Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia atangaza bei mpya ya mpunga

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi wa Ifakara, Ulanga, Mlimba na Malinyi kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa CCM Ifakara, Kilombero mkoani Morogoro. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Awali, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliwasilisha pendekezo la kuongezwa kwa bei katika mpunga, akilenga kuondoa madalali

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kuridhia pendekezo la Wizara ya Kilimo la kuongeza bei ya kilo moja ya mpunga kutoka Sh500 hadi Sh900.

Sambamba na hilo, ameitaka Serikali inunue zao hilo kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kuepuka madalali ambao mara nyingi wanawakandamiza wakulima.

Uamuzi huo wa Serikali umeibua furaha kutoka kwa wakulima, wakisema utaondoa changamoto ya masoko kwa upande mmoja, lakini utawafaidisha kutokana na shughuli zao.

Hadi Rais Samia anafikia uamuzio huo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alishawasilisha pendekezo la kuongezwa kwa bei hiyo, akilenga kuondoa madalali.

Rais Samia ametangaza uamuzi huo leo Jumatatu Agosti 6 2024, alipowahutubia wananchi wa Wilaya ya Ifakara mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku sita mkoani humo.

Amesema pamoja na nyongeza ya bei hiyo,  pia Serikali inapaswa kununua mpunga huo kwa wakulima kupitia NFRA.

Walichosema wakulima

Kutokana na uamuzi huo, Meneja wa Ushirika wa Wakulima Wadogo wa Umwagiliaji wa Mpunga (Uwawakuda), Wilbard Olomi amesema ongezeko la bei hiyo litawafanya wakulima wanufaike na shughuli zao.

Olomi amesema, nyongeza ya Sh400 kutoka katika bei ya awali ni karibu nusu yake na kwamba itawaepusha na madalali.

Pia, amesema uamuzi wa Serikali kununua mpunga huo, utawapa wakulima hasa wadogo uhakika wa soko la mazao yao ya kilimo.

“Tumekuwa tukilima na hatimaye kunakosekana soko la uhakika, ndiyo maana tunajikuta tunaishia kuwauzia madalali. Wenzetu wanakwenda kwenye masoko wanayaongezea thamani mazao na wanafaidika,” amesema.

Meneja wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) Kituo cha Dakawa kinachojihusisha na utafiti wa mpunga, Dk Jerome Mghase amesema ongezeko la bei ni fursa kwa wakulima.

Kutokana na ongezeko hilo, alieleza gunia lililokuwa linauzwa kwa Sh70,000 kwa sasa litauzwa kwa Sh90,000 ikiwa ndiyo bei inayoeleweka.

Katika mazingira hayo, ameeleza mkulima atanufaika na kilimo, lakini hata wafanyabiashara hawatapata hasara.

Amesema punguzo hilo litawanufaisha zaidi wale wakulima ambao si wafanyabiashara, kwa maana wanaolima na kuuza shambani.

“Kuna wale ambao huwa wanauziana wenyewe kwa wenyewe na ili auze anasubiri bei ichanganye, pengine hawa hawataguswa maana atasubiri kipindi cha uhaba ndiyo auze,” ameeleza.

Wakati anayaeleza hayo, Rais Samia amewataka viongozi wasiwe sehemu ya wanaowakandamiza wakulima katika ununuzi wa mpunga huo, akisema vitendo hivyo vinavunja haki.

“Tumeweka viongozi ngazi mbalimbali tuwasaidia wananchi, mnapojiingiza kwenye biashara hii na kwenda kunyonya nguvu ya mkulima hufanyi haki, uwe diwani uwe nani kama unafanya biashara hii ya kuongeza kipimo kwenye debe la mkulima hufanyi haki,” amesema.

Sababu ya kauli yake hiyo ni kile alichoeleza, ana taarifa za uwepo wa viongozi ambao nao wanajihusisha na shughuli za biashara hiyo.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Bashe amependekeza kuongezwa kwa bei ya mpunga kutoka Sh500 kwa kilo hadi Sh900.

Siasa na uvamizi maeneo ya hifadhi

Wakati huohuo, Rais Samia amekemea tabia ya uanzishwaji wa vijiji vipya unaofanywa kwa masilahi ya kisiasa, akisema ndiyo inayochochea uvamizi wa maeneo ya hifadhi.

