara ya kwanza akaanza kuimba wimbo ‘Narudi Nyumbani’ akitumia maneno haya,

Narudi nyumbani, Narudi kwa mjomba, kwani alikuwa anaeleza kuwa Mzee Makassy alikuwa mjomba wake.

Watu wengi wanaufahamu wimbo huu ukiwa na maneno, ‘Narudi nyumbani, narudi Matimila’, kwani hayo ndiyo maneno aliyoyatumia alipokuja kuurekodi wimbo huo akiwa Orchestra  Super Matimila, hiyo ni baada ya kumuacha mjomba wake kwa mara ya pili na kuirudia tena bendi hiyo ambayo alidumu nayo mpaka siku zake za mwisho.

Fan Fan hakukaa sana Orchestra Makassy baada ya hapo ndipo alipoondoka na kuhamia Uingereza.

Katika awamu yake ya pili, Dr Remmy alikuwa na mkataba maalumu na Mzee Makassy, alikuwa analazimika kuwa jukwaani kwa saa mbili kila onesho, na hakika alikuwa akipanda jukwaani, vibao vyake vyote maarufu vilikuwa viliporomoshwa, kuanzia vile alivyovirekodi akiwa Orchestra Makassy katika awamu ya kwanza kama vile siku ya Kifo, Harusi ya Mwanza na vinginevyo ambavyo alianza kutunga.

Kati ya nyimbo mpya alizotunga ulikuweko wimbo ulioitwa, ‘Nimefika nimeona’, katika wimbo huu Dr Remmy alikuwa akiimba kuhusu mikoa yote nchi akiutaja mmoja mmoja, na wilaya zake, na sifa za watu wake, ulikuwa wimbo mrefu sana, mara nyingi alikuwa akianza mkoa wa Mtwara, baadhi ya maneno yalikuwa haya,

Nimefika nimeona kwa macho yangu mwenyewe, Mazingara ya nchi na wananchi wanaishi vipi,
Nimefika Mtwara,
Nimewakuta Wamakonde,
Wanapenda sana Sindimba,
Wanalima sana Korosho’

Kwa vile alikuwa bingwa wa kutunga maneno ya papo kwa papo aliweza kuongeza sifa nyingi za watu wa kila sehemu aliyoitaja.

Basi aliziimba wilaya zote za Mtwara na kisha kuhamia mkoa mwingine mpaka alipomaliza nchi nzima, ni rahisi kugundua wimbo huo mmoja ulikuwa mrefu mno na ulichukua zaidi ya saa moja.

Wanamuziki wakaitisha kikao kulalamikia urefu wa wimbo huo na kumtaka Remmy afupishe wimbo huo, kikao kile kilikuwa kigumu sana na ngumi zilitaka kurushwa,  ni katika kipindi hiki ambapo Dr Remmy aliamua kurudi tena Super Matimila.  

Wikiendi iliyopita niliingia kwenye onesho la bendi moja maarufu, siku hizi ni kawaida ukiingia kwenye bendi kukuta bendi ikipiga nyimbo mbalimbali za bendi za zamani, wengine wakiwa wameiga vizuri, wengine wakiwa wazi hawakushughulika kuufanyia mazoezi wimbo wanaoupiga.

Lakini safari hii nilikutana na ubunifu mpya, kwanza sijui kwa kujua au kwa ubunifu, bendi hii ilikuwa imeunganisha nyimbo mbili za Dr 
Wimbo wa Remmy wageuka wa kuombea hela

Remmy, ‘Narudi nyumbani’ na ‘Nimefika nimeona’. Katika kuunganisha huko, muimbaji alikuwa amegeuza tungo hizo na kuwa wimbo mmoja wa kuombea fedha. 

Muimbaji alianza na kuimba narudi nyumbani, kisha kuanza kutaja mikoa na wilaya mbalimbali kama ilivyokuwa kwa wimbo ‘Nimefika nimeona’, ila sasa kwenye kila wilaya mwimbaji alikuwa akiyataja makabila na kuyapa sifa kuwa huwa yanatuza sana fedha, kwa mfano kati ya maneno yalikuwa,
 ‘ Narudi Iringa,
 Iringa kuna Wahehe,
 Wanapenda sana kutuza,
Wanatuza noti nyekundu nyekundu tu,
Wanatuza kuliko kabila jingine’,

Na hivyo hivyo kuendelea na makabila kutoka pande mbalimbali za nchi, nikaona watu wanapanga foleni kutetea sifa kila kabila lao lilipotajwa, kweli mjini shule. Lala Pema Dr Remmy Ongala, wajukuu zako bado wanaishi kwa nyimbo zako.