Serikali yaonyeshwa njia kujenga uchumi endelevu
Muktasari:
Serikali yatakiwa kuhakikisha usalama wa chakula na uboreshaji wa lishe katika kupunguza umasikini
Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo, sekta binafsi na asasi za kiraia wametaja maeneo ambayo Serikali inapaswa kuweka nguvu zaidi ili kujenga uchumi endelevu, ikiwamo kuhakikisha usalama wa chakula, uwekezaji katika rasilimali watu na mabadiliko ya tabianchi.
Wamesema hayo leo Februari 09, 2024 kwenye kikao cha majadiliano ya kimkakati ngazi ya wataalamu mwaka 2024 kilichobebwa na kaulimbiu: “Kuelekea Dira ya Maendeleo 2050 kuongeza kasi ya uimara na maendeleo jumuishi.”.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Zlatan Milisic amesema kuhakikisha usalama wa chakula na uboreshaji wa lishe ni muhimu katika kupunguza umasikini na kuwa na nguvu kazi kwa ajili ya kutimiza Dira ya 2050.
Amesema wanatambua nia ya Serikali katika kuboresha usalama wa chakula na upatikanaji wake, hasa katika kuongeza bajeti ya kilimo lakini yapo maeneo yanayopaswa kufanyiwa kazi zaidi.
Milisic amesema ni muhimu kushughulikia upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo na upotevu wa mazao baada ya mavuno kutokana na miundombinu duni ya uhifadhi, uwezo duni wa wakulima kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Amesema wanawake wana jukumu katika kuzalisha chakula na kulisha familia, hivyo ni vyema kuhakikisha sera na programu zinazolenga kutokomeza njaa ziwafikie watu wote.
Milisic amesema mfumo imara wa chakula unahitaji kilimo kinachoendana na mabadiliko ya hali ya hewa, maboresho ya kidijitali, upanuzi wa kimkakati katika uzalishaji wa chakula, uhifadhi, usambazaji, usimamizi wa upotevu wa mazao baada ya mavuno na msaada zaidi kwa wakulima wadogo.
Pia, amesema kunahitajika uwekezaji katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
"Mabadiliko ya hali ya hewa pia ni suala la usawa wa kijinsia, mara nyingi wanawake hutegemea zaidi maliasili ili kujipatia riziki na wako katika hatari zaidi ya majanga ya hali ya hewa kama vile mafuriko, ukame na dhoruba ambazo zimekuwa za mara kwa mara," amesema Milisic.
Katika hatua nyingine, Milisic amesema mwaka 2050 Tanzania itakuwa ni miongoni mwa nchi tatu barani Afrika zenye idadi kubwa ya watu, hivyo ni vyema ikaanza kuwekeza katika rasilimali watu.
"Tunaamini kuwa, Tanzania itaweza kupata maendeleo kamili ya kijamii na kiuchumi ikiwa tutashirikiana kuendeleza rasilimali watu, kwa kuwekeza kwa vijana, kutoa fursa kubwa kwa wanawake na wasichana, kupata elimu na afya bora, kuwa na ujuzi na tija na kuwawezesha wananchi wote kutambua uwezo wao kikamilifu," amesema Milisic.
Mkurugenzi Mkuu wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga mbali na kuunga mkono uwekezaji katika rasilimali watu, mabadiliko ya tabianchi na usalama wa chakula, ametaka uwekezaji zaidi katika nishati.
Amesema ni vyema Serikali ikashughulikia matatizo yaliyopo katika usambazaji wa nishati ili kupunguza matumizi ya nishati mbadala ambayo yanaongeza gharama za uzalishaji.
"Tunatambua jitihada zinazofanywa na Serikali hasa uwekezaji katika sekta hii na tunaamini hii ni moja ya sehemu itakayofanya uchumi wetu kuwa himilivu," amesema Maganga.
Amesema uwekezaji katika teknolojia ni muhimu ili kuendana na mabadiliko makubwa yaliyopo.
"Miundombinu, ufikiwaji na unafuu wa gharama, ni vyema kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha teknolojia inakuwa kipaumbele chetu," amesema Maganga.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO), Lilian Badi amesema upatikanaji wa mikopo nafuu kwa shughuli za kiuchumi za uzalishaji mali bado ni changamoto.
Amesema ni vyema kukabiliana nayo ili ndoto ya maendeleo jumuishi iweze kutimia.
Badi amesema azaki bado zinakabiliwa na changamoto hasa zitokanazo na mifumo, sera na utekelezwaji wa sheria.
"Tunaomba Serikali iangalie upya mifumo, sera na sheria hizo ili kuongeza mchango wa azaki katika kutekeleza maendeleo ya Taifa," amesema Badi.
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu Mwamba amesema maendeleo ya miundombinu ni msingi wa kufungua uwezo wa uzalishaji, kuwezesha biashara na kukuza ukuaji jumuishi nchini.
"Majadiliano yetu yatazingatia uwekezaji mkakati, mfumo wa sera na udhibiti na juhudi za ushirikiano zilizolenga kuboresha mawasiliano, kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu na kutengeneza mazingira yanayowezesha maendeleo endelevu,” amesema Badi.