Tabia za uanzishwaji vijiji vipya, amesema aghalabu hufanyika katika nyakati zinapokaribia chaguzi, wagombea wakilenga kunufaika kisiasa.

“Inapokaribia chaguzi hizi hasa madiwani, mtu akiona yuko vibaya upande mwingine wa eneo lake, anakwenda kusogeza watu kuanzisha kijiji.

“Sasa haya ya kuanzisha vijiji bila kujali tunavianzisha maeneo gani, vijiji vingi vilivyoanzishwa ndani ya maeneo ya hifadhi ni kwa ajili ya wanasiasa wameanzisha, iwe ni madiwani iwe wabunge,” amesema.

Pamoja na kwamba wanasiasa hao ndiyo wanaowapeleka wananchi katika maeneo hayo, amesema baadaye wanageuka kuwa watetezi wao, akidai wanapoondolewa kwenye hifadhi wanaona wanaonewa.

“Alafu ni hao hao wanaokuja kusimama kuwatetea watu walioingia ndani ya hifadhi, maana yake hawa wananchi wetu, wanateseka wanapata shida, lakini ulipowapeleka ulikuwa unajua ni eneo la hifadhi,” amesema.

Msisitizo wa Rais Samia ni kukoma kwa tabia hiyo, kwa kuwa inavunja sheria na kuathiri uhifadhi wa ardhi kwa matumizi ya baadaye.

Katika hatua nyingine, amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Angelar Kairuki kulinda maeneo ya hifadhi, badala ya kuacha wananchi wavamie hadi kuweka makazi ya kudumu.

“Mpaka wananchi wanahamia wanajenga, wanajenga shule, kituo cha afya bado mnawaangalia baadaye huko wameshatulia ndiyo aah vijiji wamevamia watoke, hii nayo sio haki,” amesema.

Wanaodai fidia

Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia amewataka wananchi wanaoidai Serikali fidia baada ya kupitiwa na miradi, wasubiri miradi hiyo ikamilike kwanza, kisha utaratibu utafanyika kuhakikisha wanalipwa.

Kinachosababisha uamuzi huo, amesema ni umuhimu wa miradi hiyo kwa wananchi, hivyo Serikali inaona ianze kuitekeleza kwanza kwa manufaa ya wengi ndipo ichakate utaratibu wa fidia.

Mkuu huyo wa nchi ameibuka na hoja hiyo baada ya malalamiko ya wananchi wa wilaya mbalimbali za Mkoa wa Morogoro kudai malipo ya fidia baada ya kupitiwa na mradi wa umeme wa Kihansi yaliyoibuliwa na mbunge wa Mvomero, Aboubakar Assenga.

“Kwa hiyo kwa wale wanaotudai fidia zao kwa maendeleo yao wenyewe tunaomba muwe na subira. Tuacheni tumalize miradi ya maendeleo wananchi wengi wafaidike alafu tutaangalia masuala ya fidia,” amesema Rais Samia.

Katika maelezo yake aligusia uwepo wa baadhi ya watu wanaoweka vikwazo vya utekelezwaji wa miradi husika kwa sababu hawajalipwa fidia.

“Tuacheni tufanye miradi, mambo ya fidia mimi nawahakikishieni hatonyimwa mtu haki yake. Tukiwa tayari tutalipa fidia, kwa hiyo niwaombe sana wananchi achieni miradi ijengwe kwa manufaa yenu fidia itakuja kulipwa,” amesema.

Mchengerwa atoa wiki mbili

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ametaka uchunguzi wa malalamiko ya wananchi kuchangishwa fedha ufanyike.

Uchunguzi huo, unalenga kile alichoeleza, kuna malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Namawala wilayani Kilombero, kuchangishwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mganga wa Halmashauri na Mwalimu.

Lakini, Mchengerwa amesema anazo taarifa kuwa fedha hizo zilizochangwa zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mwenyekiti wa kitongoji.

Kutokana na mazingira hayo, amemwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Dunstan Kyobya afanye uchunguzi na ndani ya wiki mbili awasilishe ripoti kwake.

Kuhusu changamoto za masuala ya ushuru, amesema leo angekutana na uongozi wa mkoa huo kwa ajili ya kujadili namna ya kuelewana.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917