Majanga mikopo ya ujasiriamali nchini

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kuhamasisha wanawake, vijana na wenye ulemavu kujisajili kupitia mfumo mpya wa maombi ya mikopo mtandaoni, Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeonyesha kuwa mikopo hiyo kwa kiwango kikubwa hutumika nje ya malengo.

Ripoti ya utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) 2020/2021 inayotolewa na NBS inaonyesha zaidi ya asilimia 80 ya wanaokopa mikopo hiyo nchini wanaitumia kwa mambo binafsi yasiyorudisha fedha hizo.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa juzi jijini Dar es Salaam imeonyesha asilimia 31.8 ya wanaokopa fedha hizo wanazitumia kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani, asilimia 12.4 kwa ajili ya matibabu, asilimia 13.1 kwa ajili ya ada za shule na asilimia 1.1 kwa ajili ya kufanyia sherehe.

Vilevile, inasema asilimia 11.7 wanatumia fedha hizo kwa ajili ya kulipa kodi ya nyumba au makazi na asilimia 11 kwa matumizi mengine ya nyumbani ambayo hayakufafanuliwa.

Wakopaji wachache waliosalia ndio wanatumia fedha hizo kwa masuala ambayo yamekusudiwa yanayoweza kuzalisha na kupata fedha za kulipa mkopo, kama vile asilimia 26.4 (biashara), kununua vifaa vya kilimo (asilimia 0.5), asilimia 8.5 (pembejeo) na asilimia 1.9 kununua ardhi ambayo hata hivyo inaweza kuwa ya biashara au shughuli nyinginezo.

Ripoti hiyo imetoka kipindi ambacho kuna taarifa za wakopaji wengi kushindwa kurejesha mikopo hiyo ya halmashauri na kuilazimisha Serikali kukuna kichwa kutafuta njia mbadala ya utoaji wake.

Hali hiyo inadhihirishwa na ripoti kadhaa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa zaidi ya miaka mitano ambazo zimekuwa zikieleza ukubwa wa tatizo hilo na kuonyesha mamilioni ya shilingi za umma zinavyoteketea kupitia mikopo hiyo.

Kwa mfano, mikopo ambayo haikurejeshwa mwaka 2015/16 katika halmashauri 76 ilikuwa ni Sh4.7 bilioni, sawa na asilimia 50. Mwaka uliofuata 2016/17 kwenye halmashauri 84 ni Sh5.8 bilioni (asilimia 63) hazikurejeshwa na mwaka 2017/18 ni Sh10.04 bilioni (asilimia 59) ambazo hazikurejeshwa katika halmashauri 90.


Inategemea malengo

Akizungumzia ripoti hiyo, Mtaalamu wa masuala ya kibenki, George Muntu alisema matumizi ya mikopo yanategemea na aina na malengo ya mkopo husika.

“Mikopo inatofautiana, kuna inayotolewa kwa wafanyakazi (personal loan) ambayo haina shida kwa matumizi ya aina yoyote kwa sababu huyu anakatwa kwenye mshahara wake na kuna ile ya wajasiriamali ambayo inapaswa itumike vizuri kuzalisha faida na baadaye kurejesha fedha hizo,” alisema.

“Kwa upande wa wajasiriamali wanaochukua mikopo, inatokea mara nyingi mtu anapunguza kiasi kwenye mkopo na kukipeleka kwenye kitu kingine ambacho ni nje ya malengo ya mkopo,” aliongeza.


Hali duni

Kwa upande wake, Mchumi na Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji Uchumi Nchini (NEEC), Profesa Aurelia Kamuzora alisema hali duni ya maisha ni sababu mojawapo ya watu wengi kutumia mikopo nje ya malengo.

“Pato la chini la wananchi ni sababu mojawapo, mtu anachukua mkopo kwa ajili ya biashara na kufanya ujasiriamali, lakini akirudi nyumbani analazimika kuchukua kiasi kilekile cha mkopo kuhudumia familia ili kukidhi mahitaji yao ya msingi,” alisema.

Profesa Kamuzora alisema tatizo hili pia linachochewa na utamaduni wetu kuwa mara zote baba ndiye mwenye maamuzi ya mwisho, mikopo hii mara nyingi hukopeshwa wanawake. Kwa hiyo unakuta mwanamke anaamrishwa na mume wake kutoa fedha za mkopo kwa ajili ya shughuli za ndani.

Pia alisema kuna “tatizo la uelewa, Tanzania watu wengi hawajui utaratibu wa kukopa na namna ya kutumia mkopo ili usije kuwagharimu baadaye. Nahisi ni wakati muafaka elimu hii kutolewa,” aliongeza.

Mwajuma Buremo, mfanyabiashara na mjasiriamali eneo la Mabibo, Dar es Salaam alisema ingawa makundi maalumu yanapewa kipaumbele kwenye mikopo, wengi hawaitumii kwa usahihi.

“Kwa sasa hivi wajasiriamali wengi wanachukua mikopo yao kwenye ‘microfinance’ na serikalini ambapo makundi maalumu ya vijana, wanawake na watoto wanapewa. Tatizo bado lipo kwenye matumizi, wengi wanafanyia mambo yao tofauti na biashara,” alisema.

“Kuna wakati tuliunda kikundi cha wauzaji wa bidhaa mtandaoni na tulifanikiwa kupata mkopo kutoka halmashauri, lakini mpaka leo tunaoendelea na biashara tumebakia watatu kati ya 15,” alisema.