Kodi kubwa zinawanyima fursa Watanzania kumiliki simu bora

Tanzania ina kiwango kikubwa cha kodi na ushuru inaotoza kwenye simu za mkononi ikilinganishwa na mataifa mengine duniani.

Viwango hivyo vinaelezwa kuwa juu kuliko mataifa mengi ya kusini mwa Jangwa la Sahara, Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, Ulaya, Asia hata Amerika Kusini, hatua inayowadumaza Watanzania kumiliki simu janja.

Ingawa kodi na ushuru hubadilika mara kadhaa, ripoti ya Shirikisho la Kampuni za Simu Duniani (GSMA) iliyotolewa mwaka 2021 inaonyesha Tanzania inakusanya asilimia 34 ya tozo na ushuru kwenye kila simu inayouzwa kwa mteja.

Kiwango hicho ni kikubwa kuliko asilimia 21 kinachotozwa Ulaya au asilimia 18 huko Amerika ya Kusini na asilimia 26 kusini mwa Jangwa la Sahara. Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika kodi ni asilimia 24 sawa na Asia.

Taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), tozo na ushuru unaokatwa kwa kila simu inayopita bandarini ni asilimia 18 zikijumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ushuru wa maendeleo ya reli na kodi ya bandari.

Kutokana na hali hiyo, bei ya simu moja nchini hujumuisha zaidi ya theluthi moja inayoenda kwenye kodi na ushuru wa Serikali.

Simu ya Sh350,000 kwa mfano, inabidi iuzwe kwa Sh500,000, kwa hiyo mzigo wa Sh150,000 ni kodi na ushuru unakwenda kwa mteja wa simu hiyo.

Kutokana na mazingira hayo, baadhi ya wafanyabiashara wa simu janja wanasema Serikali inaweza kukwama kufanikisha malengo yake ya kufikia asilimia 80 ya wananchi kutumia intaneti ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 46 ya sasa, hivyo kushauri kuurejesha msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye simu janja ambao Serikali iliutoa kwenye bajeti ya mwaka 2021/22, ikihusisha pia vishikwambi (tablets) na modemu kabla ya kuufuta mwaka 2022/23 kwa madai ya kutoona mabadiliko ya bei kwa walengwa.

Hafsa Mohamed, meneja mauzo wa duka la simu za Infinix lililopo Kariakoo anasema baada ya kuondolewa kwa kodi hiyo simu ya Sh260,000 ilishuka hadi Sh210,000, huku ya Sh1.4 milioni ikiuzwa Sh1.18 milioni.

“Nilikuwa nauza simu janja 15 hadi 20 kwa siku, ila sasa hivi ni chini, napata wateja watano. Kasi imepungua,” anasema Hafsa.

Reginald Asenga, meneja mauzo duka la simu za kampuni ya Vivo anasema simu ya Sh270,000 ilishuka mpaka Sh229,000 VAT iliposamehewa, lakini baada ya kurejeshwa inauzwa kwa bei yake halisi ya Sh270,000, hivyo akashauri zikaribishwe kampuni kubwa za simu kuja kuwekeza kwa masharti nafuu. Vivo inauza wastani wa simu 5,000 kika mwezi nchini.

“Kampuni hizi kubwa zilikuja kuwekeza nchini badala ya wananchi kufuata simu nje, itaongeza ushindani hivyo kupunguza bei kwa mtumiaji wa mwisho, kwani wengi wataweza kuzipata hapahapa kwa bei nafuu,” anasema Asenga.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara, Dk Donath Olomi anasema Serikali inatakiwa kulitizama suala hilo kwa hesabu zitakazosaidia kupunguza umaskini kwa wananchi, kuongeza wigo wa mapato na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.

“Ni hesabu tu, inabidi waangalie (Serikali) kwa kutambua kwamba endapo tutaondoa kodi nyingi ili watumiaji waongezeke manufaa yatakuwa mengi kuliko uchukuaji wa kodi kabla ya kupata simu hizo. Kama mataifa ya wenzetu kodi ziko chini basi wananufaika zaidi kuliko sisi,” anasema Dk Olomi.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya Oktoba 2022 inaonyesha kuna jumla ya simu za 2G (viswaswadu) milioni 52.3 pamoja na simu janja milioni 17 pekee zinazotumika nchini, sawa na asilimia 27 ya mawasiliano ya 3G kwa idadi ya watu milioni 62 nchini.

Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ben Mwaipaja anasema Serikali ilianza kukusanya maoni kwenye sekta hiyo Novemba mwaka jana, katika kongamano la kuboresha sera za kodi.

“Walikuwepo maofisa wa kampuni za simu, kwa hiyo kama maoni hayo waliyatoa basi wasubiri kwenye wasilisho la bajeti kuu ya Serikali itakayosomwa Juni huenda yakawepo. Haya maoni pia tunayapokea, lakini tunashauri wafanyabiashara kujenga uaminifu wa kulipa kodi kwa hiari,” anasema Mwaipaja.


Kwa nini sasa?

Wito kusamehe VAT umetolewa siku chache baada ya kutangaza mwelekeo wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha kusomwa, ukibainisha unalenga kuhamasisha kujenga uchumi wa kidijitali kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi wananchi kuzitumia fursa zilizopo kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (Unicef) mwaka 2021 inaonyesha asilimia 75 ya waliohojiwa walisema kikwazo kikubwa cha kumiliki simu janja kwao ni gharama kubwa, huku asilimia 12 wakilalamikia gharama kubwa za intaneti na asilimia saba ubovu wa miundombinu ndio tatizo kwao.

Wakati mradi wa Tanzania ya kidijitali wa miaka mitano ukiendelea kutekelezwa, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari anakiri changamoto hiyo akidai Serikali inaendelea na juhudi za kuongeza matumizi ya simu janja zinaendelea.

“Serikali kwa sasa chini ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) iko kwenye maandalizi ya kushawishi uwekezaji ili tuwe na kampuni ya ndani inayozalisha simu janja zenye gharama nafuu ili kuongeza idadi ya watumiaji wa intaneti, hazitakuwa na mambo mengi kama hizi tunazoagiza sasa,” amesema Dk Bakari.